Kwaresma: Njia ya Msalaba

Kwaresma: Njia ya Msalaba

Sang'udi

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2016
Posts
9,138
Reaction score
22,236
Tufwate njia ya msalaba
Tuifwate mpaka Kalvario
Tusimamepo bila haya
Msalaba, Msalaba, huponya roho
Sala mbele ya altare
Ee Mkombozi wangu, nimekuja leo kufuata njia ile uliyoshika siku ya kufa sadaka yetu. Nimetubu dhambi zangu zote; ninataka kugeuza mwendo wangu; ninaomba kwako niwapatie roho za waamini marehemu waliomo toharani, rehema zote zilizotolewa na Kanisa kwa njia ya msalaba.

Nawe Maria Bikira Mtakatifu, uliyefuata njia ile ya nyuma ya mwanao Yesu, uniangalie kwa wema, unitie moyo mkuu, nisipende dhambi tena, nikivumilia kazi na usumbufu na mateso na matukano yatakayonipata.
 
Kituo 01.jpg

Umekosa nini we Yesu
Kushtakiwa bure kwa Pilato
Wenye kustahili hukumu
Si wewe, si wewe Bwana, ni sisi

KITUO CHA KWANZA

Yesu anahukumiwa afe
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Pilato anamhukumu Yesu ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi. Anabembeleza urafiki wa Kaisari.

Ee Yesu usiye na kosa, hata mimi ningeweza kutenda mema mengi, lakini naogopa macho ya wenzangu, na maneno yao. Ee Bwana, niimarishe utashi wangu, nijitegemee katika kushika madaraka yangu.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 02.jpg

Ole msalaba huo mzito
Apagazwa Mwana mpenzi wa Mungu
Mwili waenea mateso
Alipa, alipa madhambi yetu.

KITUO CHA PILI

Yesu anapokea msalaba
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Yesu anakubali kuupokea msalaba kwa ajili ya wokovu wa watu. Ndivyo alivyonifundisha moyo wa sadaka, moyo wa kujitolea na kujisahau kwa ajili ya wengine.

Ee Yesu wangu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu kwa Mungu, kwa umma na kwa Kanisa. Hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee Yesu niyapokee bila kunung’unika, na kuyabeba vyema.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 03.jpg

Ona Muumba mbingu na nchi
Yupo chini mzigo wamwelemea
Na mtu kiumbe chake kwa ukali
Ampiga, ampiga bila huruma.

KITUO CHA TATU

Yesu anaanguka mara ya kwanza
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Yesu amedhoofika sana, anaanguka chini, kisha anasimama, anaendelea na safari ya ukombozi.

Ee Yesu uliyeanguka chini ya msalaba kwa ajili ya udhaifu ukasimama tena; usiniache katika tamaa nikianguka dhambini, bali nisimame mara moja, nikufuate.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 04.jpg

Huko njiani we Maria
Waonaje hali ya mwanao
Ni damu tupu na vidonda
Machozi, machozi yamfumba macho.

KITUO CHA NNE

Yesu anakutana na Mama yake
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Wote wawili mama na mwanae wanaumia sana moyoni kwa ajili ya dhambi zangu.

Ee Yesu Mwana wa Maria, unitilie moyoni mwangu upendo na ibada kwa Bikira Maria: unijalie na ulinzi wake, nisitende dhambi tena.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 05.jpg

Kwa Simoni heri ya kweli
Mimi pia Yesu nisaidie
Kuchukua mzigo wa ukombozi
Kuteswa, kuteswa pamoja nawe.

KITUO CHA TANO

Simoni wa Kirene anamsaidia Yesu
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Nausifu ukarimu wa Simoni wa Kirene. Ee Bwana unijalie ukarimu kama huo, nitie ushujaa kama huo, niitikie nami wito wa kukusaidia kuchukua msalaba.

Nitoe zaka na michango yote ya uenezaji wa dini. Nijitolee mimi mwenyewe katika kazi ya maendeleo ya dini. Uwajalie vijana wengi wito wa Upadri, waweze kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia. Uwaimarishe viongozi wa dini. Ustawishe moyoni mwa waamini wote mwamko wa utume.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 06.jpg

Uso wa Yesu malaika
Bethlehemu walikuabudu
Bahati yake Veronika
Kupangusa, kupangusa mfalme wa mbingu.

KITUO CHA SITA

Veronika anapangusa uso wa Yesu
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Mama huyu ni kinyume kabisa cha Pilato. Veronika anajua analopaswa kutenda, na analitenda bila kujali macho na maneno ya makundi ya watu waovu.

Ee Yesu uliyemtuza Veronika zawadi ya picha ya uso wako juu ya kitambaa, unijalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema, ili roho yangu ipambwe kwa chapa ya uungwana na utakatifu wako.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 07.jpg

Wakimvuta huku na huku
Wauaji wanamchokesha bure
Chini wamtupa bado kwa nguvu
Aibu, aibu yao milele.

KITUO CHA SABA

Yesu anaanguka mara ya pili
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu uliyelegea mno kwa mateso makali, unapoanguka mara ya pili kwa ajili ya udhaifu wa mwili, wanionya kwamba hata mimi naweza kurudi dhambini kwa udhaifu wa moyo.

Nipe basi neema ya kuepuka nafasi za dhambi na visa vyenye kunikwaza na kunirudisha dhambini.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 08.jpg

Wanawake wa Israeli
Musilie kwa sababu hiyo
Walilieni hao kwa dhambi
Upanga, upanga ni juu yao.

KITUO CHA NANE

Akina mama wanamlilia Yesu
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Asanteni sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma.

Ee Yesu uliyetulizwa na wanawake, unipe moyo wa kuwaheshimu akina mama wote. Uwaite na wasichana wengi waingie utawa, ili watulize Moyo wako mtakatifu kwa sala na sadaka zao.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 09.jpg

Mwokozi sasa ni ya tatu
Waanguka chini ya msalaba
Katika dhambi za ulegevu
Nijue, nijue kutubu hima.

KITUO CHA TISA

Yesu anaanguka mara ya tatu
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu unayezidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu, upate kunistahilia neema ya kuutiisha mwili wangu na kuusulubisha. Licha ya kuepuka nafasi za dhambi.

Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee Yesu mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 10.jpg

Mje malaika wa mbingu
Funikeni mwiliwe kwa huruma
Vidonda vyake na utupu
Askari, askari wamemvua.

KITUO CHA KUMI

Yesu anavuliwa nguo
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Askari wanamvua kwa nguvu nguo yake, iliyogandamana na madonda yake; wanayaamsha mara moja mateso yote aliyoteswa tangu mwanzo.

Ee Yesu unayavumilia mateso makali haya, upate kunifundisha kuuvua kwa nguvu moyoni mwangu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu urafiki wa Mungu, hata ikinipasa kutoa sadaka kubwa.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 11.jpg

Hapo mkristo ushike moyo
Bwana wako alazwa msalabani
Mara miguu na mikono
Yafungwa, yafungwa kwa misumari.

KITUO CHA KUMI NA MOJA

Yesu anasulibiwa msalabani
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu uliyepigiliwa misumari msalabani, nakutolea akili na utashi wangu, vifungwe pamoja na miguu yako, nipate kuwaza, kusema na kutenda siku zote yale tu yanayolingana na utukufu wa msalaba wako mtakatifu.

Ee Yesu, mimi ni mfungwa wako. Nisaidie kuimarisha kifungo hicho kwa sala, Sakramenti na fadhila za kikristo.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 12.jpg

Yesu mpenzi nakuabudu
Msalabani unapohangaika
Nchi yatetemeka kwa hofu
Na jua, na jua linafifia.

KITUO CHA KUMI NA MBILI

Yesu anakufa msalabani
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu uliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, unijalie nichukie dhambi, nisiishi kamwe katika dhambi.

Nifahamu kwamba nilipobatizwa kwa jina lako, nilibatizwa katika mauti yako, ili utu wangu wa kale usulibiwe nawe, mwili wa dhambi uangamizwe, nisitumikie tena dhambi.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 13.jpg

Mama Maria mtakatifu
Upokee maiti ya mwanao
Tumemwua kwa dhambi zetu
Twatubu, twatubu kwake na kwako.

KITUO CHA KUMI NA TATU

Yesu anashushwa msalabani
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu uliyeshushwa msalabani baada ya kufa, unijalie nidumu katika maisha ya kujitoa sadaka mpaka siku ya kufa kwangu.

Nielewe na nikubali kwamba baada tu ya kufa ndio mwisho wa vita na mashindano ya kikristo.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Kituo 14.jpg

Pamoja nawe kaburini
Zika dhambi na ubaya wa moyo
Yesu tuwe wakristo kweli
Twakupa, twakupa sasa mapendo.

KITUO CHA KUMI NA NNE

Yesu anazikwa kaburini
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Ee Yesu, ulizikwa kaburini, ukafufuka siku ya tatu. Mimi pia nilizikwa pamoja nawe kwa njia ya Ubatizo katika mauti yako.

Kwa vile wewe ulifufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, unijalie nami nifufuke, yaani nishike mwenendo mpya, mwenendo wa uzima wa neema.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
Katika roho yangu Bwana
Chora mateso niliyokutesa
Nisiyahau madeni
Na kazi, na kazi ya kuokoka.

(Hiari yako – mbele ya altare)

KITUO CHA KUMI NA TANO

Yesu amefufuka
  • Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru.
  • Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.
Habari njema aliyotuletea Yesu ni kwamba baada ya kila Ijumaa Kuu huja sikukuu ya Pasaka; kwamba punje ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali hiyohiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi.

Twakushukuru, ee Yesu, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.

Baba yetu – Salamu Maria – Atukuzwe Baba.
K. Ee Bwana utuhurumie W. Utuhurumie
Roho za waamini wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa Amani. Amina.
 
SALA YA MWISHO

Mbele ya Altare: Yesu wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu.

Nawe Maria Mamangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona mwanao mpenzi kuinama kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema.
 
Ninawatakia Wakristo wote, na kwa namna ya pekee Wakatoliki, mfungo mtakatifu wa Kwaresma. Tudumu katika sala, kufunga na kutoa sadaka.

PS: Mods ninaomba msiuunganishe huu uzi ili iwe virahisi kuu-access kwa watakaoweza kuutumia wakati wa sala.
 
Back
Top Bottom