Chini ya anga tulivu ya pwani ya Tanzania, safu za mawe yaliyosimamishwa katika Makaburi ya Wataalamu wa China zilipambwa kwa mashada mapya ya maua, huku viongozi, wanadiplomasia, na raia wakisimama kimya wakitoa heshima kwa maisha yaliyopotea mbali na nyumbani. Siku ya Qingming ya mwaka huu haikuwa ya heshima tu bali ya kibinaadamu zaidi.
Sherehe hiyo pia iliadhimisha miaka 50 ya kuanza kwa shughuli za biashara za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), reli inayoendelea kubeba bidhaa na hadithi za urafiki kati ya China, Tanzania, na Zambia.
Miongo kadhaa iliyopita, China ilitoa msaada bila masharti, ikituma wataalamu, wahandisi, na wafanyakazi zaidi ya 50,000 Afrika Mashariki. Pamoja na wenzao wa Tanzania na Zambia, walijenga reli iliyopita kwenye milima, mabonde, na nyika, wakishinda changamoto kubwa za vifaa na mazingira.
Matokeo ya juhudi hizo haikuwa miundombinu tu, bali ishara yenye nguvu ya mshikamano miongoni mwa mataifa yanayoendelea.
Hata hivyo, hadithi ya TAZARA haikuwa ya mtu kuwa na malengo makubwa, bali pia ya mtu kujitolea. Wataalamu sabini wa China walipoteza maisha yao wakati wa ujenzi wa reli na miradi inayohusiana na reli hiyo.
Siku ya Jumamosi, watu mashuhuri, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Patrobas Katambi na Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian, walijitokeza kuweka mashada ya maua kwenye makaburi yao, wakiinama kwa heshima kwa mashujaa waliopoteza maisha yao.
"Haya si majina tu," mmoja wa waliohudhuria alinong’ona wakati sherehe ikiendelea. "Ni sehemu ya hadithi yetu."
Katambi aliielezea TAZARA kuwa ni "zaidi ya njia ya reli," akiiita ni ushuhuda hai wa kuheshimiana, kuaminiana, na maono ya pamoja ya maendeleo. Alihimiza watu kuwa na dhamira mpya ya kuhifadhi na kuboresha reli kama njia ya kuwaenzi wale walioijenga.
Chen alitilia mkazo mtazamo huo, akibainisha kuwa reli hii imesafirisha zaidi ya tani milioni 30 za mizigo na zaidi ya watu milioni 40 kwa miaka mingi, na kuifanya kuwa njia muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania, Zambia, na nchi jirani.
"Ni mashujaa waliojenga mnara wa urafiki wa China na Tanzania na China na Afrika," alisema.
Kwa watu wengi nchini Zambia na Tanzania, TAZARA si ishara ya dhahania; bali ni njia ya maisha iliyounganishwa katika historia za watu binafsi na za kitaifa.
Bruno Ching'andu, mkurugenzi mkuu wa TAZARA, aliangazia umuhimu wake kwa uhai wa Zambia wakati wa miaka ya mwanzo ya uhuru.
"Bila reli hii, tungeteseka sana," raia huyo wa Zambia alisema. "Ilitupatia uwezo wa kufika bandari ya Dar es Salaam wakati tulipoihitaji zaidi."
Reli hiyo iliwezesha usafirishaji nje wa shaba, bidhaa za kilimo, na vifaa muhimu, ikisaidia kuleta utulivu wa kiuchumi na kuunganisha jamii. Baada ya muda, pia iliwezesha mawasiliano ya kitamaduni, ikiwaleta watu wa asili tofauti pamoja katika njia yake.
Wazungumzaji katika sherehe hiyo walisisitiza kwamba TAZARA inasimama kama mradi tofauti na miradi mingi ya miundombinu ya zamani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, James Kinyasi Millya, alisisitiza kwamba msaada wa China ulikuja wakati ambapo yenyewe ilikuwa bado inakua.
"Walitupa msaada kama ishara ya urafiki tu," alisema. "Hakuna masharti, hakuna madai, ni mshikamano tu."
Alilinganisha hili na reli za enzi za ukoloni, ambazo mara nyingi zilijengwa ili kunyonya rasilimali badala ya kuwawezesha wakazi wa eneo hilo.
Maafisa walisema, tofauti hiyo, inaendelea kufafanua moyo wa uhusiano wa China na Tanzania hadi leo.
Karibu nusu karne baadaye, TAZARA inaingia katika ukurasa mpya.
Mkataba wa makubaliano uliosainiwa mwaka 2025 unalenga kufufua reli iliyozeeka, kuboresha ufanisi na kurejesha jukumu lake kama njia muhimu ya usafiri wa kikanda. Na ufufuaji huo umeongozwa na kampuni ya ujenzi ya China ya CCECC.
"Ili kuwaenzi wale waliojitolea muhanga, ni lazima tuhakikishe reli hii inaendelea kuhudumia vizazi vijavyo," alisema."
Ushiriki wa China nchini Tanzania pia umepanuka kwa kiasi kikubwa, ukijumuisha miradi mikubwa ya miundombinu na uhusiano unaokua wa kibiashara. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za TAZARA, biashara ya pande mbili ilizidi dola bilioni 10 za Marekani mwaka 2025, ikionesha ushirikiano wa kiuchumi unaoongezeka.
Wakati sherehe ilipokaribia kuanza, hali ilibadilika kutoka maombolezo hadi utulivu. Mashada yaliwekwa kwa upole kwenyea mawe ya kaburi, rangi zake zikionekana waziwazi makaburini – na kukumbusha kwamba kumbukumbu pia zinaweza kurejeshwa upya.
"Kizazi baada ya kizazi kitakumbuka," Millya alisema. "Huu ni urafiki ulioandikwa si tu katika historia, bali katika damu pia."
Miaka hamsini baada ya treni zake za kwanza kuanza kufanya kazi, TAZARA inabaki kuwa zaidi ya chuma na reli inayoenea kote Afrika Mashariki. Ni daraja kati ya mabara, ushuhuda wa kile ambacho mataifa yanaweza kufikia pamoja, na hadithi hai iliyoumbwa na watu wa kawaida waliofanya mambo ya ajabu.
Katika njia zake, mambo ya zamani na yajayo yanaendelea kukutana, yakiongozwa na moyo wa urafiki ambao, kama reli yenyewe, yanadumu.