Ni muda tu ulifika wa Chama na Konde Boy kuondoka kwani viwango vyao vilikuwa juu sana na walipata ofa kubwa sana kuzidi uwezo wa Simba kifedha. Na sikuona namna ambavyo Simba wangeweza kuzia wasiondoke. Na Konde Boy na Chama ni wachezaji wa kimataifa na mawakala wao nao ni wa kimataifa kwa vyovyote vile mikataba yao japo sijaiona lakini naamini lazima ilikuwa na kipengele cha kuondoka mara tu wapatapo ofa kubwa. Tuwe wakweli tu mtu mzima yoyote yule anapoamua kuondoka mahali iwe ni kwenye ndoa, kazini, mchezaji, mlinzi, hata "house girl" huwezi kumzuia na ikitokea umemzuia kwa nguvu abaki kila mtu anajua madhara yake. Japo Simba walikuwa na uwezo wa kuwalazimisha wamalizie mikataba yao lakini mwishoni wangeondoka bure kabisa. Pia wangeweza kucheza chini ya kiwango na kuigharimu timu na mbaya zaidi wachezaji wenye vipaji vikubwa na malengo ya baadaye wasigekubali kusajiliwa Simba wakijuwa kuwa watabaniwa wakipata ofa kubwa.
Watu wanoujua mpira kwa undani wanajua kabisa kuna Konde Boy mmoja tu na kuna Chama mmoja tu kwahiyo nashangaa sana watu wanapoanza kuwalinganisha na wakina Banda. Hiyo katu haiwezekani kwani mburudishaji kama Chama anatokea baada ya miaka kadhaa. Ile "work rate" ya Konde Boy sijui unaipatia wapi kwa siku za karibuni. Ni raha sana kuwatazama hao wachezaji wawili jinsi wanavyouamrisha mpira ufanye watakavyo lakini sasa watakosekana hiyo lazima kila mpenda mpira alikubali. Kwangu mimi binafsi kidogo naweza kumlinganisha Chama kiuchezaji na watu wawili mafundi Hamisi Gaga "Gagarino" na Said Mwamba "Kizota" japo uchezaji wao bado haulingani kwa asilimia 100%.
Kwa hiyo hao wakina Banda waachwe waje waonyeshe vipaji vyao ikiwezekana na wao waweke alama zao kivyao kwani Mungu amemjalia kila mmoja kipaji cha aina yake. Lakini kitendo cha kuwalinganisha ni "big no". Inaweza kutokea japo si rahisi kati ya hawa wachezaji wapya wakawa sawa na Chama au Konde Boy au hata kuwa zaidi yao lakini hiyo ni bahati nasibu na nadra sana kuwa hivyo kwa siku za karibuni. Na duniani kote ipo hivyo kwa mfano mchezaji gani leo tunaweza sema ni sawa na Ronaldino Gaucho, au Messi au Ronaldo. Lakini wakina Mbappe, si wanakuja na staili zao na tunaanza kunawakubali kivyao vyao.