Habari, nimetunga riwaya ambayo nategemea nitapata maoni yenu kwani iko mbioni kuchapishwa. Na hapa nimeona niwawekeeni kitabu hicho na nitarudi kupata maoni yenu baada ya kukisoma. Nategemea sana maoni na ushauri wenu wana JF wote ambao ni wapenzi na washabiki wa Riwaya. KARIBUNI.
View attachment 54349
Tayari nshasoma kitabu chote.
Pengine ulitaraji nifanye uchambuzi wa
fani na
maudhui yake hadi kufikia hatua ya kutoa '
hukumu' kwa kusema udhaifu wa mwandishi ni moja, mbili, tatu.. Lakini niseme kuwa hilo sitalifanya, na badala yake nakupa maoni ya jumla tu. Umeonesha umahiri katika kujenga taharuki na kumfanya msomaji avutike kuendelea kusoma; hilo ni jambo jema ambalo riwaya nzima imetawaliwa kwalo. Lakini nimepata mashaka kidogo juu ya umakini wa
Bonge kukubali kudanganyika kwa urahisi vile kubadilishiwa begi na asigundue haraka. Kumbuka umesema kwamba begi hili limenunuliwa tu dukani na kupelekwa moja kwa moja bila kushughulika na kuliwianisha uzito, sura ya uchakavu... almradi kujenga mazingira ya kulifananisha na begi halisi. Hilo halionekani na linajenga mashaka kwenye
uumbaji wa wahusika ambao wanapaswa kuonesha umahiri kuuvaa uhusika wao. Liko jambo moja la kukosekana muwala wa matukio fulani fulani. Mathalani riwaya haijabainisha kifo cha Chausiku au Merina kinavyohusiana na mlolongo wa matukio mengine. Labda iwe ni kwa lengo la kuacha mwaya wa kuendeleza riwaya siku za mbeleni, lakini 'mzigo' kutofunguliwa licha ya tangu mwanzo kuonesha kwamba ungefunguliwa hata kama hilo lingemaanisha kifo linaancha maswali mengi kuliko majibu. Msomaji pengine anaweza kutabiri (yaweza kuwa kwa makosa...!) kwamba ndani ya begi kulikuwemo ngozi ya binadamu, viungo vya albino hasa kutokana na mdokezo mahala fulani kwamba pana harusu ya uozo 'ilisikika' kutoka kwenye mzigo. Mhusika Bonge alipata kujitambulisha mahala fulani kuwa ni afisa wa Polisi. Pengine lilikuwa jambo lenye afya zaidi ikiwa ukweli juu ya hili ungabainishwa ili kwamba jamii ipate funzo. Kwamba pana watu matapeli hujisingizia kwamba wao ni watu fulani kumbe sio; au watu fulani tuliowapa dhamana fulani fulani kwenye jamii wanaonesha tabia iliyo ghalati kabisa na viapo vyao. Pengine nikushauri kwamba una nafasi kubwa ya kuireusha zaidi riwaya hii na kuifanya kuwa ndefu kwa kuziba mainya ile iliyomo kwenye msuko wa matukio. Ujue mathalani vifo vyote vilivyotokea hatujaona 'urefu' wa mkono wa dola na msomaji anaweza kuamini kwa makosa kwamba ni rahisi kumuua mtu na bado usitiwe hatiani kwa kuwa tu utatoroka kutoka Dar es Salaam kwenda Musoma.
Natua hapa kwa leo, naamini tutaendela kubadilishana tajriba.