Lissu: Mbowe ameshapoteza Public opinion

Lissu: Mbowe ameshapoteza Public opinion

Na Shabani Lissu

Jaribio la panya la kumchagua mmoja wao kwenda kumfunga paka kengele si jaribio la lelemama linamhitaji panya shujaa wa kufanya hivyo, vivyo hivyo jaribio la kukabiliana na Mwenyekiti Mbowe kwenye uenyekiti wa chama si jaribio rahisi, ni la kishujaa nitaeleza.

Chama cha Chadema kilikuwa cha pili kusajiliwa baada ya ujio wa vyama vingi mwaka 1992, mmoja wa waanzilishi wake Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei alikiongoza chama hicho hadi mwaka 1998 na kung'atuka, akamuachia Marehemu Mzee Bob Nyanga Makani ambaye naye alistaafu mwaka 2003. Alipochaguliwa Mbowe mwaka 2003 msamiati wa kung'atuka au kustaafu ukatoweka. Yeyote mwenye ubavu na ushawishi aliyejaribu au kutamani kushindana na Mbowe alipata misukosuko ndani ya chama. Hii imejenga dhana kuwa chama hiki ni cha kifamilia au cha kikanda chenye malengo yasiyo dhahiri kwa sababu uongozi wake kwa maana ya uenyekiti haujawahi kwenda nje ya familia kwa maana wenyeviti wastaafu na wa sasa wanaunasaba.

Dhana hii ya chadema kunasibishwa na ukanda na undugu inasababishwa na Mbowe mwenyewe na haikisaidii chama. Miaka 20 madarakani ni mingi na ingeweza kuzalisha wenyeviti wengine wasionasibishwa na undugu wala ukanda.

Uimara na udhaifu wa Mbowe umejengwa katika dhana ya uhafidhina (Conservativism) yeye mwenyewe kwa kukaa zaidi kitini anaamini na kuaminishwa na wahafidhina ( wasiopenda mabadiliko) kuwa bila yeye chama kitakufa au kudhoofika. Wakati anatangaza nia ya kugombea alidai kuwa kwa vile chama kipo katika mnyukano wa makundi isingekuwa busara yeye kukaa pembeni, alichosahau ni kuwa mnyukano ule angeumaliza kwa urahisi kama angeamua kutokugombea. Wahafidhana wana tabia ya kuamini kuwa wao ndio suluhisho la kila kitu, wahafidhina huzungukwa na wanufaika ambao bila mhafidhina kiongozi matumbo yao yatakuwa mashakani. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kila alipotaka kung'atuka wahafidhina walimwambia kuwa nchi bado changa inamhitaji mpaka alipogundua kuwa kumbe uchanga waliousema ni matumbo yao na familia zao kwa vile huenda mabadiliko yangeweza kuwaweka pembeni. Mbowe alidai kuwa ana 'vimemo' vingi vya kuombwa endapo atachaguliwa tena awakumbuke kwenye ukatibu, hao ndio wahafidhina. Kwa bahati mbaya Mbowe amezungukwa na watu kama Benson Kigaila anayeweza kutamka kuwa haamini katika ukomo wa uongozi na anadai katiba mpya, akiingia madarakani atatoka kweli kwa amani? Kigaila ambaye chama chake kilikuwa kinashinda mahakamani kuwashitaki wabunge 19 huku mmoja wa wabunge hao ni mke wake!! Watu wa aina hii hawawezi kumsaidia Mbowe.

Chadema bila Mbowe itakufa?

Sidhani, hii ni kete anayoitumia Mbowe kubaki madarakani sambamba na wahafidhina wenzake. Utajiri wa Mbowe unatumiwa kama fimbo na hii yeye anaweza kuendelea kuifanya chadema imtegemee ili wamtegemee.

Vyama vinakufa au kuyumba kwa minyukano ya vyeo inayosababishwa na ung'ang'anizi wa madaraka na tofauti ya mitazamo ya mafahali wawili katika chama. Mifano ni mingi nitaeleza.

1. Alhaji Zubeir Mwinshehe Manga Mtemvu Vs Mwl Nyerere. baada ya mkutano wa Tabora Jan 21-26 1958 kujadili kura tatu na masharti mengine ya upigaji kura akiwa Katibu Mwenezi wa TANU, Mtemvu hakuamini katika masharti hayo hivyo baada ya kupishana mawazo na Mwl Nyerere alijiondoa na kuanzisha chama chake kiitwacho ANC. Kitendo hiki kiligawa mtazamo na nguvu za Waafrika bila sababu.

2. Rais Jomo Kenyata Vs Jaramogi Oginga. Wakiwa na sifa zote za kuwa marais, Kenyata alimteua fahali mwenzake Jaramogi kuwa makamu wake. Baada ya msuguano mrefu hatimaye Jaramogi aliondoka KANU na kuanzisha chama chake(KPU) wabunge ishirini na saba wa kitaifa na waziri Ochieng Onego walijiuzulu na kumfuata Jaramogi na kuteteresha serikali ya Jomo.

3. Raila Odinga Vs Kijana Michael Wamalwa. Baada ya Jaramogi kufariki Raila kwanza alijaribu kugombea umakamu mwenyekiti wa chama cha babaye Ford Kenya na kushindwa na James Orengo. Mwaka 1996 aligombea Uenyekiti wa chama kushindana na Kijana Wamalwa. Hakukubali matokeo hivyo aliondoka na kuanzisha chama cha NDP, kabla ya uchaguzi mkuu wa 1997 wabunge wote wa Luo Nyasa kupitia Ford Kenya walijiuzulu na kuhamia NDP.Ford Kenya ikafa.

4. Arap Moi Vs Raila Odinga. Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 Kenya, Moi alishauri na kuwaomba wanasiasa waandamizi Kenya kuungana na KANU, wakitambua kuwa Moi aliahidi kustaafu hivyo waliona fursa mbeleni. Walihamia KANU na kushauri iitwe NEW KANU huku Raila akiwa Katibu Mkuu wake. Pamoja na kukubaliana kuwa mpeperusha bendera kupitia chama atapatikana kwa kupigiwa kura lakini MOI muda ulipowadia alimteua Uhuru Kenyatta bila utaratibu na kusisitiza kuwa ndiye mgombea urais. Chama kikisheni wanasiasa wote waandamizi Kenya na saba miongoni mwao walijiandaa kugombea katika mchujo. Raila na wenzake walianzisha Rainbow Coalition baadaye wakauita umoja wao NARC na kumsimamisha Mwai Kibaki ambaye alishinda na kuiua KANU rasmi.

5. Augustino Mrema Vs Mabere Marando et all.Mrema alijiondoa CCM Machi 4, 1995 na kujiunga na NCCR Mageuzi Machi 15,1995, Mabere Marando akampisha uenyekiti na yeye kuwa Katibu Mkuu. Mrema alishinda uchaguzi mdogo Temeke baada ya mahakama kumuengua Kihiyo wa CCM. Mwaka huo mwishoni kukaibuka pande mbili ndani ya chama yaani Mrema na Marando. Walijaribu kuitisha mkutano mwaka 1997 mkoani Tanga. Kwa bahati mbaya kila fahali akawa na wajumbe wake. Marando aliungwa mkono na wajumbe wa Kamati Kuu na aliitisha kikao Splendid hotel wakati huo huo Mrema alikuwa Fourways hotel kukutana na Wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC). Mrema aliambiwa mkutano unaotakiwa kuanza ni wa Kamati Kuu lakini alikataa. Mkutano wa Mrema ulivamiwa na akina Marando na kuharibika.Wote baadaye walikutana Raskazone hotel kujaribu kumaliza tofauti lakini hawakuelewana na matokeo yake kila mtu alitolewa nje na mlinzi wake huku taa zikiwa zimezimwa. Kila mmoja alirudi Dar na kufikia ofisi tofauti. Mrema Manzese na Marando mtaa wa Lugoda. Huu ulikuwa mwisho wa NCCR Mageuzi na Mrema alitimkia TLP.

6. Prof Lipumba Vs Maalim Seif. Katika uchaguzi wa 2015 vyama vilivyokutanishwa kwa muamvuli wa Umoja wa Kudai Katiba Mpya ( UKAWA) walikubaliana kusimamisha mgombea mmoja huku Lipumba akivizia nafasi hiyo. Ghafla Edward Lowasa alijiunga na Chadema na kuwa mgombea wa urais kupitia UKAWA na Babu Haji Duni kutoka CUF akawa mgombea mwenza. Lipumba kwa hasira akajiuzulu uenyekiti wa CUF na kujitenga na uchaguzi wa 2015. Mwaka mmoja baadaye 2016 akatangaza kurudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti akitegemea kugombea uenyekiti tena. Maalim Seif na wenzake walifungua kesi lakini Lipumba alishinda kesi. Maalim Seif akahama chama na wafuasi wake na kuelekea ACT Wazalendo na huo ndio ulikuwa mwisho wa CUF inayoeleweka kwa umma.

Mifano ya vyama kupoteza muelekeo kwa sababu za minyukano ya viongozi waandamizi ni mingi, Je, Chadema hawajifunzi kutokana na mifano hiyo. Inawezekana wanajua ila hulka za viongozi wanaotakiwa wakiokoe chama ndio tatizo.Mbowe na Lissu ni watu tofauti kimtazamo na kimkakati. Nitaeleza.

Mwenyekiti Mbowe uimara wake upo kwenye kuamini katika mazungumzo huku akitumia mabavu ya wastani.Miaka 20 ya kuamini anachokiamini angekuwa amefika mbali na hapa ndipo wenzake wanapokuwa na mtazamo tofauti.Kwa bahati mbaya ameingia kwenye mtego wa hulka ya kibinadamu ( utamu na ulevi wa madaraka). Miaka 20 madarakani ni mingi hasa kama wanaokuzunguka ni machawa wako. Machawa wana tabia mmoja tu, kukusifia na kuwashughulikia watu wema kwako. Katika chama kichanga ambacho uimara na taswira yake bado inajengwa na 'personalities' mnapokuwa na mafahali wawili suluhisho siyo kuwakutanisha kwenye uchaguzi, chama kitaumia tu.Jambo la kufanya ilikuwa ni maridhiano ya kiuongozi.Mmoja asubiri mwingine aendelee au wote wapumzike aje mtu wa kuwaunganisha wote wawili. Hivi kulikuwa na sababu gani kuwakutanisha Sugu na Msigwa kanda ya Nyasa ilihali wote ni taswira ya chama? Labda kama mwenyekiti alikuwa anajua hiki kilichotokea.

Kwa maoni yangu Mbowe ameshapoteza 'Public Opinion' hili limeshamtokea Prof Lipumba. Umma haumtambui tena kama mwanamageuzi. Kwa bahati mbaya Mbowe halitambui hili. Wanamapinduzi wana tabia ya kuumizana wenyewe kwa wenyewe hasa wakiwa wanaelekea kwenye anguko. Oliver Tambo mwaka 1977 katika kambi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini nchini Angola aliwakumbusha wenzake kuwa kupigania uhuru siyo kazi kubwa sana bali kazi ipo kwenye kuutunza uhuru au mapinduzi hayo.( it’s not difficult to wage a liberation struggle than keeping it). Mbowe anaweza kujikuta hakufanya lolote miaka yote ya kupigania mageuzi nchini.

Kwa upande wa Lissu uimara wake upo kwenye unyoofu wake. Si mtu wa kupenda sana mazungumzo kwenye jambo la haki, hudai kupewa sio kuomba. Mazungumzo ya kisiasa huzaa rushwa ya kiuongozi/ nusu mkate au pesa benki.Lissu haamini kwenye hilo. Kwa tabia hii ni kipenzi cha wanachama wengi wa kawaida ndani ya chama chake na nje. Kwenye siasa wakweli ni wachache na wana maadui wengi viongozi ndani ya vyama vyao na marafiki zao ni wanachama wa kawaida. Ukweli wake unatafsiri ya mapungufu ya kiuongozi kwa viongozi wenzake. Hawafichii siri za uovu wao. Watu wa hulka ya Lissu wanaaminika kutotumia busara, si watu wa 'kucompromise' hivyo huogopwa.

Nini Kitatokea January 2025?

Tofauti ya kimtazamo kati ya Lissu na Mbowe imeanza kuonekana zamani kidogo, alipoingia Rais Mama Samia madarakani. Mara kadhaa Lissu amelalamikia maridhiano na ameshawahi kumtuhumu Mbowe kuhongwa V8 mbili na serikali, aliendelea kutuhumu kuwa maridhiano yalifikia hatua ambayo kati yao kuambiwa watapewa vyeo uchaguzi ujao ( nusu mkate), akawatuhumu pia wenzake kuhongwa na Abdul, akatuhumu pesa chafu nyingi kwenye chaguzi za chama akihoji ni kwa faida ya nani? Akalalamika pia kukatazwa kufanya mkutano Iringa na chama chake na alipolazimisha kufanya aliambiwa asizungumzie baadhi ya tuhuma. Kwa mwenye akili timamu alijua kuna shida.Kugombea kwake uenyekiti ni kujaribu kutibu kansa kwenye 'stage' ya mwisho. Kwa hulka yake ni lazima uchaguzi uwe huru na wa haki kumbakisha Chadema. Simuoni ndani ya CCM kwa sababu Lissu ni mpambanaji kwa hulka. Che Guevara baada ya mapinduzi ya Cuba alikuwa waziri wa fedha na Gavana wa benki kuu Cuba lakini aliviacha vyote hivyo na kuchukua silaha akidai kupambana na udhalimu wa kidunia ni wito wake na alikufa kimapinduzi huko Bolivia. Labda ataungana na Zitto ACT Wazalendo. Akibaki ndani ya Chadema hatapata ushirikiano wa maana kwa viongozi wa juu ambao bila shaka safu haitabadilika sana hivyo akubali kuwa mwanachama mfu.

Mwenyekiti Mbowe atashinda uchaguzi huu, uchaguzi si tukio la muda mfupi, ni mchakato wa muda mrefu. Kwa kiongozi aliyekaa miaka 20 madarakani asilimia 80 ya wanaoingia madarakani kwa nafasi ya maamuzi kama mkutano mkuu ni watu wake. Akishinda ana kazi ya kubadilisha maoni ya umma juu yake. Kama Lissu atabaki najua atajaribu 'kubalance' uongozi kwa kupendekeza viongozi wanaomuunga mkono Lissu katika nafasi za juu, atapata kikwazo kwa wahafidhina wanaotamani kusiwe na masalia ya Lissu Chadema, akifanya hivyo na Lissu akibaki Chadema uwezekano wa makundi kuwepo baadaye ni mkubwa. Ana jambo la kufanya kama kiongozi.

Historia ni mwalimu mzuri, tusubiri wakati utaamua.

Shabani Lissu
0717042451

View attachment 3188568
Ni balaa
 
Back
Top Bottom