Kumekuwa na mazoea katika jamii mtoto anapoanza kuota meno huanza kuharisha na hivyo kuaminika kuwa meno yanasababisha mtoto kuharisha.
Ukweli ni upi?
Ukweli ni upi?
- Tunachokijua
- Ukuaji wa watoto hupitia hatua nyingi tangu kuzaliwa kwao. Mabadiliko haya huhusisha tabia na namna ambavyo mifumo ya mwili hufanya kazi.
Ukuaji wa watoto huwa haufanani, lakini wengi huanza kuota meno wakiwa na umri wa kati ya miezi 4 hadi 7. Tofauti na jinsi ambavyo wazazi wengi huamini, tendo hili la kiasili huwa sio chanzo cha kuhara kwa mtoto.
Haya yanathibitishwa na chapisho la Pamela DenBesten, lenye kichwa cha habari "Is teething associated with diarrhea?"
Kuhara ni matokeo ya uwepo wa ugonjwa mwingine au uwepo wa mazingira yasiyo salama yanayo mzunguka mtoto kwa wakati huo, hasa yale yenye uchafu.
Ifahamike kuwa wakati huu watoto huwa na hamu ya kula kila kitu pamoja na kusugua fizi zao maana huwasha, hivyo wanaweza kula uchafu wa aina mbalimbali ambao kwa mantiki nyepesi ndiyo huwafanya waanze kuhara.
Dalili za kawaida za kuota kwa meno ni
- Kuvimba na kulainika kwa fizi
- Hasira na kulia
- Kuongezeka kidogo kwa joto la mwili (homa ya kawaida)
- Kulazimisha kula kila kitu
- Kikohozi
- Kusugua fizi
- Kuweweseka
- Kung’ata na kuvuta chuchu wakati wa kunyonya
Kwa kurejea tafiti mbalimbali, maelezo ya wataalam wa afya pamoja na chapisho la Taasisi ya National Health Service (NH), JamiiForums imebaini kuwa Kuharisha ni ugonjwa unaotokana na mtoto kula vitu vichafu, pia sio dalili ya kawaida ya kuota kwa meno.
Watoto wanaopatwa na changamoto hii wanapaswa kupelekwa hospitalini haraka kwa uchunguzi na matibabu.