[h=3]JIHADHARI UNAPOTUMIA LAPTOP[/h]
SAYANSI na teknolojia vimechochea kasi ya maendeleo ya sekta mbalimbali hivyo kuiwezesha jamii kupiga hatua katika nyanja anuai.
Maendeleo hayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uvumbuzi wa kila aina duniani.
Kompyuta ni moja ya nyenzo ambazo zimekuwa zikitumika katika sekta mbalimbali kwa lengo la kurahisisha ufanisi katika utendaji kazi.
Zana hiyo hutumika kwa ajili ya kuandika taarifa mbalimbali pamoja na kupata mawasiliano ya intaneti, ambayo huunganishwa na kompyuta.
Kuwepo kwa zana hiyo, kumeleta mageuzi makubwa duniani, ndiyo maana kuna msemo kwamba maendeleo katika sekta ya mawasiliano yameifanya dunia kuwa kijiji.
Katika eneo hilo, uvumbuzi ulianza kwa kutengeneza kompyuta kubwa za mezani lakini kazi hiyo iliboreshwa na kuanza kutengenezwa kompyuta za mkononi maarufu
kama ‘laptop'.
Kompyuta hizo ndogo za mkononi, zimewezesha kurahisishwa kwa kazi na hata mawasiliano kwani mtu anaweza kutumia popote alipo na hata kutuma ujumbe au waraka duniani kote.
Aina hiyo ya kompyuta zinaweza kutumika mtu akiwa ofisini, baa, mgahawani, kwenye basi au kwenye meli. Mtu anayetumia anaweza kuweka mezani au popote anapoona panafaa na kumwezesha kufanya kazi yake bila matatizo.
Kwa watu wengi ambao huwa safarini au sehemu yoyote ambayo haina meza, huweka kifaa hicho kwenye mapaja na kuendelea na kazi zao. Kwa kufanya hivyo, hujisikia raha mustarehe na kazi hufanyika bila wasiwasi.
Pamoja na kompyuta hizo kurahisisha kazi, imeelezwa kuwa kuitumia huku ikiwa kwenye mapaja ni hatari kwa afya.
Awali, ilikuwa ikifahamika kuwa matumizi ya kompyuta kwa muda mrefu yanaweza kumfanya mtumiaji kupata matatizo ya macho na mishipa ya fahamu.
Lakini utafiti uliofanyika hivi karibuni, umebaini kuwa matumizi ya kompyuta ndogo kwa kuiweka kwenye mapaja husababisha ugonjwa wa ngozi na wakati mwingine saratani ya ngozi.
Madaktari waliofanya utafiti huo ambao matokeo yake yalitangazwa Oktoba, mwaka huu, hali hiyo husababishwa na joto la kompyuta hiyo. Joto la kompyuta hiyo hufikia hadi nyuzi joto 52.
Joto linalotokana na kompyuta hiyo, kwa mujibu wa watafiti hao na madaktari bingwa wa tiba ya binadamu, linaweza kusababisha mtumiaji kupata ugonjwa wa ngozi.
Wanasema ngozi ya mtumiaji huwa na vipele vidogo ambavyo baadaye husababisha mapaja kubadilika rangi au kuwa na vidonda.
Katika tukio la hivi karibuni, mtoto mwenye umri wa miaka 12 alikumbwa na madhara hayo katika paja lake la kushoto baada ya kutumia kompyuta ndogo kwa kucheza mchezo kwa saa kadhaa kila siku kwa zaidi ya miezi sita.
Matumizi kama haya ni hatari kwa afya yako. Chukua tahadhari ili usiungue mapajani.
"Kijana huyo alithibitisha kuwa kompyuta aliyekuwa akiitumia ilikuwa ya moto upande wa kushoto, lakini hata baada ya kugundua hakubadilisha namna ya kuiweka wakati wa kuitumia," wanabainisha watafiti hao kutoka Uswisi katika jarida linalohusu tiba ya watoto.
Wanasema mwingine aliyekumbwa na madhara hayo ya kubabuka ngozi kwenye mapaja na rangi yake kubadilika ni mwanafunzi wa sheria nchini Marekani.
Mwanafunzi huyo ambaye ni msichana, alipopata tatizo
hilo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya utafiti, alikwenda kuwaona madaktari wake wa ngozi.
Baada ya kwenda kwa ajili ya kumfanyia uchunguzi, madaktari wake walishangazwa na hali hiyo na walishindwa kubaini nini kilichomsibu. Lakini baadaye waligundua kuwa alipatwa na mkasa huo kwa sababu ya kutumia kompyuta ikiwa kwenye mapaja kwa muda wa saa sita kila siku.
Madaktari hao bingwa walifanya utafiti huo kuanzia mwaka 2007 na wamebaini kwamba watu wengi wameathirika na tatizo
hilo.
Hata hivyo, wataalamu hao wakiongozwa na maprofesa Andreas Arnold na Peter Itin wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Basel, Uswisi, wanasema tatizo hilo linaweza kuwa kubwa lakini ni vigumu kuelezea ni kwa kiasi gani kwa kuwa wengi hawajaripoti na kufanyiwa tiba.
Taarifa hiyo ya utafiti umewafikia watengenezaji wa kompyuta
kama vile Apple, Hewlett Packard na Dell na wameonya kuwa ni hatari kutumia zana hizo zikiwa zimewekwa kwenye mapaja au katika ngozi ambayo haijafunikwa na kitu chochote.
Mwanamdunde: JIHADHARI UNAPOTUMIA LAPTOP