Nov 07, 2023 08:12 UTC
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema: "Kwa sasa tunashuhudia jinsi Anglo-Saxons wanavyoisukuma Asia Magharibi kwenye ukingo wa vita vikubwa. Sera hii imeonekana wazi zaidi katika maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Ukraine."
Sergey Lavrov ameongeza kuwa: "Kuna mifano mingi ya jambo hili, lakini matokeo yake yanafanana: kuangamiza au kudhoofika serikali za nchi, kama zilivyojaribu kufanya huko Iraqi, Libya au Syria."
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema: Matokeo ya sera hizi za nchi za Magharibi ni ongezeko la ugaidi na misimamo mikali, kuporomoka kwa familia na mawimbi ya mamilioni ya wakimbizi.
Hapo awali Lavrov alikuwa amesema kuwa Moscow inalipa kipaumbele cha kwanza suala la usitishaji vita mara moja kati ya pande zinazohusika katika mzozo wa Palestina na Israel.
Russia imewasilisha miswada kadhaa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikisisitiza udharura wa kusitishwa mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza, lakini miswada hiyo imepigwa na nchi za Magharibi washirika wa Israel hususan Marekani.