JISOMEE HAPA CHINI..
KWANI ADAM NA HAWA WALIKUWA RANGI GAN
Biblia kitabu cha Mwanzo kinasema; wote tunatoka kwa Adamu na Eva. Ninahisi kuwa hao Adamu na Eva walikuwa weupe ndiyo asili ya wayahudi. Hivi je, waafrika, yaani watu weusi tulitoka wapi?
nafurahi sana kuwa u msomaji wa biblia, na nafurahi pia kuwa wewe una imani thabiti juu ya Mungu aliyetuumba tukianzia na wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva. Hata hivyo, nasikitika kuwa biblia inakuacha njia panda unapojitazama na kujiona kuwa mweusi wakati kichwani una wazo kuwa wazazi wetu wa kwanza walikuwa weupe!
Ni kweli kwamba watu wa kwanza kuumbwa walikuwa wawili tu, mwanaume na mwanamke walioitwa Adamu na Eva. Na ukweli wa jambo hilo unathibitishwa kwanza katika biblia hasa katika kitabu cha mwanzo ile sura ya 1:27-28a. Inasomeka hivi,
Mungu akaumba mtu kwa mfano wa Mungu alimwumba mwanaume na mwanamke
Katika Agano Jipya Bwana wetu Yesu Kristo kusisitiza kuwa walioumbwa kwanza ni watu wawili tu yaani Adamu na Eva, alisema hivi,
Hamkusoma ya kuwa yeye aliyeumba mwanzo, aliwaumba mume na mke? mwisho wa kunukuu. Mt 19:4.
Ushahidi mwingine ni wa kuenea kwa dhambi ya asili, dhambi ambayo walioifanya walikuwa wazazi wetu wa kwanza yaani Adamu na Eva. Dhambi hiyo imeenea kwa kila binadamu wote. Ndiyo kusema, kama Mungu angekuwa ameumba watu zaidi ya Adamu na Eva, wenye kuambukizwa dhambi hiyo wangekuwa ni wale tu wa uzao wa Adamu na Eva.
Uthibitisho mwingine wa kwamba hapo mwanzo Mungu aliumba watu wawili tu yaani Adamu na Eva na kutokana na hao wawili sisi tumepatikana (yaani binadamu wote) ni jina letu. Watu wote duniani wanaitwa binadamu. Maana yake bin-Adamu, hakuna anayeitwa binjiwe. Hiyo ni ishara wazi kwamba watu wote shina lao ni Moja tu yaani Adamu na Eva kama baba na mama yao.
Hizo ni baadhi tu ya thibitisho la imani yako kuwa hapo mwanzo Mungu aliumba kwanza watu wawili tu, Adamu na Eva na kutokana na hao, binadamu wote wamepata kuwepo duniani. Hivyo hilo unaloamini ndilo unalopaswa kulishika na kuwaambia wengine.
Katika swali linauliza kuwa hao Adamu na Eva ndiyo wazazi wa wayahudi na hao Adamu na Eva walikuwa weupe kama walivyo wayahudi, je sisi kama binadamu, yaani wa uzao wa Adamu hivyo mbona tu weusi? Sasa huo weusi tumeupata wapi? Kabla ya kukupa jibu la swali lako, naomba kwanza nikuweke sawa kwa jambo hili,
Ni kweli kuwa wayahudi ni weupe kama ulivyosema katika swali lako na ni kweli kuwa wayahudi wametokana na Adamu na Eva kwa sababu wayahudi ni watu na watu wote wametokana na Adamu na Eva hivyo lazima Adamu na Eva wawe ndiyo asili ya wayahudi, kama ilivyo kwa binadamu wengine kama vile wazungu, waasia, wachina waafrika n.k.
Lakini naomba nikuondoe hisia kwamba Adamu na Eva walikuwa weupe kama wayahudi. Najua utashtuka sana kwa maneno hayo, lakini baada ya muda si mrefu utanielewa ninachotaka kukuambia.
Ni hivi Biblia haisemi lolote juu ya rangi waliyokuwa nayo Adamu na Eva kama vile ambavyo haisemi kuwa watu hao wa kwanza walikuwa wafupi au warefu, wanene au wembamba. Na kama haisemi na leo hii sisi tunawaona waiskimo, watu walio wafupi kabisa duniani wao wametoka wapi? Au tunawaona watu warefu kama waingereza na wao wametoka wapi. Au tunawaona wachina watu wanene kama baadhi ya wachina-wao wametoka wapi. Leo hii tunawaona watu wembamba kama waingereza hata tukawaita English figure wao nao wametoka wapi. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, kama vile ambavyo hatujui kama Adamu na Eva walikuwa warefu au wafupi, wanene au wembamba ndivyo ambavyo hatuwezi kusema kwa uwazi kuwa Adamu na Eva walikuwa weupe kama walivyo wayahudi.
Inafaa tufahamu kwamba, wayahudi ni kweli kuwa ni weupe, lakini wayahudi kama taifa lisihesabiwe kuwa ndilo uzao wa moja kwa moja wa Adamu na Eva na hivyo tukitaka kujua rangi ya Adamu na Eva basi tuwatazame wayahudi, la hasha! Kwa taarifa tu, taifa la wayahudi lilianza kupata historia yake baada ya mwito wa Abrahamu ambaye aliishi miaka zaidi ya maelfu baada ya kuumbwa kwa Adamu na Eva. Hilo urejee Mwanzo. 5-12. ninachotaka kusema hapa ni kwamba, baada ya Adamu na Eva hadi kipindi cha Noah yaani kipindi cha gharika kuu iliyoangamiza watu wote duniani, kulikuwa na watu wengi sana duniani kwani tayari ilikwishapita miaka zaidi ya elfu mbili. Tena baada ya gharika kuu iliyomnusuru Noah tu na wana hadi Abraham ambaye wayahudi wanamhesabu kama ndiye babu yao aliyechaguliwa miongoni mwa mataifa mengi, ilipita miaka zaidi ya elfu moja na hivyo kulikuwa na watu wengi duniani wakiwemo weusi-kama kwani wakati huo bara la Afrika lilikuwapo.
Kuthibitisha kuwa wakati huo, yaani kabla ya kuitwa kwa Abrahamu tayari dunia ilikuwa na watu wa rangi mabalimbali, kutajwa kwa majina ya watoto wa Hamu ambaye alikuwa mmoja kati aya watoto wa Noah. Watoto hao ni Misri na Kushi. Kumbe Misri ni sehemu ya Afrika hali kadhalika Kushi ni eneo la Ethiopia ya sasa ambako watu wake ni weusi. Rejea Mwanz. 10:6. Hapo zamani majina ya watu ndiyo pia yalikuwa yanachukua majina ya mahali. Miaka mingi baadaye ndipo Abrahamu ambaye alitokana na ukoo wa Shemu aliyekuwa mmoja wa wana wa Noah alipopata kuwapo. Rejea Mwanzo. 11:10-31.
Kuhusu Agano kati ya Mungu na Abrahamu rejea kitabu cha Mwanzo 17:1-24.
Mpaka hapa bado sijakupa jibu la swali lako la kuwa wewe au watu weusi wametoka wapi. Kama umenifuata vizuri wewe mwenyewe unaweza kubaini kwamba watu wa rangi zote wametokana na Adamu na Eva kama vile ambavyo watu wa maumbile mbalimbali wametokana na wazazi hao wawili. Sasa, walikujaje? Hapa sasa uniruhusu nikupe hoja za kisayansi. Lakini kabla ya kukupa hoja hiyo naomba ukubali kwamba kama vile ambavyo biblia haisemi kuwa mtu wa kwanza alikuwa wa rangi gani, nami nakuambia kuwa inawezekana mtu wa kwanza yaani Adamu na Eva si lazima kuwa walikuwa weupe na inawezekana wazazi hao walikuwa weusi kuliko weupe kama wanavyodhani watu wengi na wewe pia. Nasema walikuwa weusi kwa sababu, kinachofanya watu watofautiane katika rangi ni mazingira. Watu wengi wanaoishi katika ukanda wa Ikweta ni weusi kwani sehemu hiyo ina jua kali sana, hivyo rangi hiyo nyeusi ni muhimu katika kuwalinda watu hao dhidi ya magonjwa ya ngozi kama kansa yanayotokana na mionzi ya jua.
Weusi huo hutaokana na muunganiko wa chembechembe hai iitwayo melanini iliyopo katika vishina vya vinyoleo ambavyo huwa ni vyeusi. Lakini kadiri watu wanavyoishi mbali na ukanda wa Ikweta ambako jua hupungua makali yake, melanini pia hupungua na hata kutoweka kabisa na hivyo mtu aishiye maeneo hayo yenye jua hafifu huwa mweupe kwa sababu ya kukosa chembechembe hizo kwa sababu hawazihitaji katika mazingira yale ya jua hafifu. Ndiyo maana watu wanaoishi Kongo katika Afrika ni weusi zaidi kuliko wale wanaoishi Afrika kusini na Afrika ya Kaskazini ambako makali ya jua yamepungua. Au ukienda India, wahindi wanaoishi upande wa kusini si weupe kama wale wa Kaskazini, wao ni wekundu au weusi kabisa kwa sababu upande huo umepitiwa na Ikweta hivyo kuna joto na jua kali. Au ukienda Amerika ya kusini kama vile Brazil. Watu wa kule wengi ni weusi sababu si tu kwamba weusi hao walitoka Afrika kipindi kile cha utumwa, la hasha! Historia inatuambia kwamba wakazi wa asili wa Amerika ya kusini ni wahindi wekundu ambao nimekuambia kuwa wapo pia upande wa kusini wa India.
Ninachosema hapa ni kwamba, Mungu aliumba watu wawili tu Adamu na Eva, lakini watu walivyoongezeka mno duniani na kwenda kuishi sehemu mbalimbali duniani zenye mazingira na hali ya hewa tofauti zikawafanya watu hao wawe na rangi inayotofautiana kadiri ya mazingira waliyoishi na kuzaliana. Kwa mfano, watu walioenda kuishi mazingira kama ya Ulaya ambako melanini haihitajiki walipata kuwa weupe kama wayahudi, wale waliokwenda kuishi katika mazingira ambayo kuna jua kali na hivyo melanini inahitajika wakawa rangi yao nyeusi kama unavyowaona waafrika sababu katika Afrika kuna jua kali na hivyo melanini inatakiwa.
Hapo awali nilidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba Adamu na Eva walikuwa weusi na si weupe kama watu wengi wanavyodhani. Tena wapo watu wanaosema kuwa watu weusi walitokana na uzao wa Hamu mtoto wa Noah ambaye baba yake alimlaani baada ya kuutazama uchi wa baba yake. Mwanzo 9:20-27. Habari hizo ni za uwongo zilizotungwa na wazungu wa karne ya kumi na tisa waliotaka kuhalalisha biashara halamu ya utumwa kwa kusema kuwa waafrika ni uzao wa Hamu ambaye alilaaniwa na hivyo waafrika wamelaaniwa ndiyo maana ni halali kuwa watumwa.
Hoja ya kwamba huenda wazazi wetu wa kwanza yaani Adamu na Eva walikuwa weusi inatolewa na wanasayansi wengi wakitoa hoja kwamba ni rahisi kwa mtu kubalika kutoka weusi kwenda rangi nyingine kuliko kutoka weupe kuja weusi. Kwa hoja hiyo, wanadai kwamba kama Adamu na Eva wangekuwa weupe basi watu weusi wasingepatikana. Hata katika mazingira ya kawaida watu waliozaliwa weupe hawawezi kujifanya weusi ila weusi wanaweza kujifanya weupe.
Ni kweli kwamba wayahudi ni weupe, na ni kweli kwamba Adamu na Eva walikuwa wazazi wa kwanza wa watu wote pamoja na wayahudi. Ni kweli pia kwamba hapa duniani kuna watu weusi kama walivyo waafrika. Utofauti au asili ya rangi hizo tofauti umetokana na mabadiliko ya kimazingira ambamo watu wamekuwa wakiishi. Lakini biblia haituambii kuwa watu hao wa kwanza yaani Adamu na Eva walikuwa wa rangi gani; yawezekana walikuwa weupe au pia yawezekana walikuwa weusi kama wanasayansi wengi wanavyosema wakitoa hoja zao za kisayansi. Hivyo usidhani kuwa wayahudi au watu weupe wataanza kuwahodhi Adamu na Eva wakidai kuwa ndiyo wazazi wao halisi na sisi watu weusi tumepatikana kwa ajali tu. Siyo hivyo hata kidogo.
Kuelewa kwamba biblia haikuwa na lengo la kuweka rekodi ya namna gani kitu kilivyoanza. Kitabu cha Mwanzo kinatoa masimulizi ya namna gani binadamu na ulimwengu kwa jumla ulivyoanzishwa kwa mkono wa Mungu. Kwa namna ya pekee, kitabu hicho kinatoa masimulizi ya namna gani binadamu alianza na si namna watu walivyoanza. Watu wote weusi kwa weupe wote ni binadamu walioumbwa na Mungu wakianzia kwa wazazi wao Adamu na Eva. Mabadiliko ya kimazingira ndiyo yaliyowafanya waonekane tofauti baada ya miaka ya miaka min