Nitoe wazo jingine:
Kuna ubaya gani wa kuwa na Serikali moja kuu (Rais, Makamu, na Waziri Mkuu na Baraza moja la Mawaziri) halafu mnakuwa na Mabaraza ya Wawakilishi katika pande zote za muungano na kuwa na Gavana wa pande zote mbili ambaye anasimamia Maeneo huru (Bara na Zanzibar)? Hivyo kimsingi unabakia kuwa na serikali mbili (Provincial na Union) Na mahusiano na ni kati ya serikali ya province na ile ya muungano. Na kuna mahusiano yanayohusu interstate. Kimsingi ni kama mfumo wa Marekani ambapo haziko serikali 50 (in fact they are) lakini kimahusiano ni serikali mbili FEderal na State (regardless of the number of states).
Mfumo wa namna hii utakuwa mzuri sana hasa kama tutaamua kuungana na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Mzee Mwanakijiji, heshima yako!
Unasema kama tutaamua kuungana na Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi? haya ni mawazo ya raia kama mimi na wewe, ambao tuna nia ya kushirikiana na ndugu zetu, na hatuoni matatizo yoyote ya kutawaliwa na Rais mmoja. Ebu fikiria mkutano wa kufikirika kati ya Museveni, Kikwete, na Kibaki. Ikiwekwa mezani kuwa hizi nchi ziungane, wazo kubwa vichwani mwa hao watu watatu ni nani awe Rais miongoni mwao. Hoja itakufa pale pale.
Museveni ameingia madarakani kwa mtutu wa bunduki, na inavyoonekana ndivyo atakavyotoka. Anajiona yeye peke yake ndiye bora kuwa Rais kuzidi mtu mwingine yeyote. Ameshawishi uvunjaji wa katiba ili aendelee kutawala. Anaweza kumwambia Kikwete na Kibaki kuwa tuungane na Rais awe Kibaki au Kikwete? atataka awe yeye au hakuna Muungano, au Muungano uwepo na yeye aendelee kuwa Rais wa Uganda.
Vivyo hivyo kwa Kibaki. Ameshindwa uchaguzi lakini amejiapisha na kutwaa tena madarakani juu ya damu za raia anaotaka kuwalinda. Kikwete amejiandaa miaka kumi kuchukua madaraka na ameingia kwa kuteketeza mamilioni ya fedha za wananchi kwa mgongo wa kuwaletea maisha bora. Nani kati ya hawa viongozi watatu atamfuata mwenzake na kutaka nchi zao ziungane, huku akitambua kwamba katika Muungano anaweza kupoteza madaraka yake? Matokeo yake, tunaambulia miundo ya miungano inayolinda madaraka ya viongozi, badala ya kulinda maslahi ya wananchi.
Lakini angalia, Wakenya wanafanya biashara Tanzania, na Watanzania wako Kenya wanafanya biashara. Mabasi ya kutoka Dar kwenda Mwanza na Bukoba yanapitia Kenya na Uganda. Watanzania, Wakenya, na Waganda walioko nchi za nje, hawakuwa na matatizo yasiyokuwa na vichwa wala miguu. Mwaka juzi tu Kikwete alikutana na Bush kuteta, na katika hali ambayo haieleweki, Wakenya wakadai Kikwete alimwongelea vibaya Kibaki. Sasa angalia Wakenya wanavyotukanana na Watanzania kwenye mitandao.
Mgogoro wa Burundi ni wa Watusi na Wahutu. Mgogoro wa Rwanda ni wa Wahutu na Watusi. Ilifikia mahala yakawepo mapendekezo kwamba, ili kutatua migogoro ya aina hii, inabidi Watusi wote wapelekwe Rwanda na Wahutu wote wapelekwe Burundi ili kila kabila lijitawale, liwe na Rais wake, kwa sababu inajulikana kuwa tatizo ni madaraka (mlo). Ilifikia mahala kuwa hata nchi kama Somali ambayo haina kabila, ila kuna koo, au Ethiopia, zitengwe katika vibaba ili kila kibaba kiwe na Rais wake.
Angalia Urusi ilivyosambalatika. Msambalatiko unaendelea na itafikia mahala hata zile zilizodhaniwa kuwa ni nchi, zitagawanyika katika vibaba au koo, na kila ukoo utataka kuwa na bendera, wimbo wake wa taifa, na Rais wake. Sababu ya yote haya ni madaraka, na raia baki wanachochewa na kuingizwa katika mkumbo. Kwa nini tuige mifano ya nchi au makundi ya watu wanaojigawa? Vilevile sioni sababu yakuiga mifano au makundi ya watu wanaoungana. Kwa nini tusiangalie asili yetu nini?
Hizi hoja za kumezwa na kupoteza utaifa sijuhi mantiki yake nini hasa. Yaani leo inaaminishwa kuwa Mmasai wa Tanzania akiungana na Mmasai wa Kenya, wote wawili watapoteza utaifa wao? Ebu nipe historia ya utaifa wa Mmasai? Ukweli ni kuwa, hili kabila moja la kimasai, lenye mataifa mawili ya Tanzania na Kenya, likirudi katika hali yake ya asili, halipotezi utaifa wake, kinachopotea ni madaraka ya watawala wa Tanzania na Kenya. Hilo ndilo tatizo letu wakati wa kutafuta muundo wa Muungano ambao ni muafaka. Hili sio tatizo la Afrika tu, bali dunia nzima.
Hivi kabla ya ukoloni, watu wa Afrika walikuwa wamemezwa na nani? huu woga wa kumezwa unatoka wapi? Serikali ya Tanganyika iko wapi? Nitajie makamu wake au Rais wake. Kwa hiyo inakubalika kwa Serikali ya nchi kubwa kama Tanganyika "the majority" kumezwa ndani ya Serikali ya Muungano wa Tanzania, lakini haikubaliki kwa nchi ndogo kama Zanzibar "the minority" kumezwa ndani ya Serikali ya Muungano.
Umetoa mfano wa Marekani, lakini hata Rais wa Texas, Samwel Houston, alikuwa na mawazo kama haya haya, kuwa eti Texas ni nchi ndogo ingemezwa na Marekani. Lakini kilichojulikana, na ambacho kinajulikana mpaka leo, ni kuwa Rais Houston, na kama walivyo wanasiasa wengine, aliweka mbele hatima ya madaraka yake, kuliko hatima ya jinsi raia wa Texas ambavyo wangenufaika na Muungano. Hivyo, maamuzi ya hatima ya muungano wao hayakuachwa mikononi mwa Rais Houston.
Toka nchi ya Texas "the minority" na nchi ya Marekani "the majority" ziungane, ilichukuwa muda mrefu kabla hata ya kutoa Rais wa Marekani. Raia wa Texas hawakupoteza utamaduni wao, asili yao, na kadhalika. Sasa hivi wanafaidi matunda ya Muungano. Kuwapa watu madaraka sio lazima kuwa na Serikali za majimbo.
Ni kitu gani ambacho Rais wa Zanzibar anashindwa kukifanya ila kinaweza kufanywa na Waziri Mkuu wa Zanzibar? Alafu hii hoja ya kuwa wakati Muungano unaundwa, lengo lilikuwa kuwa na Serikali tatu, Aboud Jumbe amelitoa wapi? Mbona katika ukurasa 4 wa Kitabu cha Uongozi wetu na hatima ya Tanzania, imeandikwa kwamba waasisi hawakutarajia kuwa na Serikali tatu au moja? Jumbe na Nyerere nani mkweli?