Jana Mlimani TV walinikosha sana kwa kumuonyesha Mwalimu akizungumza na Waandishi wa Habari pale Kilimanjaro Hotel mwaka 1995. Ukiisikiliza hiyo hotuba yake ama kuisoma kwenye kijitabu kinachoitwa NYUFA kwa kweli utaamini kwamba Mzee yule alikuwa anaona mbali na alikuwa mtabiri wa kweli wa hatma ya Tanzania si kama yule mzee wa majini pale Magomeni Mikumi! Mwalimu alisema Tanzania imeanza kuwa na nyufa kwa kukiuka misingi mizuri iliyokuwa imewekwa huko nyuma. Alizungumzia hatari za rushwa, ukabila na udini. Akasema nchi inanuka rushwa, Watanzania ni vulnerable ukabila haujaisha upo chini tu ya ngozi zao kwa hiyo usipoendelea kudhibitiwa ukabila utarudi. Akawaomba Watanzania wasiendekeze udini maana vyote hivyo ni hatari kubwa kwa mustakabali wa nchi.
Mwalimu alizungumzia kwa kina kuhusu rushwa na jinsi inavyohitaji utashi na uongozi thabiti kushughulikia tatizo hilo. Akaeleza jinsi rushwa ilivyokuwa ikishughulikiwa kwa nguvu zote katika utawala wake. Wale waliokamatwa wakitoa ama kula rushwa walipelekwa mahakamani na walipohukumiwa Serikali ilikuwa imeishaweka adhabu ya kufungwa jela miaka 2 na kupigwa viboko 24! Mwalimu alitania kwamba hivyo viboko 12 mla rushwa/mtoa rushwa anapigwa anapoingia jela na 12 anapotoka jela akamuonyeshe mkewe! Akahadithia kwamba katika awamu yake aliwahi kukamatwa hata Mgiriki mmoja raia wa Cyprus corrupt mtoa rushwa ambaye alikuwa akitamba kwamba alikuwa ameiweka Serikali mfukoni. Alikamatwa, akapelekwa mahakamani, Akafungwa jela kama Watanzania wengine. Watu chungu nzima akiwemo Rais Kenyatta wa Kenya walijaribu kumuomba Mwalimu amuachie mgiriki yule, lakini Mwalimu akakataa kata-kata akisema mtu huyo ni mshenzi, alikuwa na mfuko mkubwa kiasi gani kuweza kuiweka Serikali yote mfukoni mwake?!! Hatimaye aliachiwa baada ya Askofu Mkuu Makarios wa Cyprus kutuma ujumbe kumuomba Mwalimu amsemehe mgiriki huyo. Mwalimu akakubali kwa masharti kwamba asionekane tena sio nchini tu bali Afrika Mashariki yote! Hivyo ndivyo rushwa ilivyokuwa ikishughulikiwa katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu.
Sasa inavyoelekea Dr. Slaa ambaye ameonyesha dhahiri kuchukizwa na ufisadi ana mwelekeo wa kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere katika kurekebisha makosa kadha wa kadha yaliyofanywa na utawala wa CCM yanayohatarisha sana mstakabali wa Taifa letu. Kwa sababu hiyo lazima CCM waogope kwa kuwa endapo Dr. Slaa atafanikiwa itakuwa ni mwanzo wa mwisho wa mafisadi nchini mwetu!