SIKU chache baada ya Yanga kumtema, Hamis Kiiza na nafasi yake kupewa Mliberia Kpah Sherman, mchezaji huyo raia wa Uganda ameibuka na kusema ipo siku timu hiyo itaukumbuka mchango wake kikosini.
Kwa muda mrefu Kiiza hakuwa na maisha mzuri ndani ya kikosi cha Yanga chini ya Kocha Marcio Maximo akikosa nafasi kikosi cha kwanza na awali alinusurika kutemwa mwanzoni mwa usajili, lakini akaachwa siku chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa.
Hata hivyo, Maximo naye amesitishiwa mkataba wake pamoja na msaidizi wake Leonardo Neiva na kiungo raia wa Brazil, Emerson Roque ambaye amempisha Amissi Tambwe.
Kiiza ambaye kwa sasa anatajwa kujiunga na URA ya Uganda, aliliambia Mwanaspoti kuwa ipo siku Yanga itaukumbuka mchango wake katika timu na itakuwa imechelewa kumrejesha kwani atakuwa amepiga hatua nyingine kisoka kwani anaamini ana kiwango kizuri cha kuendelea kucheza soka kwa mafanikio.
Bado naamini nina uwezo mkubwa, nimekaa Yanga kwa kipindi kirefu na niliweza kuisadia japo kwa sasa muda umefika wameniacha, mimi ni mchezaji na soka ndiyo kipaji na ajira yangu, hivyo naamini nyota yangu ya soka ilipotea chini ya Maximo, bado nina imani kwamba kuna siku nitakumbukwa kwa mchango wangu Yanga, alisema.
Hatua waliyochukuwa inaweza kuwa ni sahihi kwao, Yanga ni timu kubwa na bado ina wachezaji wazuri, siyo kwamba kuondoka kwangu kutaifanya Yanga iyumbe, hapana, kuendelea kuwepo ama kuachwa ni moja ya maisha ya soka kwa mchezaji.
Yanga sasa imebaki na wageni watano ambao ni Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Sherman (Liberia), Tambwe (Burundi) na Andrey Coutinho wa Brazil.