Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,184



Kuwalaumu wanafunzi au waalimu pekee ni kutafuta majibu mepesi kwenye maswali mazito. Lengo la elimu ni kukulainishia maisha lakini kama ukiwa nayo na yule asiyenayo nyote mnarundikwa kundi moja basi motisha wa kuwa na elimu hupotea.
Wanafunzi wengi wanaona jinsi jamii na hususani serikali yao inavyodharau wasomi wake na hivyo kujenga mitazamo ya kuwa maisha yao hayana uhusiano wowote ule na elimu hiyo. Hivyo kutokazana kujifunza na matokeo yake ni kutofanya vizuri mashuleni.
Motisha ulioporwa na serikali ni katika maeneo yafuatayo:-
1) SERIKALI INAABUDU WANASIASA!
Kama mshahara wa Raisi siku hizi ni siri yake na wakati wa Nyerere mshahara wa Raisi ulikuwa Tshs 5, 000/= tu kwa mwezi. Unapoona usiri katika shughuli za umma ujue ni ujambazi wa uporaji tu ndiyo unaoendelea hapo. Serikali inaona aibu jinsi ambavyo imeuinua mshahara wa Raisi na hata kutuficha sisi waajiri wa huyo Raisi!
Bunge kazi kubwa ni kuongezeana mishahara na posho bila kuwepo chombo ambacho kinachoratibu mishahara na mafao ya watumishi wote wa umma ili kujenga misingi ya haki na kuheshimiana. Bungeni hupigia ukelele khali duni za watumishi wa umma lakini hutasikia khoja binafsi ya kuboresha masilahi ya watumishi wa ngazi za chini wa serikali ambako wengi ndipo wamo.
Aidha kinyume na matakwa ya kikatiba, Serikali imewabagua watumishi wote wa Umma na kuja na sheria ya mafao ya viongozi wa kitaifa ya mwaka 1999 na kuiboresha mwaka 2005. Huu ni ubaguzi wa kutisha na katiba inakataza tusibaguane kabisa. Serikali ikielewa ya kuwa ukokotoaji wa mafao ya kustaafu hakuzingatii khali halisi ya mfumuko wa bei na mapato wao kazi yao ni moja ni ya kuwalinda walaji wakuu serikalini wakaja na formular za 80% ya mshahara wa sasa ambao tayari umerekebishwa kumudu mfumuko wa bei huku walalahoi wanaachwa kwenye formulars ambazo hazina uhusiano wowote ule na mshahara wa sasa!
Mwanafunzi aliyepo shuleni hivi leo anaona hii dhuluma na kuvunjika moyo kukazana shuleni kwani haoni elimu hiyo itamsaidiaje kwenye maisha yake ya kiutu uzima.
2) Soko la ajira ni finyu.
Mimi huwa nacheka mpaka mbavu zinaniuma pale ambapo naona na kusikia "waajiriwa" viongozi wa serikalini wanapowahimiza vijana wajiajiri wakati wao "waajiriwa" ukifikia muda wa kustaafu huchukua mikataba kujiongezea utumishi haramu serikalini. Pia viongozi hao huhubiri "kujiajiri" wakati wao kamwe hawajawahi kujiajiri na kuelewa ugumu katika hiyo sekta ya ujasiriamali.
Mwanafunzi aliyepo darasani leo anajiuliza hivi kweli hii elimu itanipeleka wapi, maana hana mtaji hususani uzoefu wa kujiajiri na serikalini wazee wanashikilia ajira hadi kufa..............
3) Wasomi wageni ndiyo kipenzi cha serikali.
Kampuni za kigeni ndizo hupewa mnofu na hii serikali yetu kwa visingizio lukuki vikiwemo wanauzoefu na kampuni za kizawa kuambulia mifupa. Sasa unategemea kweli kwenye mazingira ya namna hii divisheni ziro zisiongezeke? Lazima kuwepo uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiwango cha elimu na upatikanaji wa mkate vinginevyo elimu hiyo haina maana...........
4) Ajira za kujuana.
Hivi utamwelezaje mwanafunzi wa leo anapoona ajira kila mahali ni kujuana na wala siyo sifa? Sasa akazane ili iwe nini kama anachotakiwa kufanya siyo kusoma bali kumfahamu mwajiri wake tu kupitia soko la kufahamiana na kufahamishiana? Wengine wanaliita soko tajwa kuwa ni soko la kuwezeshana........
5) Wasomi kutopewa mitaji ya kuanza kujiajiri.
Wahubiri wa "mkajiajiri" kwa vile wao hawajawahi "kujiajiri" wanakosa ufahamu wa changamoto za ujasiriamali na mojawapo ya changamoto hizo ni ukosefu wa mitaji. Jitihada za kuwakopesha huishia shs elfu hamsini ambayo ukimwuliza yule anayezitoa anatarajia mkopeshwaji atazifanyia nini hawezi kukujibu zaidi ya kujitetea uwezo wake ndipo ulipoishia. Kama hela hazitoshi kwanini hata unatoa mikopo feki hivyo kama siyo kupotezea watu muda na matumizi mabaya ya rasilimali?
6) Ukosefu wa sera ya soko la ajira binafsi!
Kama kweli tupo makini katika kuliinua soko la ajira binafsi sera zake ziko wapi? Na ni nani aliyezibuni? Tusitegemee "waajiriwa" serikalini watuandalie sera za tasnia ambayo wao wenyewe hawana uzoefu nayo.
7) Migogoro ya ajira haitatuliwi kwa haraka!
Maeneo mengi ya kazi, nguvukazi inazuiwa kufanyakazi kwa sababu ya migogoro ambayo ni mingi na hatujaweza kuweka mfumo wa kuitatua kwa haraka ili kuruhusu nguvukazi iweze kuchangia kwenye pato la taifa. Taratibu za kisheria zilizopo zinakwamisha juhudi za kuwatumia wataalamu wetu vilivyo.
Mwanafunzi anapoyaona haya unafikiri hamu ya kusoma atakuwa nayo kweli?
8) Mitaala kutumika kuua vipaji vya wanafunzi!
Elimu lazima itoe mwanya wa kukuza vipaji vya wanafunzi badala ya sera zilizopo za kuwalazimisha wanafunzi wote kusoma aina moja ya masomo. Yule mwenye ujuzi wa michezo aendelezwe kulingana na vipaji vyake siyo alazimishwe kuacha michezo na kuzama kwenye hisabati, fizikia na kemia ambayo hana kipaji nacho. Yule ambaye amejaaliwa kwenye fani ya muziki, uigizaji, mapishi na elimu nyinginezo ambazo hazifundishwi mashuleni sasa ziingizwe kwenye mitaala na kuendeleza vipaji hivyo.
9) Mitaala iwe na uhusiano na maisha ya kila siku.
Sehemu kubwa ya mambo yanayofundishwa mashuleni hayana uhusiano na changamoto tunazokutana nazo na hivyo kuwa elimu hiyo haimsaidii mhitimu kuweza kumudu maisha na hivyo kumchanganya kabisa. Kwanini mwanafunzi ahangaike na elimu ambayo haimtatulii kero zake za kila siku?
10) Kusisitiza elimu ya juu badala ya elimu ya msingi na ya kati!
Vyuo vingi vya kati vimegeuzwa kuwa vyuo vikuu kama vile kazi nyingi hufanywa na wenye elimu ya chuo kikuu jambo ambalo silo kweli. Sehemu kubwa ya ajira ipo kwenye elimu ya kati badala ya kuongeza vyuo vikuu na bajeti yake msisitizo uwe kwenye elimu ya mikono (Vocational skills) kupitia vyuo vya VETA ambako wahitimu wakitoka wana ujuzi wa kuingia soko la ajira bila ya kuhitaji mafunzo ya ziada.
Kwa kurekebisha haya, utakuta wanafunzi wakijituma kwa sababu motisha wa kufanya vizuri unakuwa uko wazi na kwa kila mtu kuona, wapi anatoka, yuko wapi na anaelekea wapi......................na hakuna kubaguliwa ndiyo misingi ya utu na isipokuwepo wachache sana watakuwa na dhima ya kufanya vizuri na hivyo kukazana...........