Hebu jiulize mwanafunzi akipata alama zote mtihani wa darasa la saba kwa masomo matano anapata 250, kwani kila somo linajumla ya alama 50. Miaka ya nyuma kwenda sekondari ilikuwa kufikisha jumla ya alama 100. Hii ilikuwa sawa na ufaulu wa alama 20 tu kwa kila somo, ufaulu ambao hauhitaji kupata nusu ya jumla ya alama. Kama ufaulu ungekuwa nusu ya alama mwanafunzi angelazimika kupata wastani wa alama 125. Kituko ni mwaka huu ambapo Dr. Shukuru Kawabwa pamoja na kudanganya kwa kusema kiwango cha ufaulu kimepanda wamelazimika kuchukua wanafunzi ambao wamepata alama chini ya 100 na kushuka hadi alama 70 hii ni sawa na kupata wastani wa alama 14 kati ya 50 kwa kila somo. Taarifa zisizo na shaka zinaeleza kuwa kwa alama za ufaulu za awali tayari kuna baadhi ya sekondari za kata zilikwisha kosa wanafunzi au kupata wanafunzi chini ya kumi huku sekondari nyingi zikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 120. Ni lazima utakubaliana na mimi kuwa kumlazimisha mzazi kulipa ada na michango mingine ya shule kwa kijana aliyepelekwa sekondari akiwa na alama chini ya 100 ni kumwibia pesa tu kwani kijana huyu hawezi kuvuka mtihani wa kidato cha pili. Kuna tetesi pia kuwa matokeo ya mtihani wa kidato cha pili ni mabaya sana. Ni wanafunzi wachache sana waliofikisha alama ya kufaulu ya 30. Kama serikali isipochukua uamuzi wa kushusha alama hizi walau kufikia 15 zipo shule za kata zitakosa wanafunzi wa kidato cha tatu mwakani. Tujiulize tunaelekea wapi?.