HAKI NA WAJIBU
Kuwajibika ni haki
Kuwajibika ni haki
Haki na wajibu ni maneno ambayo huenda tumeyasikia mara kwa mara katika harakati za kutafuta maslahi katika sehemu za kazi na vibarua au jina lolote linalomaanisha sehemu ambayo watu hufanya kazi ili kujipatia chochote kitu cha kujimimu na maisha haya ya kila siku waungwana wanasema kinachofanya walau mkono uende kinywani. Huko basi, tumeyasikia sana maneno haya, wengine wakijua maana, wengine wakifuata wengine wakijua maana, wengine wakifuata mkumbo wa jamii kulingana na mazoea yaliyo katika jamii Husika na wengine wakiwa hawajui maana ya maneno haya.
Katika makala hii ningependa ndugu wasomaji tufahamu kwa pamoja maana ya maneno haya mawili na hatimaye la tatu,”uwajibikaji” Nikianza na neno haki, haki maana yake ni kitu (kiwe cha kushikika au kutoshikika) anachostahili mtu kukipata iwe ni kwa kuwa mzaliwa na kuwa mwanajamii wa jamii husika, kwa kufuata utaratibu wa kuwa mwanajumuiya ya mahali husika,pia haki inaweza kuwa malipo anayopatiwa mtu baada ya kufanya kazi kama inavyoelezwa katika mkataba Husika kati ya mfanyaji kazi na mwajiri wa kazi Husika. Mfano wa baadhi ya haki za Mtanzania ni haki ya kuishi kwa amani na kulindwa na vyombo vya usalama vilivyopo nchini,haki ya kupiga kura kuchagua viongozi wa ngazi Husika kila mwananchi kwa eneno analoishi. Haki nyingine ni kila mwajiriwa wa serikali ama sekta binafsi ana haki ya kupita malipo yake kila mwisho wa mwezi au kila baada ya muda waliokubaliana na mwajiri wa taasisi Husika, kwa taasisi zote za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za afya,usafiri na (au)malazi,waajiriwa hao wana haki ya kupokea na kufaidika na huduma hizo kama inavoonesha kwenye mkataba Husika. Maneno mengine yenye maana sawa na haki ni stahiki,maslahi.
Wajibu kwa upande mwingine ni hali au ukweli wa kuwa na jukumu la kukabiliana na kitu au kuwa na udhibiti wa mtu inayojumuisha yote anayotakiwa kufanya mtu kwa nafasi husika iwe ni kwa maneno matendo kulingana na ama makubaliano ya jamii husika au makubaliano ya pande mbili yote iwe ni kwa mujibu wa sheria,maadili ya sehemu husika kimila au kidini na kadhalika.Kwa Mfano ni wajibu wa kila mwananchi wa Tanzania kutunza mazingira na na viumbe hai vinavyomzunguka. Niwajibu wa baba kulinda na kuihudumia familia yake,ni wajibu wa mama kusaidiana na baba katika hilo, vilevile ni wajibu wa watoto kuwatii na kuwaheshimu wazazi wao, kusoma kwa bidii. Uwajibikajikaji ni kitendo cha kutimiza wajibu.
Mara nyingi haki imekua ikiongelewa sana kuliko wajibu, maneno kama pambana, jiongeze, chakarika, jishughulishe piga kazi yalikua ni machache ukilingnisha na maneno “haki yetu”, maslahi, stahiki, migomo mingi imekua ikisababishwa na watu kutopata haki zao. Hali ilibadilika kidogo mara Tanzania ilipopata Rais wake wa awamu ya tano, hayati Daktari John Joseph Pombe Magufuli, ambaye sera yake ililenga sana vijana na wananchi kwa ujumla wajikite zaidi kufanya kazi kwa bidii akiwa na kauli mbiu yake, ”HAPA KAZI TU” hii ilisaidia sana kuleta hamasa kwa wananchi kujikita katika kujishughulisha katika nyanja mbalimbali ili kuljiletea maendeleo mfano wahitimu walijikita sana katika kujiajiri kuliko kusubiri kuajiriwa, waajiri na waajiriwa hasa wa serikali kuhakikisha kutimiza majukumu yao kwa ubora zaidi kwani alihakikisha kua mwenye kuwajibika atapata haki yake na asiyefanya hivyo atapata alichostahili kulingana na sheria, machinga walilipia kiasi kidogo kufanya biashara na kadhalika. Tulishuhudia pia miradi mingi ya kiserikali ikisimamiwa ipasavyo na kufanyika kwa ufanisi na kumalizika kwa wakati muafaka hii iliwaongezea wananchi imani juu ya serikali yao na hata kupunguza malalamiko. Huu kwa upande wangu ni mfano hai unaoendana na sentensi yangu ya makala hii “Kuwajibika ni haki”.
Kwa mfano huo hai kwa hayati Rais wa awamu ya tano ni wazi kwamba haki inaenda sambamba na uwajibikaji ama wajibu kwani uwajibikaji ni moja ya nguzo muhimu sana katika maendeleo (yo)yote duniani kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi, familia,jamii na taifa kwa ujumla. Kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja ni kitu cha kawaida sana watu kupanga mipango mipya ya maendeleo kiafya na hasahasa kiuchumi kila sikukuu za mwisho wa mwaka kuelekea mwaka mpya ili kuanza upya mwanzoni mwa mwaka na hata kufikia malengo hayo kwa mwaka unaoanza. Mipango hii mingi hasa kwa vijana na wanafunzi huwa haitimii na michache huishia nusu au kufanikiwa kwa kiasi kidogo sana.
Sababu kubwa ya kutofanikiwa kwa mipango hii huwa ni kutokuwajibika kwa mtu binafsi katika mikakati na malengo aliyojiwekea, kuahirisha mambo limekua changamoto kubwa sana katika kufanya swala la uwajibikaji kutumia, pia msukumo rika una mchango mkubwa sana katika kufanya uwajibikaji kuwa mdogo hasa kwa vijana, kwani huwapa vijana msukumo wa kutaka kufanana na wengine na kukubalika katika makundi fulani fulani katika jamii na marafiki na hivyo kutowajibika katika malengo, mipango na mikakati yao waliyojiwekea.
Katika ngazi ya familia wazazi wasipowajibika kuwalea Watoto katika misingi mizuri ya kimaadili na kiimani watasababisha Watoto kuingia katika imani zisizo nzuri na kusababisha wimbi la kuporomoka kwa maadili katika jamii husika. Watoto vilevile wasipowajibika kusoma kwa bidii itapelekea kuwa na jamii iliyikosa elimu na ujuzi wa mambo muhimu hivyo kuwa na kizazi kisichoendana na kasi ya maendeleo kidunia.
Uwajibikaji una athari chanya katika kila eneo la maisha ya mwanadamu ya kila siku iwe ni mahusiano, ambayo haya yanaweza kuwa ni ya mtu binafsi na Mungu(kiimani), mahusiano ya mtu na mpenzi wake, mahusiano ya Kifamilia, mahusiano ya wafanyakazi na wafanyakazi wenzao, mahusiano ya wafanyakazi na waajiri wao, mahusiano ya viongozi wa ngazi Husika na watu husika wanaoowaongoza. Kama kila mtu akiwajibika katika nafasi yake kila mtu atapata haki yake. Kuwajibika ni haki.
Attachments
Upvote
1