Rugemeleza
JF-Expert Member
- Oct 26, 2009
- 668
- 136
Hii makala imekaa kisomi na ni jibu la wale wasiowapenda watoto wetu.
Kwa nini elimu bure inawezekana?
Dk. Kitila Mkumbo
Dk. Kitila Mkumbo
TANGU kuanza kwa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010, kumekuwa na mjadala mahsusi kuhusu sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha sita.
Sera hii imepingwa na kuzomewa vikali na Chama cha Mapinduzi (CCM). Binafsi awali sikutilia manani upinzani wa kutoa elimu bure kwa sababu ulitolewa na Kampeni Meneja wa chama hicho, Abdulrahmani Kinana, nikidhani kwamba alifanya hivyo kwa sababu za kisiasa na kipropaganda ukizingatia kwamba vyama vya siasa viko katika ushindani mkubwa wa kuomba ridhaa ya wapiga kura.
Hata hivyo, nimeanza kutilia manani upinzani huu baada ya Rais Jakaya Kikwete naye kujitokeza hadharani kupinga sera hii na kuungwa mkono na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta. Upinzani wa sera hii kutoka kwa viongozi hawa wakuu katika nchi yetu umetia uzito wa kipekee hoja ya kwamba elimu bure haiwezekani kutolewa katika nchi maskini kama Tanzania.
Bila kufafanua dhana ya kutoa elimu bure na uwezekano wake, wananchi wataanza kuamini kwamba hili ni jambo lisilowezekana hasa watapoambiwa na viongozi wa chama tawaka na serikali yake. Ufafanuzi huu ni muhimu ukizingatia kuwa tupo katika jamii ambayo imejengwa katika mfumo wa kipropaganda wa kuamini au kuaminishwa kuwa chochote kinachosemwa na viongozi wa serikali na chama tawala kuwa ni kweli.
Aidha bado kuna watu katika jamii yetu ambao hutilia shaka chochote kinachosemwa na viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati wengine, bila kuzingatia mantiki ya hoja.
Pengine kabla ya kufafanua juu ya uwezekano wa kutoa elimu bure, ni vizuri kuweka kumbukumbu sawa. CCM wana historia ya kupinga sera zenye kujaribu kuwapunguzia wananchi makali ya maisha, na hawajaanza na hili la elimu bure.
Itakumbukwa kuwa mwaka 1995 wapinzani waliahidi kufuta kodi ya kichwa (CCM waliita kodi ya maendeleo) ambayo ilikuwa inaleta adha kubwa kwa wananchi hadi wengine kufikia hatua ya kujificha porini ili wasikamatwe na askari mgambo.
CCM walipinga vikali sera hii wakisema kuwa haiwezekani kuendesha serikali bila kodi hiyo. Hata hivyo, baada ya uchaguzi mkuu wa 1995 serikali ya CCM iliifuta kodi hii, aghalabu kwa shinikizo.
Mwaka 2000 wapinzani walikuja na sera ya kufuta ada katika shule za msingi kama njia ya kuwawezesha watoto wengi zaidi kujiunga na elimu ya msingi. Kama kawaida yao, CCM walicharuka tena wakidai kuwa wapinzani wanaota ndoto.
Hata hivyo baada ya uchaguzi wa 2000 ada katika shule za msingi ilifutwa, japokuwa kwa shinikizo kubwa la Benki ya Dunia. Kwa hiyo, kwamba CCM leo hii wanapinga vikali tena bila aibu sera ya elimu bure sio jambo la kustaajabu.
Pengine jambo pekee la kustajaabu ni kwamba wapinzani wa sera ya elimu bure ni viongozi wa chama kinachojiita cha kijamaa. Haingii akilini hata kidogo kwa kiongozi wa chama kinachojiita cha ujamaa kupinga sera ya kutoa elimu bure. Msingi wa ujamaa ni usawa na fursa kwa wote.
Wana ujamaa popote walipo wanakubaliana kwamba njia rahisi ya kufikia usawa na kutoa fursa kwa kila mtu ni kuhakikisha kwamba elimu na huduma zingine za jamii zinamfikia kila mtu. Ili kutimiza hili, wana ujamaa wanakubaliana pia kwamba ni muhimu na lazima kwa huduma hizi kugharamiwa na serikali bila wananchi kuzilipia moja kwa moja.
Hii ni mantiki ya msingi ya ujamaa ambayo mwanachama wa kawaida wa chama kinachojiita cha kijamaa anapaswa kuielewa, achilia mbali kiongozi wake.
Wapinzani wa sera ya kutoa elimu bure wametumia kigezo cha gharama katika kuhalalisha upinzani wao. Kwamba haiwezekani kutoa elimu bure kwa sababu kufanya hivyo itamaanisha serikali iache kutekeleza majukumu mengine ya msingi.
Katika makala hii ninaonyesha kwa ufupi sana jinsi ambavyo inawezekana kwa serikali kulipia gharama ya elimu kwa kutumia fedha za walipa kodi bila kumbebesha mzazi gharama za ziada.
Katika kufanya hivi nitaenda hatua kwa hatua, nikianzia na kufafanua dhana ya elimu bure kwa mazingira ya Tanzania, na kubainisha vyanzo mbadala vya mapato kwa serikali ili iweze kulipia kikamilifu gharama za elimu na huduma zingine za jamii. Elimu bure maana yake ni nini?
Watu wengi wanaopinga mpango wa CHADEMA wa kutoa elimu bure wamefanya hivyo bila kuelewa sawasawa nini hasa mantiki yake katika mazingira ya Tanzania. Nitafafanua.
CHADEMA inapoongelea kutoa elimu bure inamaanisha kufuta ada zote wanazotozwa wazazi katika shule za sekondari. Tayari wanafunzi wa shule za msingi hawalipi ada na kwa hivyo kinadharia elimu ya msingi inatolewa bure Tanzania. Hivyo basi, katika kujibu swali la je inawezekana kutoa elimu bure ni muhimu kukokotoa mahesabu ya ada wanazolipa wanafunzi.
Hii itatupa picha halisi ya fedha ngapi zinakusanywa kwa malipo ya ada na ni kiasi gani cha mapato serikali itapoteza kwa kufuta ada hizo. Ukishamaliza kukutoa katika hatua hii ni muhimu vilevile kuonyesha vyanzo vya mapato mbadala vitakavyoziba pengo hili. Katika aya zifuatazo nitajaribu kukokotoa mahesabu haya.
Ada ya shule ya sekondari kwa sasa ni shilingi 20,000/= kwa shule za kutwa na shilingi 70,000/= kwa shule za bweni. Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 35 ya wanafunzi wa sekondari wanaacha shule kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kwa wazazi wao kushindwa kulipa ada.
Kuna taarifa kutoka baadhi ya wilaya ambapo wazazi na walezi waliwashauri watoto wao wasifanye vizuri katika mitihani ya darasa la saba ili wasiingie katika matatizo ya kulipa ada kwa kuwa hawana uwezo. Hiyo ndiyo athari ya ada katika shule za sekondari hapa nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo za mwaka 2010, idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari za serikali ni 1,401,330. Katika shule zaidi ya 2000 nchi nzima, shule za bweni zipo 170 zenye wanafunzi wasiozidi 120,000.
Hii inamaanisha kuwa kwa mwaka serikali inakusanya takribani shilingi bilioni 25.6 ikiwa ni ada kutoka kwa wanafunzi wa kutwa na takribani shilingi bilioni 8.4 kutoka kwa wanafunzi wa bweni. Kwa hivyo, serikali inapata jumla ya shilingi bilioni 34 ikiwa ni mapato yatokanayo na ada ya wanafunzi katika shule za serikali, na hii ndiyo pesa ambayo serikali itaikosa kwa kutekeleza sera yake ya elimu bure.
Kama serikali itafuta michango mingine yote ambayo wazazi wenye watoto katika shule za sekondari wanalipa italazimika kuongeza bajeti yake kwa ajili ya shule za sekondari kwa kiwango cha shilingi takribani bilioni 40. Hii ndiyo kusema kuwa gharama ya kutoa elimu bure, kwa maana ya kumuondelea mzazi mzigo wa ada na michango mingine, ni shilingi zisizozidi bilioni mia moja (bilioni 100) kwa mwaka!
Swali ambalo wenzetu wapinzani wa sera hii wanauliza ni kuwa je serikali itatoa wapi hizi pesa? Katika aya zinazofuata ninakokotoa mahesabu mengine kuonyesha vyanzo vya mapato vya kugharamia sera ya elimu bure.
Katika ilani ya uchaguzi ya CHADEMA msingi mkubwa wa kukuza uwezo wa serikali wa kuhudumia wananchi umejengwa katika kubana matumizi ya serikali na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi. Katika hili wameeleza waziwazi kwamba watapunguza ukubwa wa serikali kutoka mawaziri zaidi ya 40 wa sasa hadi wasiozidi 20, ikiwa ni pamoja na manaibu mawaziri.
Hii ndiyo kusema kuwa CHADEMA watapunguza gharama za kuendesha serikali kwa zaidi ya nusu.
Kuhusu kupanua wigo wa mapato ya kodi, Ilani ya CHADEMA imeweka mkazo katika mambo mawili. Mosi, katika kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija. Pili, mkazo umewekwa katika kuongeza vyanzo vya kodi ambavyo vimeanishwa vizuri katika bajeti mbadala mbalimbali zilizowasilishwa na kambi ya upinzani bungeni kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Nitatumia mfano wa kupunguza misamaha ya kodi kuonyesha jinsi ambayo serikali inaweza kujiongezea mapato ya ziada na kujenga uwezo wake wa kutoa huduma kwa wananchi.
Wataalamu wa kodi wameshauri kwa miaka mingi kuwa misamaha ya kodi isizidi asilimia moja (1%) ya pato la taifa au asilimia 10 ya makusanyo yote ya kodi. Wataalam hawa wanabainisha kuwa punguzo la kodi kwa kiwango hiki hakitaathiri mazingira ya uwekezaji hapa nchini. Hata hivyo, Serikali ya CCM imepuuza ushauri huu wa kitaalam.
Matokeo yake serikali imeendelea kupoteza mapato mengi ya kodi. Kwa mfano, serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008/2009 ilisamehe kodi kwa kiwango cha asilimia 2.7 (2.7%) ya pato la taifa ikiwa ni sawa na shilingi bilioni 731.3.
Kama serikali ingefuata ushauri wa wataalam wa kodi ingesamehe kodi kwa kiwango kisichozidi shilingi bilioni 270. 8 na hivyo kuokoa takriban shilingi bilioni 500!! Ilani ya CHADEMA imetamka waziwazi kuwa Serikali ya CHADEMA itatekeleza ushauri wa wataalam na kuhakikisha kuwa misamaha ya kodi haizidi kiwango cha asilimia moja ya pato la taifa.
Hii ndiyo kusema kuwa kwa hatua ya kupunguza misamaha ya kodi pekee, Serikali ya CHADEMA itaweza kuokoa takribani shillingi bilioni 500, ambazo ni mara tano ya kiwango kinachotakiwa kuwasomesha watoto wa maskini bure.
Tuangalie mfano wa pili. Katika ilani yake, CHADEMA wameahidi kubana matumizi ya serikali kwa kuachana na matumizi ya anasa. Moja ya eneo ambalo CHADEMA wamelenga kuokoa fedha ni eneo la posho. Mifano michache itasaidia kuonyesha kiwango cha pesa kinachoweza kuokolewa kupitia posho.
Kwa mujibu wa vitabu vya bajeti, katika mwaka wa fedha wa 2008/09, Serikali ilitenga shilingi bilioni 506 kwa ajili ya posho, kiwango ambacho ni sawa na mishahara ya walimu 109,000, au zaidi ya theluthi mbili ya walimu wote nchini.
Katika mwaka wa fedha wa 2009/10, kiwango kilichotengwa kwa ajili ya posho kilikuwa sawa na asilimia 59 ya mishahara yote ya wafanyakazi wa serikali. Sehemu kubwa ya posho hizi ni zile zinazolipwa kwa viongozi na maafisa katika taasisi za serikali na haziwahusu watendaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu huko vijijini.
Katika Ilani yake, CHADEMA imeahidi kupunguza kiwango cha posho ili kisizidi asilimia 15 ya mishahara wanaolipwa wafanyakazi wa serikali. Kwa hatua hii, Serikali ya CHADEMA itapunguza kiwango cha posho kutoka shilingi bilioni 506 za sasa hadi shilingi bilioni 126, na itakuwa imeokoa shilingi bilioni 380, ambazo zitaenda katika miradi ya maendeleo, ikiwemo kuboresha mashule na huduma zingine za jamii.
Kwa hatua mbili tu za kupunguza misamaha ya kodi na kupunguza posho zisizo na tija kwa viongozi na maafisa wa serikali, serikali itaokoa shilingi bilioni 880!! Hii ni mifano miwili tu ya namna ambayo serikali makini inaweza kutumia vizuri pesa za walipa kodi kwa ajili ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za jamii, ikiwemo kutoa elimu bure.
Hatujakokotoa fedha zitakazookolewa kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kufuta nafasi za wakuu wa wilaya. Hatujakokotoa fedha zitakazopatikana kwa kutokomeza ufisadi serikalini, na wala hatajukokotoa fedha zitakazopatikana kwa kuimarisha mikataba ya madini. Kwa hiyo utaona kuwa, kwa kutumia mifano michache niliyoitoa hapo juu, tatizo letu sio ukosefu wa fedha katika kutoa elimu bure na huduma zingine za jamii. Tatizo letu kubwa ni utashi wa kisiasa na kukosekana umakini na uvivu wa kufikiri miongoni mwa watu tuliowakabidhi dhamana ya uongozi. Tukiwa na uongozi makini, adilifu na wenye upeo, utakaotumia raslimali zetu vizuri na kukusanya mapato ya kodi sawasawa na kuyatumia ipasavyo, tuna uwezo wa kutoa sio tu elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, bali pia huduma zingine za jamii.
-------------------
Mwandishi wa makala hii ni mhadhiri katika Idara ya Saikolojia ya Elimu na Taaluma za Mitaala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anapatikana kwa simu namba 0754 301908