CCM inapata uoga gani kama mpinzania atazungumza na balozi? Mbona wapinzani wamekuwa wanatoa maoni yao kwenye mitandao na hata kweye TV ambazo zinaonekana cuniani kote?
Mnyika si alizungumza wiki iliyopita tu akaelezea jinsi Chadema wanavyoona kwamba wanaonewa na mambo mengine mengi? Kwani mabalozi hawawaezi kuona hayo wakajua wapinzania wanavyosema? Kukutana na mpinzani kuna athari gani?
Na kama Maalim Seif ni rafiki na huyo kaimu balozi, hawaruhusiwi kuzungumza wawili wakiwa nyumbani kwa Maalim Seif? Mbona inaonekana kama kila atakachofanya mpinzani "kinatutiwa mbinu" ya kukigeuza kiwe ni kama jinai?
Nawaombeni sana nyie viongozi wa Chama Tawala hapa Tanzania, Kumbukeni kwamba hata panya akiona amezidiwa na mtu anayemwinda huwa huyo panya anamrukia huyo mtu amng'ate ili ashituke aachane naye.
Kumbukeni kwamba hata yaliyotokea kule Soweto Afrika Kusini yalihusisha watoto wadogi kabisa wa shule za msingi lakini kwa vile walivyokuwa wamechoka kuona wanaonewa walifika mahali wakasema afadhali wapigwe risasi wafe kuliko kukaa kimya wakiwa wanaonewa.
Nawaombeni Chama Tawala mtambue kwamba kama itafika mahali wapinzania waseme 'liwalo na liwe' hakuna atakayeweza kuzima huo moto. Na waathirika wakubwa watakuwa ni viongozi wenu.
Mnaweza kuwa mnadhani kwa vile Watanzania "wamezoea kuishi kwa amani" hawataweza kufanya jambo la kuvunja amani. Lakini, hali ya maisha hapa Tanzania ni ngumu sana kwa sasa. Watanzania wengi (asilimia sitini au zaidi) ni vijana, na vijana wana mihemuko.
Wengi hawana ajira hata wale ambao walisoma wakitegemea kupata ajira. Hawana mitaji ya kuanza ujasiriamali wala kufanya kilimo. Kwa hivyo, nawaomba sana, tena sana, viongozi wa CCM, mtambue kwamba you are sitting on a time bomb (mnakalia bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote).
Nawaomba mbadilike katika namna yenu ya kufikiri. Pamoja na kujenga miradi mikubwa kama Stieglers, reli ya kisasa na kuwa na ndege nyingi, vijana hao watafurahi lakini kama wao hawafiadi na hiyo miradi bado mioyoni mwao hawatakuwa na furaha. Ni rahisi sana vijana kama hao kutumiwa kisiasa kusababisha amani ya nchi ipotee kabisa.
Tunamwomba Mungu hilo lisitokee. Lakini na nyie viongozi wa chama tawala, tafuteni mbinu za kuzalisha ajira nyingi kwa vijana na kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja wakati uchumi wa taifa unapanda kama sasa.
Mungu ibariki Tanzania.