Umejengwa utamaduni wa ajabu kwa kutoa Sifa kwa viongozi wa kisiasa wanaposimamia utekelezwaji wa miradi ya kitaifa, na kusahaulika Mwananchi ambaye ndiye aliyemwaga jasho kutafuta pesa na kuipa kodi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Sifa hizo kwa sasa zimeenda mbali zaidi kusifia hata pale ambapo wanasiasa hao hawajahusika hata katika usimamizi jambo lolote ila sifa hupelekwa kwao kuwa wamefanya jambo hilo kutokea.
Huo ni utamaduni usiofaa kwani ni mbinu ya kuwalazimisha watu kuona mazuri hata yasioyokuwepo na kuwafanya watu wasione udhaifu wa viongozi hao kisiasa.
Mbaya zaidi kumezuka hata tabia ya kuweka sherehe za kuwapongeza viongozi eti kwa kutekeleza miradi, katika sherehe hizo hutumia tena pesa za walipa kodi japo sherehe nyingi hufichwa kwenye jina la uzinduzi ambapo unakuta gharama ya uzinduzi inaweza kukaribia gharama ya mdari husika!
Una point konki, lakini umeuzunguka mno mbuyu.
Nikuambie tu kwamba unachokijua ama usichokijua, hii tabia ya uchawa pamoja na kujifyetua akili hata kwa watu waheshimiwa kabisa katika jamii ni ajira inayowalipa sana wao kwa kushibisha matumbo yao.
Ni ubinafsi na uzandiki kwa uzalendo wa Taifa kwa mheshimiwa kama Waziri, Rc, Dc ama Mbunge kusimama hadharani na kusema kwa mfano: ... 'Mama katoa pesa kujenga kipande cha barabara kutoka point 'A' kwenda point 'B' na maneno mengine yenye kufanana na hayo wakati wakijua kabisa kuwa ni ya uongo mtupu.
Rais ni muajiriwa wa wananchi, ni kiongozi wa utekelezaji wa maamuzi ya Taifa, analipwa kwa kazi hiyo kama mwajiriwa yeyote mwingine wa Serikali na hana pesa hata senti 5 kuweza kuitoa mfukoni mwake kutekelezea mradi wowote hata wa kujenga choo cha shimo cha shule.
Walishaona kwamba kumsifia Rais kwa maneno ya uzandiki na unafiki wa uongo ni kumuenzi na kumfurahisha yeye ili kumfubaza mawazo yake, asiweze kuziona dosari zake katika uongozi wake na asiweze kuona watu wengine wenye sifa bobezi zenye kufaa kuweza kulitumikia taifa, kwamba wao ndiyo watu bora na wapo karibu na mama.
Na kama wako mbali, basi kwa kupaza sauti zao za kusifia, wataonekana na kusogezwa.
Kwa hiyo kama kuukemea huu uozo, tuukemee bila ya kumumunya maneno.
Kwani kumsifia Rais kwa sifa za kweli zenye kuonekana katika utekelezaji wa majukumu yake kuna ubaya gani?
Basi mwenye kusifia, akae chini achambue sifa stahiki anazopaswa kumpa kiongozi husika na siyo kumtengenezea sifa za uongo wa mchana kweupe zisizomstahili kupewa.
Na huo utaratibu mbovu kwa matumizi ya fedha za Serikali, ndiyo athari za matokeo ya mambo tunayoyaongelea sasa.
Hiyo syndicate ya wazandiki na mafisadi, hakuna anayeweza kuwakemea katika ubadhirifu wao huo kwa sababu mwenye uwezo wa kufungua kinywa na kukaripia ili kukomesha ndiye kapigwa nusu kaputi la usingizi wa sifa, kwa hiyo hawezi kuona madhila yoyote ambayo taifa linapitia kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma.