Salim Said Salim
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania iliyounganisha Bara (Tanganyika) na Visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar) leo imetimiza miaka 44 tokea kuundwa kwake.
Muungano huu ulikuja kwa kushitukizia. Wananchi hawakuutarajia kwa vile hapakuwepo fununu wala minongono juu ya kuundwa kwake.
Tangazo la kuundwa kwake, lilitokana na mkutano uliofanyika Dar es Salaam kati ya aliyekuwa Rais wa Tanganyika (enzi hizo), Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Wolfango Dourado, amesema mara kwa mara hakushauriwa na hakuwa na habari ya mazungumzo ya kuundwa kwa Muungano. Hata baadhi ya mawaziri katika Serikali ya Rais Karume, akiwemo marehemu Abdulrahman Babu, walisema hawakushauriwa juu ya kuundwa kwake.
Wakati ule nikiwa kijana wa karibu miaka 18, nilisikia kwa mara ya kwanza kuundwa kwa Muungano kupitia taarifa ya habari iliyosema Mwalimu Nyerere na Karume wametia saini mkataba wa Muungano.
Mambo yaliotajwa kuwa ya Muungano yalikuwa 11, ikiwa ni pamoja na mambo ya ndani, mambo ya nje na ulinzi.
Katika makubaliano yale, Zanzibar ilikuwa na mamlaka kwa mambo mengi kama fedha, biashara, ushirikiano wa kimataifa, elimu, kilimo na afya.
Siku hizi baadhi ya mambo haya yamekuwa ya Muungano, huku zikisikika kelele kwamba yameingizwa katika orodha hiyo kiujanja ujanja.
Hivi leo, idadi hasa ya mambo ya Muungano haijulikani kwa uwazi. Huyu anasema hili na yule anasema lile. Wapo wanaosema ni 29, wapo wanaoeleza kuwa ni zaidi ya 35 na wapo wanaosema hawajui.
Ukitaka kujua hali halisi, jaribu kufanya utafiti mdogo kwa wabunge au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakiwamo mawaziri, kuwataka wakwambie mambo gani ni ya Muungano na yepi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina mamlaka nayo.
Kama utawauliza watu 20, wakitokea wawili ambao orodha zao zitafanana itakuwa ni miujiza. Si ajabu hata orodha ya Rais wa Muungano, Jakaya Kikwete na ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume nazo zisifanane.
Licha ya kupambana na misukosuko ya kila aina, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wabunge wa Bara kudai kufufuliwa Jamhuri ya Tanganyika na wengine wa Visiwani kutaka mahakama itamke Muungano si halali, Muungano huu umedumu muda mrefu kuliko wowote ule uliofanyika barani Afrika.
Baadhi ya miungano iliyoundwa na baadaye kuvunjika ni kama ule wa Guinea iliyounda muungano wa kisiasa na Ghana mwaka 1958 na Mali ilijiunga 1961, lakini ilipofika 1963 kila nchi ilichukua njia yake.
Rwanda na Burundi, zilikuwa nchi moja mwanzoni mwa karne ya 20 na kujulikana kama Rwanda-Urundi, lakini mwaka 1962 kila upande ukawa nchi.
Senegal na Gambia ziliungana na baada ya muda zikavunja muungano na kugawana mbao. Eritrea ilikuwa sehemu ya Ethiopia, lakini leo ni nchi mbili hasimu.
Guinea Bissau ilikuwa sehemu ya visiwa vya Cape Verde, lakini leo kila moja ni taifa huru. Somalia ni nchi iliyogawanyika vipande na orodha ya majina yake hata wenyewe Wasomali hawaijui.
Mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakati wa kugombea uhuru, lilikuwepo Shirikisho la Nyasaland lililokuwa la nchi tatu ambazo leo ni Malawi, Zimbabwe na Zambia.
Kudumu kwa miaka 44 kwa Muungano wa Tanzania, ni jambo la kupigiwa mfano, lakini ukweli ni kwamba Muungano wa Tanzania una matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kinachosikitisha ni kuona matatizo haya yanafumbiwa macho kama vile hayapo na hayaonekani.
Hivi sasa wapo wanaosema mfumo wa serikali mbili ndio mzuri, lakini wapo wanaotaka uwe wa serikali tatu na wapo waliosema serikali moja ndiyo safi na hata kuwahi kuelezwa na kiongozi wa juu wa CCM kwamba sera ya CCM ilikuwa serikali mbili kuelekea moja. Ziliposikika kelele za kukataa serikali moja kutoka Visiwani, tamko lile likamwagiwa maji ya moto.
Baadhi ya wanasiasa Visiwani na raia wa kawaida wanalalamika hadharani na vibarazani kuwa kila siku zikienda mbele Zanzibar inamezwa ndani ya Muungano na kukandamizwa hasa katika mambo ya uchumi na biashara.
Wengine wanadai Wazanzibari hawana haki ya kuamua mambo yao na lile wanalolitaka wao hupinduliwa linapojadiliwa Bara. Mfano unaotolewa ni katika kura za maoni ndani ya CCM wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi.
Katika Baraza la Wawakilishi suala la uchimbaji wa mafuta kuwa la Muungano lilizusha balaa na viongozi wa Serikali ya Zanzibar kusema mafuta yameingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano kupitia mlango wa nyuma.
Viongozi hawa walitaka dhahabu na almasi ziingizwe katika kikapu cha Muungano na si Bara iendelee kufaidika peke yake na madini hayo.
Kwa upande wa Bara wapo wanaoona Zanzibar inafaidika zaidi na kusema Serikali ya Muungano inaidekeza sana.
Wapo wanaoshangaa kusikia baadhi ya wakati Hazina ya Muungano imetoa fedha kulipa mishahara ya watumishi wa Serikali ya Zanzibar.
Mara kadhaa wapo walioshauri kufanyika kura ya maoni juu ya Muungano, lakini wapo waliohisi baada ya miaka 44 hapana haja ya kufanya hivyo.
Sababu wanayoitoa ni kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya Watanzania wa leo hawajui habari za Tanganyika wala Zanzibar kama dola tofauti.
Badala yake panasikika ushauri wa kura ya maoni juu ya kuundwa serikali ya mseto Zanzibar na mambo ya Muungano.
Lakini masuala ya kuondolewa dhamana ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kama ilivyokubaliwa awali katika mkataba wa Muungano na kuondolewa hati za usafiri kati ya Bara na Visiwani hayasikiki kuzungumziwa kura ya maoni. Kwa kifupi kilichopo ni vurugu tupu.
Mwanasiasa maarufu, Rashidi Kawawa, ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, alisema mwaka juzi kuwa ni dhambi kuhoji uhalali wa Muungano. Hakueleza kwa nini ni dhambi kuhoji Muungano na isiwe dhambi kutaka kura ya maoni kwa suala la serikali ya mseto.
Wapi duniani dhana ya serikali ya umoja wa kitaifa imeonekana kutotakiwa na watu wake, kama watu hao si wachawi? Watanzania tunasema umoja ni nguvu, sasa hivyo umoja huo utajengwa kwa kukataa serikali ya umoja wa kitaifa?
Ukweli ni kwamba Muungano una matatizo, isipokuwa pakitokea mvutano na hata kusikika lugha za hasira kutoka kwa viongozi wa Bara na Visiwani, juhudi za haraka haraka hufanywa kuziba viraka kwa kutumia chandarua.
Hapo utaona panatumika zaidi siasa kupooza tatizo na si kuiangalia hali halisi kwa undani na kupata ufumbuzi wa kudumu.
Kwa ujumla, viongozi kutoka Bara na Visiwani wanapata shida juu ya Muungano. Anavyoona huyu ndivyo mwingine anaona sivyo. Matokeo yake ni kuwababaisha wananchi.
Utasikia huyu anasema suala fulani ni la Muungano na mwingine wa upande wa pili anasema jambo hilo lipo katika mamlaka ya Zanzibar.
Mifano ni suala la Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (IOC) na kujitoa baada ya vuta nikuvute iliyokaribia kupeleka kamba ya Muungano kukatika.
Zanzibar ililazimishwa kujitoa ili Serikali ya Muungano ijiunge, lakini sasa ni zaidi ya miaka 10 na suala hilo haliguswi, huku Wazanzibar wakilalamika.
Zanzibar iliwapeleka mahakamani watu 18 kwa shutuma za kutaka kuipindua serikali na kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour miaka minane iliyopita.
Kinachoonekana hapa ni sawa na kusema mjukuu ni wangu, lakini mama yake au baba yake sikumzaa.
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambayo ni ya Muungano ilisema Zanzibar si dola na kwahivyo uhaini hauwezi kufanyika.
Alipouawa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume mwaka 1972, zaidi ya watu 50 walifunguliwa kesi ya uhaini Zanzibar.
Wakati ule hoja ya kusema uhaini hauwezi kufanyika Visiwani kwa kuwa Zanzibar si dola haikujitokeza. Wakati ule Muungano ulikuwa na miaka minane.
Mwaka jana, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alisema madai ya ukiukwaji haki za binadamu Zanzibar yaliyotolewa bungeni, Dodoma, yangelishughulikiwa na Tume ya Haki za Binadamu ya Muungano.
Serikali ya Zanzibar ikaja juu na kusema tume, ijapokuwa ilikuwa na wajumbe kutoka Visiwani, haikuwa na mamlaka ya kufanya kazi Zanzibar. Sasa Zanzibar imelegeza kamba na tume inatarajiwa kufanya kazi Visiwani, lakini kwa kiasi gani itaweza kutanua mbawa zake Zanzibar haijulikani.
Zipo wizara ambazo si za Muungano ambazo zimekuwa zikiongozwa na Wazanzibari na hili limekuwa likilalamikiwa na kuulizwa kwa nini watu kutoka Bara hawachaguliwi kuwa mawaziri katika Serikali ya Zanzibar? Vile vile wapo Wazanzibari waliogombea ubunge Bara, lakini watu wa Bara ni mwiko kugombea uwakilisha au udiwani Visiwani.
Hii ni hoja ya msingi, lakini hili linafumbiwa macho kwa sababu za kisiasa.
Serikali ya Zanzibar iliikataa Tume ya Kupambana na Rushwa na Ufisadi ya Muungano kufanya kazi Visiwani kwa vile rushwa na ufisadi si mambo ya Muungano.
Rais Kikwete ameonekana kutaka kujaribu kupata ufumbuzi kwa hayo mambo yanayoitwa kero za Muungano kwa kufanyika mazungumzo ya mara kwa mara ya pande mbili.
Mpango huu ni mzuri, lakini suala ni je, nia ya kweli ipo kumaliza hizo kero za Muungano?
Wapo wanaouliza kwa nini watu hawa wachache wawe na kibali cha kuamua hatima ya nchi hii na Rais Kikwete asilione hili jambo muhimu kama suala la serikali ya mseto, na kwa hivyo bora kupata ridhaa ya wananchi kwa kutumia kura ya maoni ili sauti za wananchi zisikike?
Jambo muhimu ni kwa viongozi kuelewa huu ni Muungano wa watu na si wa viongozi pekee au watu wa chama fulani.
Wakati viongozi wanabadilishana mawazo juu ya Muungano na raia nao wapewe nafasi ya kufanya hivyo.
Muungano una matatizo mengi. Faraja iliopo ni kwamba, wachache ndio wanaosema hawautaki, isipokuwa wanatofautiana juu ya mfumo na namna unavyoendeshwa.
Wapo viongozi, hasa wa Zanzibar, ambao huutumia Muungano kama karata yao ya mwisho pale wanapotaka jambo lao na wenzao wa Bara kuona walitakalo wenzao si jambo jema. Hapo ndio utawasikia watu hawa wakisema: Tuachieni na Zanzibar yetu na nyie mkae na Tanganyika yenu. Huu ndio ukweli na inafahamika.
Hawa ni watu hatari kwa Muungano ambao umewaleta pamoja watu wa Bara na Visiwani licha ya kuwepo matatizo.
Wapi Muungano umetokea inaeleweka, ijapokuwa hakuna ajuaye hiyo nakala ya mkataba asilia wa Muuungano ipo wapi na unasema nini ili utumike kama hadidu rejea tunapozungumzia kero za Muungano.
Hata hivyo, safari ya Muungano ya siku zijazo ni tabu kutabiri kama ulivyo upepo wa Bahari ya Hindi. Vile vile haieleweki kama nahodha wa hiki chombo kilichokuwepo safarini yupo mbele kama ilivyo safari ya meli au yupo nyuma kama ilivyo safari ya ngalawa.
Abiria wanajua wapo kwenye chombo na wapo safarini, lakini wapi wanakwenda hawafahamu!
Ni vizuri matatizo yaliyopo yakapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuimarisha Muungano. Watanzania wamechoshwa na nyimbo ya tupo mbioni kushughulikia kero za Muungano. Ni vizuri hizo mbio sasa zikafika mfundoni au angalau watu wakaelezwa zilianzia wapi, ni za masafa gani, zipo wapi na mwisho wake upo wapi.
Tuadhimishe Muungano kwa kufurahia mafanikio yetu kama taifa la watu wanaoelewana, lakini tusipuuze matatizo tuliokuwa nayo.