Ilikuwa tarehe 24 December, 2007 nilipopigiwa simu na watu wa mtandao fulani wa simu (nisingependa kuutaja jina) nikitakiwa kwenda kuchukua zawadi ya X-mas kutokana na wao kuniona kama mmoja wa watu waliokuwa wakitumia sana huduma za mtandao wao kila siku. Nilipofika kwenye ofisi zao zilizokuwa ndani ya jengo la Barclays jirani na hotel ya Movenpick (siku hizi Dar es Salaam Serena Hotel) nilikutana na baadhi ya wateja wengine waliokuwa wamefika kuchukua zawadi zao ambazo nakumbuka ilikuwa ni saa ya ukutani yenye nembo yao, wine,pamoja na pipi kadhaa. Pamoja na kwamba hao wateja baada ya kuchukua zawadi zao walikuwa wakiombwa kuchukua kalamu na karatasi ili angalau watoe maoni yao kwa nia ya kuboresha huduma za mtandao huo lakini kiukweli wengi walikuwa wakiondoka bila kuandika maoni yoyote. Mimi niliamua kutumia zaidi ya dakika 45 nikiandika maoni yangu kwa umakini mkubwa. Nakumbuka niliandika maoni ya aina tatu. Baada ya miezi kama miwili nikaona kampuni hiyo iki introduce huduma ambayo ilikuwa ni kila kitu ya kile nilichokuwa nimeandika kwenye maoni yangu. Hiyo huduma pia ikaja kuigwa na kampuni nyingine shindani na hadi leo hii hiyo huduma ipo na naamini inawaingizia hela nzuri kampuni hiyo na hata ile kampuni shindani iliyoiga kwa mwenzie. Nilichojiuliza ni iweje kampuni kwa kutumia maoni niliyoyatoa isinitumie hata ka sms tu ka kuonyesha appreciation yao juu ya hayo maoni yangu waliyofanyia kazi?! Pengine nilikuwa mzembe kwa staili niliyotumia kutoa maoni yale. Lakini pia sipendi kujilaumu kwa uzembe huo.