Exuper Kachenje
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo amesema kuwa kutekeleza suala la mgombea binafsi litawezekana tu endapo uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu utaahirishwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Marmo alisisitiza kuwa ugumu wa kutekelezwa kwa suala hilo unatokana na muda mfupi uliopo kati ya sasa na uchaguzi mkuu ujao iwapo mahakama itatoa hukumu kama ile ya awali kabla ya Oktoba.
Waziri Marmo alisema hayo jana katika mahojiano na gazeti hili kwamba, suala la mgombea binafsi linahitaji muda wa kutosha ili liweze kuingizwa kwenye sheria na taratibu za nchi.
"..Ninachosema mchakato wa kubadili katiba ni mrefu na muda uliopo sasa hautatosha. Jambo hilo la mgombea binafsi litawezekana tu iwapo itatokea uchaguzi ukaahirishwa," alisema Marmo.
Alisema kuwa kimsingi mbali na uwezo wa kutoa uamuzi wa kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi, mahakama haina uwezo wa kufanya mabadiliko ya sheria ili kuwezesha suala hilo.
"Mahakama haina uwezo wa kufanya mabadiliko ya sheria, uamuzi wake kwa mujibu wa taratibu zilizopo, hata ikiamua kuwepo kwa suala hilo basi, kimsingi lazima upitie kwenye mchakato wa kuutekeleza ambao ni kubadili katiba," alisema Marmo.
Marmo ambaye pia ni Mbunge wa Mbulu, mkoani Manyara alifafanua kuwa hata ikiwa uamuzi huo utatolewa na mahakama, lazima suala hilo lipitie katika mchakato ambao ni kubadili katiba ya nchi, taratibu na sheria za uchaguzi.
Waziri Marmo alisema kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa mchakato huo unahitaji muda mrefu na maandalizi ili kuwezesha mabadiliko hayo kufanyika.
"Haitoshi mahakama kutoa uamuzi, lazima uamuzi wake upitie kwenye mchakato, nao ni mabadiliko ya katiba, yanahitaji muda mrefu mchakato wake kukamilika," alisema waziri huyo wa serikali ya awamu nne.
Alisisitiza akisema: "Mgombea binafsi ni suala la kikatiba na kwa mujibu wa utaratibu siyo tu mahakama ikiamua inatekelezwa mara moja, katika hilo lazima mchakato wa kubadili katiba ufanyike nalo linahitaji muda mrefu. Kwa sasa hilo la mgombea binafsi kuwezekana labda uchaguzi mkuu uahirishwe."
Hivi jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa nchini wakiongozwa na Jaji Mkuu, Augustine Ramadhani waliamua kwamba hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya kuruhusu mgombea huru ndiyo inayotambuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Mahakama Kuu iliruhusu mgombea binafsi baada ya mwenyekiti wa chama cha siasa cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila kufungua kesi akidai kuwa sheria za nchi kuhusu haki ya kupiga kura na kupigiwa kura inapingana na katiba ya nchi kutokana na kutamka kuwa mgombea ni lazima apitishwe na chama.
Lakini tangu hukumu hiyo ilipotolewa mwezi Juni, 2006 ikitaka mchakato wa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi ufanyike katika kipindi cha miezi sita, hakuna kilichofanyika na badala yake serikali ilikata rufaa ikipinga mamlaka ya Mahakama Kuu kutafsiri katiba.
Rufaa hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana mbele ya jopo la majaji hao saba wa Mahakama ya Rufaa, lakini serikali iliomba suala hilo liahirishwe kwa muda wa miezi minne ili ijipange kikamilifu.
Akiwasilisha maombi hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu (DAG), George Masaju alisema sababu za maombi yao ni kutokuwepo kwa wakili mwenza anayeshirikiana naye ambaye anaifahamu vizuri kesi hiyo na ambaye anauguliwa na mgonjwa.
Alidai kuwa yeye (DAG) hakupata muda wa kuipitia orodha ya kesi zitakazotumiwa na upande wa utetezi kwa kuwa walichelewa kuipata, akidai kuwa waliipata Jumamosi ambayo ni siku ya mapumziko.
âMheshimiwa Jaji, kama utaridhia naomba shauri hili liahirishwe ili tupate muda wa kuzipitia hoja za upande wa pili ili tuweze kuisaidia mahakama kwa kuwa tuliwapelekea wenzetu List of âAuthoritiesâ (orodha ya kesi za rejea wakati wa usikilizwaji kesi husika) Ijumaa na wenzetu walituletea list of authorities zao Jumamosi,â alisema Masaju. Maelezo hayo yalionekana kumshangaza Jaji Ramadhani na akamuuliza maswali mengi kutokana na kitendo cha serikali ambayo ni mrufani kuchelewa kupeleka orodha hiyo ili nao wapewe orodha ya upande wa pili mapema wakati suala hilo lilikuwa likijulikana kwa muda mrefu.