Kwa mara nyingine diplomasia ya China yaleta utofauti Mashariki ya Kati

Kwa mara nyingine diplomasia ya China yaleta utofauti Mashariki ya Kati

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
VCG41165595505.jpg

Katika wiki za hivi karibuni China imefanya jambo kubwa la kidiplomasia kwa kuyawezesha makundi 14 ya kisiasa ya Palestina, kukaa kwenye meza ya duara na kujadili mustakbali wa uwakilishi wa watu wa Palestina, na makundi yote hasimu yamefikia maafikiano na kusaini makubaliano, yakiondoka Beijing yakiwa kitu kimoja. Hii ni mara nyingine tena kwa China kutoa mchango chanya kwenye kutafuta utulivu katika eneo la mashariki ya kati baada ya kusaidia kurudisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia.

Hii ni mara nyingine tena kwa mahasimu kukutana Beijing, kufanya mkutano wa pamoja na kuondoka na matokeo ambayo yanaashiria kuondoa tofauti kwa njia ya amani. Kwa wanaofuatilia suala la Palestina, mbali na mgogoro unaoendelea sasa kati ya Israel na kundi la Hamas, kuna mivutano na mgawanyiko mkubwa katika ya makundi mbalimbali ya Palestina hali ambayo imedhoofisha uwezo wa watu wa Palestina kuwa na sauti moja kwenye kukabiliana na ukaliaji wa ardhi yao.

Wakati baadhi ya nchi za magharibi zimekuwa zikipuuza ukaliaji na ukandamizaji wa Palestina, na hata wakati Israel inafanya mashambulizi dhidi ya watu wa ukanda wa Gaza, China kwa upande mwingine imekuwa ikihimiza amani na usalama kwa watu wa Israel na wa Palestina. Hata hivyo kumekuwa na changamoto nyingi kwa watu wa Palestina kuwa na sauti moja, kutokana na mgawanyiko mkubwa uliopo kati yao.

China inatambua kuwa mgogoro wa Palestina hauwezi kutatuliwa kikamilifu kama hakutakuwa na umoja miongoni mwa wapalestina. Ndio maana baada ya mkutano ulioyakutanisha makundi 14 ya Palestina mjini Beijing na kufikia makubaliano, Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi alisema matokeo ya msingi ni kwamba chama cha Ukombozi wa watu wa Palestina, PLO, ndiye mwakilishi halali wa watu wote wa Palestina, na kwamba baada ya mgogoro wa sasa kukomeshwa kutakuwa na serikali ya muda ya maridhiano ya kitaifa.

Wachambuzi wa maswala ya kisasa wanaona kuwa China ina mwelekeo tofauti kabisa na ule wa baadhi ya nchi za magharibi, hasa Marekani, wa kutatua changamoto ngumu za amani na usalama. Marekani kwa mfano imekuwa inapendelea zaidi matumizi ya mabavu, vikwazo na hata vitisho, kama ilivyofanya kwa Somalia, Iraq, Afghanistan, Pakistan na Libya, na inavyoendelea kufanya sasa kwenye mgogoro kati ya Israel na kundi la Hamas, na katika nchi zote matokeo yamekuwa ni majanga. Mara nyingi mwisho wa matumizi ya njia ya mabavu kutatua changamoto moto, ni msingi wa mabavu mengine na mwanzo wa msukosuko wa kibinadamu.

Licha ya kuwa ni mapema sana kutaja matokeo ya makubaliano kati ya makundi ya Palestina yatakuwa vipi baada ya mgogoro wa sasa wa Palestina kumalizika, ni wazi kuwa diplomasia ya China ya kuwaweka pamoja mahasimu kujadili na kutatua tofauti zao, ni njia inayoweka misngi wa kuleta amani endelevu. Mfano ulio wazi ni ule wa uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia, nchi hizo sasa zimeboresha uhusiano kati yao na sintofahamu iliyokuwepo sasa haipo tena. Juhudi kama hizo zinaonekana tena kwenye mgogoro kati ya Russia na Ukraine.
 
Back
Top Bottom