LHRC: Bado Dar es Salaam inaongoza kwa ukatili wa Kijinsia

LHRC: Bado Dar es Salaam inaongoza kwa ukatili wa Kijinsia

Nyendo

JF-Expert Member
Joined
Jun 4, 2017
Posts
1,455
Reaction score
5,134
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema mkoa wa Dar es Salaam bado unaongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni msongamano wa watu na muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, wakati wa warsha ya kutathimini ukatili wa kijinsia kwa wanawake katika sekta ya afya iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, ikiwa ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumzia hali ya ukatili nchini, Henga amebainisha kuwa takwimu bado ni za juu akisema, "hali ya ukatili wa kijinsia ni kwamba wanawake 7 kati ya 10 wanapata ukatili. Ukichukua manusura 10, saba ni wanawake. Ukatili unafanyika sana kwa wanawake wa miaka 15 hadi 49, na unahusisha vipigo, ukatili kutoka kwa wenza (intimate partner violence), mauaji ya wenza, na ukatili wa kiuchumi ambao umekua kwa kasi kutokana na kipato duni cha wanawake”.

Kuhusu kwanini Dar es Salaam inaongoza, Mkurugenzi huyo amefafanua kupitia ripoti yao ya hivi karibuni akisema, "Kwa ripoti ya mwaka 2024 ya Haki za Binadamu, inaonyesha kwamba Dar es Salaam bado inaongoza kwa ukatili wa kijinsia. Inapofanya hivyo ni kwa sababu ya watu ni wengi, idadi ya watu ni kubwa, na shughuli mbalimbali za uchumi ni nyingi.

Kuna mikoa kama Tabora na Mara inayofuata, lakini Dar es Salaam ndiyo inayongoza."LHRC imesisitiza umuhimu wa vituo vya huduma ya pamoja (One Stop Centers) kama kile cha Mwananyamala katika kulinda ushahidi na kumpatia mhanga haki kwa haraka."Zamani ilikuwa lazima uende polisi upate PF3 ndipo uje hospitali, mzunguko huo ulikuwa unapoteza ushahidi.

Sasa hapa ni moja kwa moja, mtu anapata haki yake na aliyefanya ukatili anafikishwa mahakamani. Lakini hali ya vituo hivi 18 Tanzania nzima imeshuka uwezo kwa sababu ya uhamisho wa watumishi, ndiyo maana leo tunatoa mafunzo upya kwa watenda kazi wa hospitali ili waweze kupata maarifa hayo," ameongeza Henga


 
Back
Top Bottom