Mwanachama Mwandamizi wa Jamii FORUM ambaye anaishi Uingereza Bwana Mwakalinga ametangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge jimbo la Kyela 2010.
Kwa Mwakyembe moto!
*Mpizani wake Uchaguzi Mkuu 2010 ajitangaza
*Ni Mtanzania mtaalamu wa kompyuta anaishi Uingereza
Monday, 03 August 2009 07:27
Na Israel Mwaisaka, Kyela
MWANACHAMA mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayefanya kazi nchini Uingereza Bw. George Mwakalinga ametangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge Jimbo la Kyela kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa 2010
Akizungumza na gazeti hili juzi, Bw. Mwakalinga, alisema ameamua kuweka wazi nia yake baada ya kuona Jimbo la Kyela linazidi kudorora kimaendeleo kama yatima asiye na mlezi.
Alisema Chama Cha Mapinduzi wilayani Kyela katika kipindi chote cha awamu hii, kimekumbwa migogoro mikubwa ambayo imeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji maendeleo kutokana na viongozi kuelekeza nguvu zao katika suala hilo.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiendelea hivyo kuzidi kupoteza matumaini ya wananchi wa jimbo hilo ndio maana ameamua kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo muda utakapofika.
Bw. Mwakalinga alidai kuwa Wilaya Kyela imekuwa na huduma hafifu zitolewazo na Serikali zikiwemo za afya, elimu na kilimo kisichokuwa na tija kwa wananchi na ubadhilifu wa fedha za umma mambo ambayo yametokana na kukosekana usimamizi wa kutosha kiuongozi.
Alisema kutokana na uzoefu wake wa uongozi na kufanya kazi mbalimbali barani Ulaya na elimu aliyonayo, anaamini kuwa ataweza kusimamia maendeleo ya wananchi wa Wilaya Kyela na kuhakikisha matabaka yaliyopo sasa kisiasa ndani ya CCM, yanakwisha.
Alisema binafsi mbali ya kuwa na kazi nzuri nchini Uingereza ameamua kuiacha na kurudi nyumbani ili kuwaendeleza watu wa Kyela baada ya kubaini mapungufu mengi yanayosababishwa na kukosekana uongozi thabiti kutokana na migogoro.
Alisema uzoefu wake kiuongozi alioupata ndani na nje utasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yake ya kuwatumikia wananchi wa Kyela kwa kiwango kinachotakiwa na kuwaondolea kero ambazo zimekuwa 'donda ndugu' lisilopona
Alisema kutokana na huduma duni za afya wananchi wengi wamekuwa wakilazimika kukimbilia wilaya jirani ya Rungwe kupata huduma hizo.
Kazi alizowahi kufanya Bw. Mwakalinga nchini Uingereza ni pamoja na kuwa Mhazini wa Jumuia ya Watanzania Waishio Nje ya Nchi (Tanzanet) kwa muda wa miaka 4 na kuwa mmoja wa wanachama waanzilishi na mdhamini wa mtandao wa Jamii Forum.
Bw. Mwakalinga ambaye ni mtaalamu mwandamizi wa kompyuta na simu ana shahada ya pili ya Sayansi ya Kompyuta aliyoipatia katika Chuo Kikuu cha Wroelaw nchini Poland pia ni mtaalamu ya Biashara.
Jimbo la Kyela hivi sasa lipo chini Mbunge wake Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na msimamo wake katika kupambana na ufisadi.
Chati ya mwanasiasa huyo msomi wa sheria aliyebobea, ilipanda zaidi pale alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyochunguza kashfa ya mkataba kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Kufua Umeme wa dharura ya Richond LLC, ambayo ilisababisha mawaziri watatu wa Serikali kujiuzulu.
Mbali ya kujiuzulu mawaziri hao akiwemo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishari na Madini Bw. Mustafa Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Afrika Mashariki, Dkt. Ibrahim Msabaha, 'mzimu' wa Richmond bado 'umeikaba koo' Serikali baada ya Bunge mwishoni mwa wiki kukataa Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo na kutaka iwasilishwe upya kwenye Mkutano wa 17 wa Bunge, Novemba mwaka huu.
habari kamili someni gazeti la Majira.co.tz.