Tundu Lissu ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, Pamoja na viongozi wengine wa chama hicho mnamo Machi 23, 2025 walifanya
mkutano wa hadhara jijini Mbeya, huku ajenda kuu ya mkutano huo ikiwa ni uzinduzi wa Kampeni ya 'No Reforms No Election'
Kumekuwapo na
chapisho lenye utambulisho wa Jambo TV likiwa na kichwa cha habari 'Lissu atangaza changamoto za kiuchumi CHADEMA, akiri kususia kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025' ambapo kauli hiyo inadaiwa kutolewa na kiongozi huyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Mbeya.
Je, ni upi uhalisia wa Chapisho hilo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck ukihusisha utafutaji wa kimtandao kwa kutumia maneno muhimu (Key word search) umebaini kuwa chapisho hilo si la kweli na halijachapishwa na
Jambo TV kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
Aidha Lissu kupitia
mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Mbeya hakutoa kauli yoyote iliyohusu hali ya kiuchumi ndani ya CHADEMA bali alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi jijini humo uhitaji wa mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu 2025 ili kuchochea uhuru na uwazi.
Akirejelea mapendekezo ya aliyekuwa Jaji Mkuu
Francis Nyalali pamoja na Tume ya Jaji Sinde Warioba, Lissu alieleza uwepo wa mambo muhimu yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuchochea uchaguzi huru na haki. Tazama hapa
1:32:46
"Badilisha tume ya uchaguzi, ondoa watumishi wa serikali wanaosimamia uchaguzi, weka watu huru, hakikisha hakuna kura feki, tengeneza utaratibu wa kampeni wa haki, na uhakikishe kila wakala anaapishwa na anaingia kwenye kituo cha uchaguzi,"
"Jukumu letu la kwanza ni kukwamisha huu uchaguzi. Hakuna mtu anayewalazimisha kwenda kupiga kura kwa bunduki. Wananchi tukiamua tunaweza kuzuia uchaguzi huu na kuleta mabadiliko tunayoyataka,"