Ni vyema kwanza tukafahamu ya kwamba PENZI ni kitu cha thamani sana na chenye kuleta mafanikio katika nyanja zote za kimaisha alizonazo mwanadamu; zingatia ya kwamba dini zote zinasisitiza pamoja na mambo mengine UPENDO kwa sauti kubwa zaidi.
Katika maisha ya sasa tuliyonayo yaliyojaa majeruhi wa mapenzi pametokea kuwa dhana halisi ya mapenzi imepotoshwa na jamii kwa sababu ya kutafutwa kwa haja binafsi na ubinafsi uliokithiri. Pengine ndani ya hili wana JF mtanisaidia kutafiti kwanini tamaa za kimaumbile na pesa ndio mkondo na chati ya penzi la sasa.
Vijana wengi hususani wasichana wamejikuta tuu wameingia katika mapenzi kwa ajili ya mikumbo, tamaa, ushindani wa mambo fulanifulani lakini huku wangali bado sana kujua wanahitaji kuwa na wapenzi kwa wakati huo ama la. Hali kadhalika vijana wa kiume pia waeshawishika kuwa na wapenzi kwa sababu ya kuiga, kupenda sifa, kupewa sifa na kulewa nazo na mengine yafananayo na hayo.
Katika hali kama hiyo na ikiwa tamaa, ushindan, mikumbo, kuiga na mengine kama hayo ndiyo itakuwa kichocheo cha Hamida na Charles kuwa wapenzi hapana shaka ni dhahiri penzi hapo halipo na hivyo kuishia kwenye maumivu makali sana juu yao kwani ni lazima mmoja kati yao atajeruhiwa pale atakapofikia hatua ya kutambua kwa kina maana ya Mapenzi na Mpenzi anayetakiwa kuwa chaguo lake halisi.
Hali kadhalika hata maisha ya ndo pia yamevamiwa na mustakabali kama huu. Kuna walioona tu kwa kuwa wazazi wao walipenda iwe hivyo na watoto wakalazimika kutekeleza ili wasiwakwaze wazazi wao ama ndugu zao. Ndoa hii huwa haina mwisho mzuri kwa kuwa ndani ya miyo ya wanandoa hawa wamelazimishwa kuridhiana na hivyo hawafurahishi nafsi zao kwa kuwa pamoja bali wanaridhisha nafsi za wazazi wao ama ndugu zao.
Wazazi hufanya hivyo kwa mitazamo mbalimbali ikiwamo ya heshima ya kifamilia iliyopo baina ya familia hizo mbili, misingi ya dini, uwezo wa kifedha hasa alionao mwanaume anayeoa, makabila na vitu kama hivi. Ikitazamwa kwa msingi wa ndani zaidi ni lazima wawili hawa watoshekane ndani ya nafsi zao na hivyo vyote vingine viwe ni vigezo ambukizi katika mapenzi yao na sio kikwazo. Ndoa iliyopata shinikizo la aina hii huishia kwenye majeraha ya mapenzi na kusababisha hasara kubwa kwa wanandoa hao na hata wale watoto waliojaaliwa kupata katika kipindi hicho kifupi walichokuwa pamoja.
Wasichana na wavulana pia wanayo kasumba ya kukurupuka katika kuingia kwenye mahusiano. Hakuna tafakari ya tahadhari ya kutosha ambayo wawili wa sasa huichukua kabla ya kukubali mualiko unaowahitaji kuwa wapenzi. Pia kuna tabia ya uongo iliyotawala kwa vijana wa kiume ambao wamekuwa wakijinadi uongo ili mradi tu watimize haja zao za kumpata msichana fulani ili marafiki zake wamsifu......hii imekuwa na hatari sana kwa kuwa kuna mashindano ya wazi kabisa yanayofanya hata wahusika kuwa na wapenzi zaidi ya wawili kwa wakati mmoja na hii si kwa wanaume wala wanawake.
Kutokana na uongo uliotumika kukutana kwa wapenzi wa aina hii nachelea kusema hainishawishi kusema ya kwamba ndani yao pia uaminifu ni hafifu. Kwa kukosa uaminifu lazima mapenzi haya yatawaliwe na maumivu makali.
Labda nadhani ipo haja ya msingi kabisa ya kuhakikisha ya kwamba watu wanabadili mienendo yao ili kuleat uwiano katika suala hili na kuwa na mapenzi ya dhati. Ni ngumu sana kumlia mtu yamini lakini ni vyema pia tukajenga roho za kuaminiana miongoni mwa wapenzi ili kuepa dhana na hivyo kuishi kwa raha mustarehe.
Wapo wale wafitini pia ambao wao kila siku hujisikia kichefuchefu wanapoona wawili wamependana sana na hawana mitafaruku ya kijinga. Kazi yao kubwa huwa ni kuhakikisha mapenzi hayo yanapotea ili roho zao zilidhike. Watu hawa waweza kuwa ndugu wa damu kabisa, Marafiki wa karibu na kadharika. Furaha yao ni kuona mmesambaratika japo wanajua kabisa wao hawawezi kuchukua nafasi ya mmoja kati ya wapenzi ninyi.
SIo vizuri kuruhusu maneno ya nje yakapenya katika ngome yenu ya mapenzi na kuisambaratisha eti kwa kuwa tu aliyekuambia ni mzazi, ndugu ama rafiki. Wapo waliojeruhiwa kwa nidhamu ya uoga, wapo waliojeruhiwa kwa kushindwa kutanabaisha ukweli wa mambo na hivyo kufa na tai shingoni. Wengine walitamkiwa maneno mazito na wazazi wao yakawaogofya na hivyo kuamua kujichinja wenyewe ili kuwaridhisha wazazi.
Ni vyema tukazingatia na kuilinda misingi ya mapenzi kwa walio ndani ya duara hili na kusimama kidete kutetea kila inapobidi kufanyika hivyo na kisha tumuombe Mungu atuimarishe katika mapenzi yetu yale halali.