Wakuu
Naomba kujua kama Kunywa mkojo ni salama kiafya?
Naomba kujua kama Kunywa mkojo ni salama kiafya?
- Tunachokijua
- Mdau mmoja wa JamiiForums amedokeza kuwa kumekuwa na wimbi la watu kushauriwa kunywa ama kuoga mkojo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na kuhoji je, suala hili likoje kiafya.
Uhalisia wa madai hayo upoje
JamiiCheck imepitia machapisho na tafiti za afya na kubaini kuwa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuwa kunywa mkojo wa binadamu una faida kiafya.
Tovuti ya UPMC health inabainisha kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa kunywa au kutumia mkojo kwa namna yoyote kuwa una manufaa kiafya.
Kwa mujibu wa ripoti ya kutoka katika jarida la taaluma linalohusu masuala ya magonjwa ya mfumo wa mkojo (Urology) inaeleza kuwa;
"Mengi ya yale tuliyosikia kuhusu matumizi ya tiba ya mkojo hayana msingi wa kitabibu, na ni tiba ya kienyeji ambayo inaweza hata kuzidisha jeraha."
Makala iliyoandikwa katika tovuti ya Web Med na kupitiwa na Kathleem Zelman ambaye ni mtaalamu wa lishe inabainisha kuwa;
"Mkojo ni mchanganyiko wenye chumvi na kemikali ambazo mwili wako unajaribu kuziondoa. Kemikali hizi zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya ikiwa utazitumia.
Zaidi ya hayo, mkojo hauna faida yoyote ya kiafya ambayo haiwezi kupatikana kwa kula vyakula au kunywa vinywaji vingine."
Dkt. Zubair Ahmad aliliambia Shirika la utangazaji la BBC kupitia makala iliyoandaiwa na shirika hilo anaeleza kuwa;
“Watu wengi wanaamini kwamba ikiwa huna matatizo yoyote ya figo, mkojo wako ni safi. Ni sawa maadamu uko ndani ya mwili lakini ukitoka nje unaweza kuambukizwa na bakteria. Kunywa mkojo katika hali kama hiyo kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.”
Anaeleza pia, “Kupitia mkojo tunaondoa uchafu mwilini. Kwa hiyo hakuna msingi wa kisayansi wa kunywa mkojo taka kuwa na manufaa.”