Kutoka ipcc hadi Udom: Dkt. Chang’a aongoza majadiliano ya mustakabali wa tafiti za tabianchi Tanzania

Kutoka ipcc hadi Udom: Dkt. Chang’a aongoza majadiliano ya mustakabali wa tafiti za tabianchi Tanzania

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
WhatsApp Image 2026-06-17 at 11.22.30.jpeg


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, tarehe 16 Juni 2026 ametembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya TMA na Chuo hicho katika nyanja za elimu, tafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika ziara hiyo, Dkt. Chang’a alikutana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, ambapo viongozi hao walijadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatakayochochea maendeleo ya tafiti, ubadilishanaji wa maarifa na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na uhifadhi wa mazingira.

Baada ya kikao hicho, Dkt. Chang’a alishiriki katika semina yenye mada ya “Climate Change and Meteorological Services Seminar”, iliyolenga kuongeza uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Semina hiyo ilifunguliwa na Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Jamii, Dkt. Zuhura Badru, na kuwakutanisha wanafunzi, wahadhiri, watafiti pamoja na wataalamu mbalimbali kujadili mbinu na mikakati ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua semina hiyo, Dkt. Badru alisema kuwa jukwaa hilo limekuwa fursa muhimu kwa jamii ya watafiti na wataalamu kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu mifumo ya tabianchi duniani, kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa TMA, kupanua maarifa kuhusu masuala ya hali ya hewa pamoja na kufahamu kwa undani huduma na muundo wa utendaji wa mamlaka hiyo.

Akiwasilisha mada yake, Dkt. Chang’a alieleza kuwa jukumu kuu la IPCC ni kufanya tathmini za kina, zenye uwazi na ushirikishwaji wa taarifa za kisayansi, kiufundi na kijamii-kiuchumi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia upatikanaji sahihi wa taarifa kwa watunga sera na wadau mbalimbali duniani.

“Jukumu la IPCC ni kutathmini kwa kina, kwa uwazi na kwa ushirikishwaji taarifa za kisayansi, kiufundi na kijamii zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia maamuzi yanayolenga kukabiliana na changamoto hizi duniani,” alisema Dkt. Chang’a.

Kwa upande wake, Prof. Lokina alisema kuwa ushirikiano kati ya UDOM na TMA utafungua fursa zaidi za tafiti, mafunzo na ubunifu katika masuala ya hali ya hewa na mazingira. Akibainisha kuwa ushirikiano huo utaimarisha uwezo wa watafiti na wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhisho endelevu la changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Semina hiyo ilihitimishwa kwa wito kwa wanafunzi, watafiti na wadau mbalimbali kuendelea kutumia maarifa ya kisayansi na matokeo ya tafiti katika kuibua na kutekeleza suluhisho endelevu litakalosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.
 
Back
Top Bottom