SoC01 Kwaheri Kapteni Zacharia Hans Poppe: Tuna mengi ya kujifunza kuhusu maisha yako

SoC01 Kwaheri Kapteni Zacharia Hans Poppe: Tuna mengi ya kujifunza kuhusu maisha yako

Stories of Change - 2021 Competition

Uchumi wa Mifugo

JF-Expert Member
Joined
May 20, 2021
Posts
345
Reaction score
580
Leo jumatano ya tarehe 15 Septemba 2021 mwili wa Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) Zacharia Hans Poppe utapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele mjini Iringa mahali ambako pia baba yake Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Hans Poppe alizikwa tarehe 26 Mei 1979.

Hans Poppe(baba wa Zacharia) ambaye wakati huo alikuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ziwa magharibi (Kagera) aliuliwa kikatili tarehe 24 August 1971 kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Iddi Amin waliokuwa wamevuka mpaka na kuingia eneo la Mutukula,baada ya kumuua waliondoka na mwili wake na kukaa nao hadi mwaka 1979 baada ya Iddi Amin kutolewa madarakani mwili wa Hans Poppe ndipo ulikabidhiwa Tanzania.

Zacharia alizaliwa mwaka 1956 baada ya masomo alijiunga na JWTZ ambako alipata uafisa akiwa na miaka 19 na kupanda vyeo hadi kufikia cheo cha Kapteni.Mwaka 1983 ni mwaka uliobadilisha maisha ya Zacharia,yeye na wanajeshi wenzake pamoja na raia wachache walipanga kuipindua Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere mpango huo ulikwama baada ya siri kuvuja na kunaswa na maafisa Usalama ambao walianza kufuatilia na hatimaye baadhi walikamatwa,wengine kukimbia na mmoja ambaye ni Komandoo Mohamed Tamimu kuuawa wakati wa mapambano ya kumtia nguvuni.

Baadhi ya majina maarufu ya walikamatwa ni Luteni Kanali Martin Ngalomba, Luteni Kanali Martin Peter Msami,Kapteni Suleiman Metusela Kamando, Kapteni Zacharia Hans Poppe,Meja Reverian Bubelwa,Kapteni Vitalis Gabriel Mapunda,Kapteni Rodric Roshan Robert, Kapteni Harry Hans Poppe (ndugu na Zacharia),Luteni Badru Rwechungura Kajaja na Luteni Dietrich Oswald Mbogoro.Majina maarufu ya raia waolikamatwa ni Pius Mutakubwa Lugangira au anko Tom au faza Tom na Hatib Gandhi au Hatty McGhee.

Awali waliokamatwa walikuwa 30 lakini baadhi walitoroka wakiwemo anko Tom na McGhee na wengine kuachiliwa huru mpaka mwisho waliofikishwa mahakamani walikuwa 19 na wote walihukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha tarehe 27 Disemba 1985.

Kutoka kuwa Afisa wa jeshi mpaka mfungwa wa kesi ya uhaini ulikuwa mtihani mkubwa kwa Zacharia lakini kila jambo linatokea kwa sababu fulani na hizo sababu zinasababisha mabadiliko, mabadiliko ambayo yanaweza kuumiza na ni magumu kuyakabili lakini mwishowe huwa ni kwa ajili ya neema.Na ndivyo ilivyokuwa kuuacha Uafisa wa jeshi na kwenda jela lilikuwa pigo kuu kwa Zacharia lakini lililoleta neema kwa watu wengi.

Mwaka 1995 Rais wa wakati huo Ali Hassan Mwinyi miezi michache kabla hajastafu aliwaachia huru wafungwa hao wa uhaini na hakujua kama mmoja wa wafungwa hao angekuja kuwa mfanyabiashara mkubwa ambaye angeajiri watu wengi,angelipa kodi na angesaidia watu wengi.

Kwa mujibu wa Crescentius Magori ambaye ni rafiki wa karibu wa Zacharia na mwanachama mwandamizi wa Klabu ya soka ya Simba anasema alipotoka jela Zacharia alipewa lori moja na ndugu yake lililokuwa kama mtaji wa biashara yake. Dereva wa lori hilo alikuwa Zacharia ambaye aliajiri utingo na kuanza kupiga kazi kwenda DR Congo,Malawi, Zambia,Rwanda,Burundi na Uganda baada ya malori kuongezeka ndipo alipoamua kuacha udereva na kubakia kuwa msimamizi.

Maisha ya Zacharia yanatupa mafundisho mengi.

Hakukata tamaa

Alifungwa jela lakini alitoka akiwa na afya njema na akili nzuri,wenzake wengi walikata tamaa waliona wamepoteza kazi na vyeo vyao na muda mwingi wamepoteza gerezani mbaya zaidi jamii iliwatenga,iliwanyanyapaa mpaka leo Kapteni Robert kule Songea anakoishi wanamuita mhaini,jina la mhaini ndilo jina maarufu la Kapteni Robert pale Songea.

Watu wengi wanapitia matatizo na changamoto mbalimbali wengine wanafukuzwa kazi, wengine wanafungwa jela, wengine wanaachana na wapenzi wao, wengine wanapata hasara kwenye biashara zao, wengine wanatengwa na jamii zao, wengine wanafirisika.Badala ya kupambana kutatua matatizo hayo hukimbilia kuua,kujiua,kuwa walevi na kutumia madawa ya kulevya kwa kisingizio cha kupoteza mawazo lakini Zacharia hakuwa hivyo hakuufikiria Ukapteni wake wakati alipokuwa anapangua gia kwenye mteremko wa Kitonga, hakuufikiria Ukapteni wake wakati akiwa anapata vikwazo vya kuvuka boda ya Kasumbalesa na hakukata tamaa alipokuwa anaegesha lori lake na kulala boda pale Tunduma kwa siku tatu hadi nne akisubiri wenye mamlaka wamruhusu kuvuka.

Zacharia anatukumbusha hata unapokuwa umepoteza mali yako,cheo chako,mpenzi wako na kazi yako hakuna kukata tamaa.Kuna maisha mengine ambayo ukiyapambania yatakupa heshima kuliko yale ya awali.

Usimamizi wa biashara

Akiwa na lori moja aliamua awe dereva mwenyewe.Usimamizi wa biashara hasa ikiwa mpya ni jambo la muhimu sana.Ukiisimamia kwa ukaribu ndipo utajua changamoto,faida,vikwazo na vitu vingine vya muhimu.Leo hii kijana ana bodaboda moja hana kazi lakini anatafuta deiwaka kwa sababu tu amemaliza Chuo kikuu,mwingine anaanzisha ufugaji wa kuku lakini hata kuingia bandani kufanya usafi au kuwaweka maji kuku hataki.

Malengo

Mtu mwenye akili nyepesi anaweza kusema alifanikiwa kwa sababu alipewa lori na ndugu yake lakini wangapi wanapewa mitaji na wanafirisika kwa kunywea pombe, kuhonga au wangapi wanapewa usimamizi wa biashara za ndugu zao au za familia na wanashindwa kuzisimamia?

Zacharia alikuwa na malengo
alitoka jela alikabidhiwa lori moja na mpaka anakufa alikuwa anamiliki vituo vya mafuta na malori mengi .Bila malengo angekuwa kama madereva wengine ambao wana wanawake na watoto kila mji.

Alisimamia kile alichokiamini ni kwa maslahi ya umma

Zacharia alisimamia kile alichokiamini,mara nyingi aliingia kwenye mizozo na wanasiasa au viongozi wa soka kwa kusimamia kile alichokiamini ni sahihi kwa manufaa ya wengi.Tarehe 4 Oktoba 2013 alipokuwa mhazini wa chama cha wenye malori Tanzania alimuita aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa wakati huo John Pombe Magufuli kuwa ni mtu asiyejua na ambaye ana chuki kubwa kwa wasafirishaji na alisema anafikiria kuwa Magufuli anafanya makusudi ili apate mgao wake wa rushwa.Mzozo huo uliibuka baada ya Magufuli kuwaagiza wafanyakazi wa mizani wa Iringa wawatoze faini wenye malori na kuwauliza kwanini faini zinapungua.

Aliisaidia jamii

Pili Misana ni mwanzilishi wa Taasisi ya Pili Misana sober house ambayo inawaweka pamoja waathirika wa madawa ya kulevya na kuwasaidia kuacha matumizi ya madawa hayo hatari anasema mwaka 2012 Zacharia alitoa shilingi milioni 20 wakati anaanzisha Taasisi hiyo na mwaka mmoja baadaye akatoa milioni 15 kusaidia Taasisi hiyo mpaka sasa Pili Misana sober house Ina matawi matatu na imesaidia waathirika 2000.

Kusaidia michezo na wanamichezo

Mchango wa Zacharia kwenye michezo hasa ushiriki na kuisaidia Klabu ya maisha yake Simba kila mtu anaujua.Michezo inaburudisha watu wengi walipata burudani kupitia mchango wa Zacharia.Michezo inaajiri watu wengi, wanamichezo wengi mahiri kama Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Ibrahim Ajibu,Said Ndemla mpaka akina Emmanuel Okwi na wengine wengi wanautambua mchango wa Zacharia kwenye maisha yao.Fedha za Zacharia zililisha familia zao ,ziliwajengea nyumba,ziliwasomesha watoto wao na zililipa gharama ya matibabu ya familia zao.

Umuhimu wa kusamehe

Mzee Mwinyi kama asingemsamehe Zacharia mwaka 1995 leo hii tungekuwa tunazungumza mengine.Msamaha wa mzee Mwinyi una maana kubwa kwa maisha ya Zacharia, kwa maisha ya Wafanyakazi wa Zacharia na kwa wale wote waliosaidiwa na Zacharia.Tuendelee kusameheana hakuna jambo ambalo halina msamaha.Kama Mungu anatusamehee,sisi kwanini hatusameheani?

Kusaidiana

Kama ndugu yake Zacharia angeamua kumcheka,kumnyanyasa na kumzodoa alipopata matatizo kama wengi wetu tulivyo ambapo mtu wa karibu yako akipata matatizo unakimbilia kuyatangaza,unamnyanyasa na kumzodoa leo hi Zacharia angekuwa si lolote na si chochote lakini msaada wa lori moja siyo tu ulibadilisha maisha ya mfungwa wa uhaini bali ulibadilisha maisha ya watu wengi waliofanya kazi na tajiri Zacharia na wale wengi waliosaidiwa na Zacharia. Kwahiyo inatupa fundisho kubwa la ndugu,jamaa na marafiki kusaidiana mmoja wetu anapopata matatizo kwa sababu hakuna aijuaye kesho yake.

Pumzika kwa amani Kapteni Zacharia Hans Poppe Wanamichezo, Wafanyakazi wako na Watanzania tutakukumbuka daima.

Screenshot_20210914-121057_1.jpg

Picha kutoka mtandaoni ya Kapteni Zacharia Hans Poppe.


Karibuni kwa mjadala na kupiga kura.
 
Upvote 9
Mamia ya waombolezaji wameshiriki mazishi ya Kapteni Zacharia Hans Poppe mchana wa Leo mjini Iringa.

RIP Legend.
 
Picha ya Zacharia Hans Poppe mwenye sare ya (JWTZ)akiwa nchini Uganda alipokwenda kukabidhiwa mwili wa baba yake.

Screenshot_20210915-195919_1.jpg
 
Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Hans Poppe(baba wa Zacharia)akiwa anakagua gwaride.
Screenshot_20210915-195958_1.jpg
 
Screenshot_20210915-161549_1.jpg
mazishi ya Zacharia yaliyofanyika siku ya jumatano tarehe 25 September 2021.
 
Chakujifunza ni kuanza kidogo au kutumia kidogo ulichokuwa nacho vizuri ili uweze kukuza haya mengine ya uwezo ukizingatia utapotea kwasababu kiuwezo tunatofautiana
Umejibu vizuri, watu wengi hasa vijana wanapata mitaji kwa kukopa,kupewa na ndugu lakini wanaifilisika kwa kuendekeza kuhonga,ulevi nk.Kinachotakiwa kile kidogo kitumike vizuri.
 
"Hans alikuwa mtu maarufu ,muongeaji na mkarimu Sana.Kila pump attendant alipenda kumhudumia.Alikuwa haondoki bila kukupa tip.1997 mwishoni alikuwa anakuja na malori yake yameadikwa Hans Poppe.Pamoja na madhila yote Hans Poppe alisimamia na kutoka , nitamkumbuka daima"-ujumbe wa Edmund C Matotay kutoka Twitter aliyewahi kufanya kazi kituo cha mafuta cha GAPCO kilichopo karibu na uwanja wa taifa.
 
Eddy Hans Poppe (kushoto)ndugu yake Zacharia naye amefariki tarehe 19 septemba 2021.Tuvae barakoa,tunawe mikono na tuchanje, Covid 19 ipo.


Screenshot_20210920-064714_1.jpg
 
Back
Top Bottom