Hivi karibuni serikali ya Rais Donald Trump ilitangaza orodha mpya ya nchi ambazo raia wake wanawekewa vizuizi vya kuingia Marekani. Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani inasema orodha hiyo inahusisha nchi zilizothibitishwa kuwa na upungufu sugu na mkubwa katika ukaguzi, uhakiki, na kubadilishana taarifa ili kulinda usalama wa taifa na usalama wa umma wa Marekani.
Orodha hiyo imeongeza nchi tano (Burkina Faso, Mali, Niger, South Sudan, na Syria) kwenye orodha ya marufuku kamili, na nchi nyingine 15 (Angola, Antigua na Barbuda, Benin, Cote d’Ivoire, Dominica, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Tanzania, Tonga, Zambia, na Zimbabwe) kwenye orodha ya marufuku kiasi.
Ukiangalia orodha hiyo ya nchi 20, nchi 16 ni nchi za Afrika, na visingizio vilivyotajwa ni sababu za usalama wa taifa na usalama wa umma. Moja kati ya mambo ambayo yana ukweli ni kuwa Marekani ina changamoto kubwa ya usalama wa umma, vitendo vya uhalifu na hasa mauaji ya kutumia bunduki ni jambo la kawaida, na mara nyingi kila tukio kama hilo linapotokea, wachambuzi na wanasiasa wa mrengo wa kulia mara nyingi wanajitahidi kuunganisha matukio haya na wageni, wakijaribu kuyatumia kuendeleza siasa za chuki. Lakini wanasikitika sana kuona kuwa wahalifu wengi ni wamarekani wenyewe na sio wageni.
Kinachofanywa na serikali ya Rais Trump, bila shaka ni chuki yake binafsi na ubaguzi alionao dhidi ya waafrika ambavyo amevionesha tangu awamu yake ya kwanza alipokuwa madarakani. Lakini kwa sasa ni mbinu na ujanja anaoutumia kuweka shinikizo kwa nchi za Afrika ili kufikia malengo yake ya kisiasa na kiuchumi.
Kuna kila dalili inayoonesha kuwa mvuto wa Rais Trump kwa wamarekani unaendelea kupungua, hasa baada ya kuona kuwa ahadi nyingi alizotoa yalikuwa ni maneno matupu, na kimsingi ameshindwa kutekeleza. Tangu aliposema kuwa atasimamisha mgogoro wa Ukraine hata kabla ya kuapishwa kuwa Rais, atapunguza mfumuko wa bei, kuifanya Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani, na kufanya nchi zote zisujudu kwa hatua zake za ushuru, watu wamekuwa wanasubiri kuona kama kweli Trump anaweza kufanya hayo. Kushindwa kwake kufanya hivyo kumemfanya Trump aone aibu na atafute shabaha rahisi inayoweza kurudisha ushawishi wake kwa wafuasi wenye mrengo wa chuki na uhasama dhidi ya Afrika, kama yeye mwenyewe.
Inawezekana kuna ukweli kiasi kuwa nchi za Afrika hazina uwezo mkubwa kwenye kusimamia maswala yanayotumiwa kama kisingizio na serikali ya Trump, lakini hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa nchi hizo ni tishio la usalama wa taifa au usalama wa umma kwa Marekani.
Tabia ya Rais Trump kutumia maswala ya kisiasa kutafuta maslahi ya kiuchumi sasa imekuwa wazi kabisa, hili tunaweza kuliona kwenye nchi ambazo hazipo kwenye orodha ya nchi inazoziwekea vizuizi. Kuna nchi ambazo zina mazingira yanayofanana kabisa, au hata kuwa na mazingira mabaya zaidi kuliko nchi zilizo kwenye orodha hiyo, lakini kutokana na kuwa zimekubali amri ya Marekani kupokea wahamiaji wanaofukuzwa Marekani, na kwa kuwa zimekubali kuingia kwenye makubaliano ya biashara ya madini, hazipo kwenye orodha hiyo.
Kwa watu wanaofuatilia hali inavyoendelea nchini Marekani wanajua kuwa tishio la usalama wa taifa wa Marekani linatokana na utekelezaji wa sera yake ya mambo ya nje, na wala halitokani na udhaifu wa nchi za Afrika kusimamia pasi zake za kusafiri, na matukio ya usalama wa umma ya Marekani pia hayaletwi na watu kutoka Afrika, bali yanatokana na kukosekana kwa haki ndani ya Marekani. Hatua za Rais Trump kuzuia watu kutoka Afrika haziwezi kubadilisha hali hiyo, na bahati mbaya pia haziwezi kubadilisha hali ya kushindwa kutekeleza ahadi zake.