Zitto
Former MP Kigoma Urban
- Mar 2, 2007
- 1,562
- 10,888
Nimeandika makala haya kwenye gazeti la Kiongozi toleo la jana Ijumaa. Ninaamini litaongeza chachu ya mjadala huu kuhusu elimu.
Makala iliyopita nilimaliza kwa kusema kwamba leo tutaona namna ya kufanya ili kuokoa maisha ya watoto waliofeli. Itakumbukwa kwamba tulizungumzia kuhusu dhana ya nchi kufaidika na uwepo wa vijana wengi (demograpic dividend) ama kupata hasara iwapo Taifa halikuandaa nguvu kazi hiyo kuzalisha mali na kuendeleza nchi (demographic bomb). Nimeona leo niandike tufanye nini kuhusu Elimu yetu.
Napenda kuwajulisha wasomaji wangu kwamba Jimbo langu la Uchaguzi ni moja ya majimbo ambayo yamefanya vibaya sana katika matokeo ya kidato cha nne. Nimekuwa nina msongo mkubwa sana wa mawazo baada ya matokeo hayo. Katika watoto 1329 wa Jimbo la Kigoma Kaskazini waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, hakuna aliyepata daraja la kwanza, 5 walipata daraja la pili, 14 walipata daraja la tatu na waliosalia walipata daraja la nne na sifuri. Asilimia 98.6 ya watoto wote walipata alama hizo za mwisho. Hayo ndio matokeo kutoka katika shule 14 za kata katika Jimbo ambalo mbunge kama mimi ninayezungumzwa nchi nzima natokea. Aibu kubwa sana.
Lawama za matokeo haya ni kwa Watanzania wote lakini uwajibikaji ni wa wasimamizi wa Elimu maana wazazi, asasi za kiraia na hata wabunge wamekuwa kila wakati wakisema kuwa ni lazima tuboreshe elimu yetu. Serikali imekuwa ikificha kichwa chini ya mchanga ikiamini kuwa kiwiliwili hakionekani, madhara yake ndio haya tunaona hivi sasa kuhusu suala la Elimu na matokeo ya kidato cha nne.
Waziri wa Elimu ndugu Shukuru Kawambwa (nashangaa sana kwanini bado ni Waziri mpaka hivi sasa) alisema kwamba tatizo kubwa ni kwamba hakuna walimu wa kutosha. Kinyume chake kabisa hivi sasa kuna walimu wengi sana nchini kiasi cha kuvuka malengo ya mkukuta ya mwalimu 1 kwa kila wanafunzi 40 (1:40). Takwimu zinaonyesha kuwa hivi sasa nchini kuna walimu wa kumwaga kiasi cha baadhi ya mikoa kuwa na uwiano wa mwalimu 1 kwa kila wanafunzi 21. Wastani wa sasa kitaifa ni 1:35. Tatizo ni nini sasa? Moja walimu wamegawanywa kwa mikoa kadhaa na maeneo ya mijini ihali maeneo ya vijijni hayana walimu. Ndio maana shule za vijijini zimefelisha zaidi kuliko shule za mijini. Pili walimu hawa hawana motisha ya kufundisha na hivyo kiukweli hawatoi elimu kabisa kwa watoto.
Waziri anasema sababu za watoto kufeli sana ni kutokuwa na maabara za kutosha. Hili ni kweli kwa masomo ya sayansi lakini sio kwa kweli kwa masomo kama kiswahili, hesabu, kiingereza, historia nk. Watoto asilimia 60 wameshindwa masomo haya pia ambayo hayana mahusiano yeyote na uwepo wa maabara. Kwa hiyo kuna tatizo la ziada kuhusu elimu na ufundishaji. Sasa kama sababu zote za kufeli hazina maana nini kifanyike?
Kuna sababu ambayo imesemwa sana wachambuzi wa mambo, kwamba Bajeti ya Elimu ni ndogo na hivyo ndio maana matokeo yanakuwa mabaya sana. Inawezekana ikawa hivyo kama tunaangalia kwa undani sana bajeti ya elimu. Lakini hebu tuone Bajeti ya Elimu kwa miaka kadhaa ya nyuma na kulinganisha na matokeo ya kidato cha elimu. Mwaka 2008/09 Bajeti ya Elimu ilikuwa asilimia 20 ya Bajeti yote ya nchi na hivi sasa ni asilimia 17. Bajeti ya Elimu ya Sekondari imeongezeka kutoka shilingi 137 bilioni mpaka 509 bilioni kati ya mwaka 2008/09 mpaka 2012/13. Hata hivyo matokeo yameporomoka kwa asilimia 34. Yaani kuna mahusiano hasi kati ya kuongezeka bajeti ya Elimu na matokeo ya watoto wetu. Sasa kama bajeti inaongezeka, walimu wapo na masomo ya historia nk hayahitaji maabara nini kimefelisha watoto wetu? Mazingira ya kufundishia na kujifunza na usimamizi wa Elimu ndio chanzo cha watoto kufeli mitihani. Nitaeleza kidogo na kisha kutoa majawabu.
Walimu wengi wanaopangwa shule za vijijini hawaendi kwa sababu ya ugumu wa maisha huko. Hii ni pamoja na kuwa mwalimu wa mjini na wa kijijini wote wanalipwa mshahara sawa licha ya mazingira magumu ya mwalimu wa kijijini. Hivyo Mwalimu anakuwa hana motisha kabisa ya kufundisha na wakati mwingine wala hahudhurii darasani. Mazingira ya walimu kufundishia ni mabaya na bajeti kubwa ya elimu haielekezwi katika eneo hili. Ukitazama Bajeti ya Tanzania utaona kuwa sehemu kubw ya Bajeti inaelekezwa kwenye matumizi ya kawaida kuliko matumizi ya maendeleo. Mwaka 2011/12 kwa mfano, asilimia 10.2% ya bajeti ndio ilikuwa ya maendeleo. Katika mazingira kama haya ni vigumu sana kuweka mazingira mazuri ya walimu kufundisha. Hali hii pia haitoi motisha kwa wanafunzi kusoma maana wanahitaji mazingira bora ikiwemo uwepo wa vitabu na vifaa vinginw vya kusomea.
Mjadala wa mishahara ya walimu ni mjadala usioisha. Kiukweli kama tunataka kuboresha elimu ni lazima tutoe upendeleo wa kipekee wa kada ya walimu katika mishahara. Hivi sasa Mwalimu mwenye cheti anayeanza kufundisha analipwa tshs 240,000 kwa mwezi, wa diploma analipwa tshs 375,000 na mwenye shahada tshs 469,000. Kwanza ni vema tuanze mpango maalumu wa kuhakikisha kuwa walimu wote nchini waanzie diploma na kuendelea. Pili mishahara ya walimu ipandishwe kwa asilimia 50 na tuwape motisha nyingine kama posho za nyumba na posho maalumu kwa kuwa Walimu ili kudhibiti ugumu maisha. Vile vile tuwe na mfumo tofauti wa kodi ya mapato kwa walimu ambapo tuseme kuwa kodi PAYE kwa walimu iwe ni asilimia 5 ya mshahara. Walimu wenye elimu kubwa zaidi na wenye ujuzi maalumu wafutiwe kodi kabisa ili kutoa motisha kwa watu wenye ufaulu mzuri kuingia kufundisha badala ya sasa ambapo ualimu unaonekana kama fani ya waliofeli.
Ni maoni yangu kwamba hivi sasa taifa lijielekeze kwenye kuimarisha hadhi ya mwalimu kwa kumlipa vizuri, kumwekea mazingira mazuri ya kufundisha na kumpa vifaa vya kutosha na hasa vitabu. Mipango yote ya elimu imweke mwalimu na mwanafunzi katikati.