MAAMUZI MAGUMU!
HATMA YA UBINGWA WA LIVERPOOL KUPITIA MBINU HIZI.
LICHA ya kusimamisha Ligi Kuu England kwa wiki tatu hadi Aprili 3 mwaka huu, vichwa vinawauma mabosi wa bodi ya EPL, kutokana na kutakiwa kuja na majibu ya nini kitafanyika iwapo virusi vya Corona vitaendelea kuitesa nchi hiyo.
Hadi sasa hakuna jibu la moja kwa moja linalotolewa na mabosi hao ambao wanatarajiwa kufanya kikao cha dharura wiki hii, kuhusiana na nini kitafanyika ikiwa tatizo la Corona litadumu kwa muda mrefu maana Ligi Kuu England haina kanuni inayoeleza hatua gani zitachukuliwa iwapo ligi itavunjika.
Lakini, wachambuzi wa soka la England wamekuja na aina nne za uamuzi mgumu ambazo vigogo hao wanaweza kuchagua moja.
UAMUZI WA KWANZA:
Kuvunja Ligi
Huu ni uamuzi unaowakera zaidi mashabiki wa Liverpool waliokuwa wanaamini huu ni mwaka wao na baada ya mechi 29 msimu huu wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 25 mbele ya Manchester City inayoshika nafasi ya pili na wanahitaji mechi mbili tu kutwaa ubingwa wao wa kwanza baada ya miaka 30.
Lakini, kwa mujibu wa uamuzi huu uliowekwa mezani na Makamu Mwenyekiti wa West Ham, Karren Brady, kwa upande wake anashauri ligi ivunjwe na kila kitu kianze upya kuwe hakuna bingwa wala timu ya kushuka daraja, hii ni nzuri kwa timu yake inayoshika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 27 na wastani mzuri wa mabao kulinganisha na timu zilizo chini ya mstari wa kushuka daraja.
Uamuzi huu unaiathiri zaidi Liverpool inayokaribia kutwaa taji la Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30, lakini pia uamuzi huu utaiathiri Leicester City ambayo ipo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
UAMUZI WA PILI:
Kumalizia MECHI
Huu ndiyo uamuzi ambao mabosi wa EPL, wanaona hauna utata kila timu na itapata inachostahili, kupitia uamuzi huu wanataka kusubiri na kumaliza ligi kivyovyote na hata kama tatizo la virusi vya Corona litachukua muda mrefu kiasi gani, lakini vikiisha tu ligi imaliziwe ndipo msimu mpya uanze.
Lakini, ili hili litokee lazima michuano ya Euro 2020 isifanyike ili kutoa nafasi kwa klabu kucheza mechi za ligi wakati wa kiangazi, maana kama michuano hiyo ikiwapo wachezaji watajiunga na timu zao za taifa na hawatapata nafasi ya kucheza soka katika ngazi ya klabu.
UAMUZI WA TATU:
Ligi kuisha hapa
Kama tatizo la Corona lisipomalizwa mapema basi mashabiki wengi wa Liverpool wanataka uamuzi huu ambao ni kumaliza ligi katika hatua hii na kuwapa ubingwa huku. Norwich City, Aston Villa and Bournemouth zikishushwa daraja.
Uamuzi huu unainufaisha zaidi Liverpool ambayo itapata ubingwa ambao inastahili, lakini unaziumiza timu nyingi, kuanzia zile zitakazoshushwa daraja wakati zikiwa na nafasi bado ya kupamba na kubaki Ligi Kuu hasa kutoka na ukweli kuwa tofauti kati ya timu ya 18 na ya 17 na 16 ni mabao tu.
Lakini pia timu ambazo zinapambana kutafuta nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester United, Wolves na Sheffield United zitaathiriwa na uamuzi huu kwa sababu bado zina nafasi ya kuingia nne bora kama ligi ikiendelea, lakini ikimalizwa hapa basi hawatashiriki michuano hiyo mwakani.
UAMUZI WA NNE:
Kuongeza idadi ya timu
Ili kuepusha kelele ya timu zitakazoshuka daraja na pia kuiwezesha Liverpool kutwaa ubingwa ambao imeupigania sana msimu huu, basi Bodi ya Ligi inaweza kuamua hakuna kushusha timu daraja na kuipa ubingwa Liverpool.
Na ili kuzipa haki zile timu ambazo zimekuwa na msimu bora Ligi Daraja la Kwanza, timu za Leeds na West Brom zipewe nafasi ya kupanda daraja, hii itamaanisha kuwa msimu ujao utakuwa na timu 22 badala ya 20, huku kila timu ikifurahi, japokuwa zile za timu zinazowania nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa zitalia lia tu.
Ndugu mwanamichezo nini maoni yako?
Sent using Jamii Forums mobile app
Sent using
Jamii Forums mobile app