Ziara ya Rais Jakaya Kikwete kwenye kata ambayo haijawahi kutembelewa na rais yeyote tangu Tanzania ijitawale, juzi ilikuwa ngumu baada ya baadhi ya magari kukwama kwa muda likiwamo na la Mama Salma.
Hali hiyo iliyotokea juzi ilitokana na ubovu wa barabara ambayo ililazimu trekta kutumika kuyakwamua.
Adha hiyo iliyapata magari hayo ambayo yanatumiwa na watu waliopo kwenye ziara ya Rais Kikwete mkoani Tabora.
Rais alikuwa akiendelea na ziara yake akitokea Tabora Mjini kwenda kata ya Kitunda ambayo haijawahi kutembelewa na rais yeyote tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Kutokana na ubovu wa barabara, helikopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ililazimika kuitwa kutoka Tabora mjini kwa ajili ya kwenda kumchukua rais kumpeleka Wilaya ya Sikonge.
Baada ya Rais kumaliza kuhutubia wananchi katika kata hiyo, helikopta hiyo ilitua na kumchukua tena kumrudisha Sikonge.
Aidha, baadhi ya magari yaliyokuwa katika msafara huo nayo yalizama katika madimbwi na kulazimika kuvutwa na trekta.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Kitunda, Rais alifurahishwa na maendeleo ya elimu na kisha akatoa Sh. milioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule katika kata tatu za tarafa ya Kiwelu wilayani Sikonge.