Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Nimemsikiliza Katibu wa Itikadi, uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi akihojiwa na mtangazaji Edwin Odemba Septemba 5, 2026 na kubaini kuwa, CCM ina wakati mgumu kujibu maswali magumu ya Watanzania kutokana na hali ya siasa inavyoendelea nchini.
Maswali ya Odemba yalijikita katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 ambao uligubikwa na vurugu zilizosababisha mauaji, watu kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Maswali mengine yalikuwa kuhusu utekaji na watu kupotea hususani tukio la kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kufukuzwa kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Dj Emmanuel Nchimbi na kama CCM bado inakubalika kwa wananchi.
CCM bado inapendwa na wananchi?
Kihongosi alijenga hoja kwamba CCM inakubalika kwa wananchi kwa kurejea mikutano ya kampeni; ushindi wa Samia wa zaidi ya asilimia 97; utekelezaji wa miradi kama SGR, Bwawa la Julius Nyerere na Daraja la Kigongo-Busisi; na ukweli kwamba sehemu ya wapiga kura wa CHADEMA walienda kupiga kura na kukichagua CCM baada ya CHADEMA kutoshiriki uchaguzi.
Lakini ushindi wa asilimia 97 si ushahidi wa kutosha peke yake wa “kupendwa” na wananchi. Kwa sababu mazingira ambayo uchaguzi ulifanyika nayo yanapaswa kuchunguzwa.
Kwa mfano, chama kikuu cha upinzani CHADEMA haikushiriki uchaguzi wa urais, kulikuwa na vurugu; kulikuwa na malalamiko kuhusu mfumo wa uchaguzi; kulikuwa na mazingira ya kisiasa yaliyokuwa na mgogoro.
Kwa hiyo, asilimia 97 inaweza kutumika kama matokeo rasmi ya uchaguzi, lakini si lazima itafsiriwe moja kwa moja kuwa asilimia 97 ya Watanzania wanaipenda CCM.
Hii ni tofauti muhimu kati ya: “CCM ilipata asilimia 97 ya kura” na “asilimia 97 ya Watanzania wanaipenda CCM.”
Hata hivyo, Kihongosi anapaswa kujua kwamba uhudhuria mikutano ya kampeni si kipimo cha moja kwa moja kwamba chama kinasikiliza wananchi. Mkutano mkubwa unaweza kuonyesha umaarufu au uwezo wa kuhamasisha watu, lakini haujibu maswali kama; Serikali imesikiliza malalamiko gani ya wananchi? Ni mapendekezo gani ya wananchi yaliyotekelezwa? Kwa nini kulikuwa na madai makubwa ya mabadiliko ya Katiba? Kwa nini vyama vya upinzani vilikuwa na malalamiko kuhusu uchaguzi? Kwa nini sehemu ya wananchi iliona mfumo wa uchaguzi hauna usawa?
Isitoshe, mikutano mingi ya CCM hutegemea kukusanya watu kwa kuwasomba kwa magari yakiwamo malori, vinginevyo, wananchi hawawezi kuja bila kukusanywa.
Vilevile, kama mitandao ya jamii sio kipimo cha hasira ya wananchi, kwa nini intaneti ilizimwa wakati wa uchaguzi kwa siku sita?
Damu ya Watanzania iliyomwagika Oktoba 29 iko mikononi mwa CCM?”
Alipoulizwa swali hili, Kihongosi alikanusha akijenga hoja yake kuwa CCM haikuchukua silaha na kumdhuru mtu yeyote, na kwamba suala la nani aliyehusika na vifo linapaswa kuachwa kwa vyombo vya uchunguzi na tume zilizoundwa.
Lakini kuna tofauti muhimu kati ya uwajibikaji wa moja kwa moja na uwajibikaji wa kisiasa/kiserikali.
Ni kweli kwamba kusema “CCM iliua watu” ni tuhuma nzito ambayo haiwezi kuthibitishwa kwa kusema tu chama tawala ndicho kilichokuwa madarakani. Ikiwa watu waliuawa wakati wa uchaguzi, nani alikuwa na wajibu wa kuhakikisha usalama wao?
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2025- 2030 inasemaje kuhusu usalama wa wananchi?
Kwa hiyo, hata kama CCM haikubeba silaha moja kwa moja, bado kuna swali la uwajibikaji wa Serikali, amri zilizotolewa, matumizi ya nguvu, chain of command na hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama.
Nani aliua wananchi?
Hili ni swali ambalo Odemba alirudia kwa msisitizo na Kihongosi alisema hawezi kusema nani aliua kwa sababu uchunguzi ulikuwa ukiendelea.
Alirejea Tume ya Jaji Chande na tume nyingine iliyoundwa kuchunguza wahusika na akasema ni vizuri kusubiri majibu ya uchunguzi. Pia alikiri kwamba CCM inaamini Watanzania waliuawa kwa sababu taarifa ya Tume ya Jaji Chande ilisema hivyo.
Kwa nini chama tawala hakiwezi kuwa na msimamo mkali zaidi wa kutaka ukweli ujulikane na wahusika wawajibishwe?
Kihongosi alitumia mara kadhaa kauli ya: “Tusubiri tume.” Hii inaweza kutafsiriwa kama kuahirisha uwajibikaji hadi matokeo ya uchunguzi yatoke.
Tatizo zaidi ni kwamba Serikali yenyewe ndiyo iliyounda mifumo ya uchunguzi. Hivyo swali la msingi linabaki:
Je, uchunguzi huo una uhuru wa kutosha kiasi gani kuweza kuwawajibisha hata wale walio ndani ya Serikali au vyombo vya dola?
Tukumbuke pia, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM alipowahutubia wazee wa Dar es Salaam Desemba 2, 2025 alisema, nguvu iliyotumika kukabili maandamano yale ilistahili, kwani isingetumika waandamanaji wangepindua Serikali.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose Migiro alipohojiwa na televisheni ya Crown, akiwapongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi iliyotukuka Oktoba 29, 2025.
Soma pia: Asha-Rose Migiro: Vyombo vya Ulinzi vilifanya kazi ya kutukuka Oktoba 29 kwa Taifa letu
Yuko wapi Dk Emmanuel Nchimbi?
Hili lilikuwa swali lenye uzito mkubwa kutokana na kujiuzulu kwake, lakini Kihongosi alisema: “Mimi binafsi sijui yuko wapi lakini naamini yupo.”
Alipoulizwa kama amefanya jitihada za kumtafuta, alisema hajafanya hivyo kwa sababu hajaona sababu ya kufanya hivyo.
Hili ni mojawapo ya majibu yenye utata zaidi katika mahojiano. Kwa upande mmoja: Nchimbi ni raia na ana haki ya faragha. Si lazima Katibu wa Itikadi wa CCM ajue kila hatua anayochukua.
Lakini upande mwingine, Nchimbi hakuwa mwanachama wa kawaida tu, bali alikuwa Makamu wa Rais; Katibu Mkuu wa CCM; kiongozi aliyekuwa na nafasi kubwa ndani ya Serikali na chama; na alitangaza kujiuzulu na kustaafu siasa katika mazingira ambayo yameibua maswali mengi.
Kwa hiyo kauli ya: “Sijui yuko wapi… na sijafanya jitihada za kumtafuta kwa sababu sijaona sababu” inaacha pengo kubwa la kisiasa na mawasiliano.
Kwa chama ambacho Nchimbi alikuwa mmoja wa viongozi wake wakuu, wananchi wanaweza kuuliza:Kwa nini chama hakikuona umuhimu wa kujua hali ya kiongozi wake wa zamani baada ya tukio kubwa la kisiasa?
Je, Nchimbi aliitwa Kamati ya Maadili?
Ikumbukwe kwamba, Kihongosi akihojiwa na Clouds TV Agosti 19 alikanusha Dk Nchimbi kuitwa kwenye kamati ya Maadili ya CCM, akisema “Hapana, mpaka sasa wewe umeona kuna taarifa yoyote kwamba ameitwa? Lakini rumours zinasema hivyo. Kama ataitwa mimi siwezi kujua either anaweza kupokea barua ya wito na sijui kama amepewa barua.”
Lakini alipohojiwa na Chief Odemba, lithibitisha kwamba Nchimbi aliitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM kama mwanachama wa chama, si kama Makamu wa Rais.
Pia alisema, sababu za kuitwa kwake ni za siri; Nchimbi alifahamu sababu hizo; CCM ilifuata taratibu zake; hatimaye Nchimbi alifukuzwa CCM; Kihongosi mwenyewe alishiriki katika maamuzi hayo na akasema aliunga mkono kufukuzwa kwake kwa asilimia 100.
Hata hivyo, Kihongosi anasema: Nchimbi hakufukuzwa kwa sababu ya kujiuzulu. Lakini swali kubwa linabaki “Ni kosa gani hasa lililomfanya afukuzwe?”
Je, alifukuzwa kwa sababu ya kudai Katiba Mpya?
Kihongosi alikataa hoja hiyo. Alisema Katiba Mpya ipo ndani ya Ilani ya CCM na kwamba viongozi wanapaswa kutekeleza ilani hiyo badala ya kuhamasisha wananchi “kupigania” Katiba Mpya.
Kama CCM imeweka Katiba Mpya kwenye Ilani yake, basi kumtaka mwanachama au kiongozi aunge mkono utekelezaji wa Katiba Mpya si jambo linalopingana na sera ya chama.
Swali linakuwa:
Tatizo lilikuwa nini katika kauli ya Nchimbi?
Je, tatizo lilikuwa, namna alivyosema? Muda aliousema? Mahali aliposema? Au alikuwa akitaka mchakato ufanyike kwa kasi tofauti na uamuzi wa chama?
Hilo Kihongosi hakulifafanua kikamilifu.
Nani alimteka Humphrey Polepole?
Hili ni swali jingine ambalo Kihongosi hakutoa jina la mhusika. Alisema CCM ilisikitishwa sana na tukio hilo na kwamba chama kilielekeza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi. Pia alisema CCM inatamani Polepole apatikane akiwa hai na kwamba vyombo vya usalama vinaendelea na kazi hiyo.
Hapa kuna tatizo kubwa la uwajibikaji. Tukio la Polepole linahusisha madai mazito ya mtu kuchukuliwa kwa nguvu na watu wasiojulikana.
Kwa hiyo swali si tu: “Uchunguzi unaendelea? Bali “Uchunguzi umefikia wapi?”
Kingine cha kujiuliza, kama kweli CC ilisikitishwa sana, “Kwa nini baada ya muda wote huu hakuna taarifa ya wazi kwa familia na umma?”
Kwa nini mamlaka ya Rais yapunguzwe?
Kihongosi alipinga pendekezo la kupunguza mamlaka ya Rais. Hoja yake ni kwamba Rais ndiye Mkuu wa Nchi na kiongozi namba moja; hivyo kupunguza mamlaka yake kunaweza kuathiri uwezo wa nchi kuendeshwa.
Hapa ndipo mjadala wa Katiba Mpya na separation of powers unapoingia.
Tatizo la hoja ya Kihongosi ni kwamba: kuwa Mkuu wa Nchi si sawa na kuwa na mamlaka yasiyo na mipaka.
Katiba inaweza kumpa Rais mamlaka makubwa huku ikiweka, checks and balances; uhuru wa Bunge; uhuru wa Mahakama; taasisi huru; mfumo wa uteuzi wenye uwajibikaji; ukomo wa baadhi ya mamlaka ya kiutendaji.
Kwa hiyo swali la msingi si: “Tumpunguzie Rais kwa nini?” Bali: “Ni mamlaka gani ya Rais yanapaswa kubaki, yapi yapunguzwe na yapi yadhibitiwe?”
Hilo ni swali la kikatiba, si suala la kama mtu anamwamini Rais au la.
Na hoja kwamba “ukimpunguzia Rais mamlaka nchi haitaenda” inahitaji ushahidi. Nchi nyingi duniani zina marais wenye mamlaka yaliyodhibitiwa na bado zinafanya kazi.
Kwa majibu haya ya Kihongosi, ni wazi kwamba CCM ina wakati mgumu wa kujieleza mbele ya wananchi na kwa kuwa kiongozi huyo amekuwa akiomba mdahali na viongozi wa CHADEMA, huenda akapata wakati mgumu Zaidi iwapo mdahalo huo utafanyika.