LHRC: Tuna taarifa Masheikh 51 bado wanashikiliwa katika magereza kwa miaka 10 sasa bila kufikishwa mahakamani

LHRC: Tuna taarifa Masheikh 51 bado wanashikiliwa katika magereza kwa miaka 10 sasa bila kufikishwa mahakamani

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2022
Posts
2,780
Reaction score
6,607
Taarifa kwa Umma _kukamatwa kwa Masheikh_page-0001.jpg

Taarifa kwa Umma _kukamatwa kwa Masheikh_page-0002.jpg

KUKAMATWA TENA KWA MASHEIKH 12 BAADA YA KUACHIWA HURU

Machi, 10 2025, Dar es Salaam
Mnamo tarehe 4 Machi 2025, LHRC ilipata taarifa kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachilia huru masheikh 12 waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi. Masheikh hao waliachiwa huru baada ya Jamhuri kutoa taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo hata hivyo walikamatwa tena na kufunguliwa kesi ile ile.

Itakumbukwa kwamba tarehe 10 Machi 2023 LHRC ilitoa taarifa kwa umma juu ya masheikh zaidi ya 40 kushikiliwa katika magereza mbalimbali kwa zaidi ya miaka 10 ikiwemo familia ya Sheikh Said Mohamed Ulatule, katika taarifa yake kwa umma LHRC ilimtaka mwendesha mashitaka wa Serikali kuwaachia huru masheikh hao kwani kukaa nao muda mrefu bila shauri kuendelea ni wazi hakuna ushahidi wa kutosha kwa mashauri haya kuendelea.

LHRC inazo taarifa kuwa kuna masheikh takribani 51 bado wamekuwa wanashikiliwa katika magereza mbalimbali hapa nchini kwa takribani miaka 10 sasa bila kufikishwa mahakamani kinyume cha ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

Kitendo cha Jamhuri kukaa na watuhumiwa kwa miaka 10 gerezani kinaashiria dhahiri kwamba Jamhuri haina ushahidi wa kutosha unaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Kupambana na Ugaidi Tanzania Sura ya 19 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2022, adhabu ya chini ya kosa la ugaidi kama ikithibitika kwa mhusika ni kifungo cha miaka 30 jela, maana yake ni kwamba kama watuhumiwa watakuwa na hatia maana yake tayari wameshatumikia moja ya tatu ya adhabu kwa mujibu wa sheria.

LHRC inatoa wito kwa Jamhuri kama kuna ushahidi wa kutosha basi kesi zote za ugaidi zinazowakabili masheikh kote nchini ziendeshwe kwa haraka ili haki iweze kupatikana kwa wahusika na kama hakuna ushahidi wa kutosha basi Jamhuri iwaachilie huru wahusika ili waweze kuungana na familia zao.

LHRC pia inatoa rai kwa mwendesha mashitaka wa Serikali (DPP) kutekeleza mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na taratibu nyingine za nchi na kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa kila anayekabiliwa na mashitaka ikiwemo kuzingatia masharti ya kifungu cha 91(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura Na. 20 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2022, pamoja na mambo mengine kifungu hicho kinaweka takwa kwa mwendesha mashitaka ya umma kutotumia mamlaka aliyo nayo kwa mujibu wa kifungu cha 91 kama hana ushahidi, kwa lugha nyingine mtuhumiwa anapashwa kufikishwa mahakamani na shauri lake kuanza kusikilizwa mara baada ya kukamatwa tena kwa tuhuma za kosa lilelile.

Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyopotea.

Imetolewa na:
Bw. Fulgence Massawe (Wakili) Kaimu Mkurugenzi Mtendaji-LHRC

Pia soma
- Masheikh 12, waliokaa gerezani miaka 10, kwa tuhuma za Ugaidi waachiwa huru

- Masheikh 12 waliochiwa na mahakama kutokana na tuhuma za ugaidi Machi 4 wakamatwa tena na kurudishwa gerezani!
 
Back
Top Bottom