Ni sawa kabisa suala ulilolileta hapa. Pamoja na kuwa serikali mara kadhaa imekuwa ikipanga sera ya lugha, lakini tumekuwa hatufiki popote kutokana na ufinyu wa fikira wa viongozi wetu.
Mimi sina ugomvi na lugha gani itumike, lakini serikali ingepaswa kuwa na sera madhubuti ya lugha, ingawaje kwa mtazamo wangu lugha yetu ya Kiswahili inapaswa kutumika kuanzia msingi hadi chuo. Wnaharakati wa lugha yetu tayari wameshafanya tafiti nyingi zinazoonesha kuwa hili linawezekana. Lakini kwa tamaa za kusaidiwa vijisenti vichache vya kukuza Kiingereza, mpango wa kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia unakwamishwa.
Wakati umefika tuamuwe kutumia lugha moja ya kufundishia. Hii haina maana kuwa tukitumia moja tutakuwa hatutumii nyengine, lakini kwa mpango wa sasa tunawasumbua na kuwadumaza watoto wetu. Sera ya sasa ni kuwa tunaanza na Kiswahili wakiwa msingi, na tunafundisha kwa Kiingereza wanapoanza sekondari. Matokeo yake watoto wetu hawajuwi Kiswahili wala Kiingereza. Kwa nini isiwe moja tu?
Imani yangu ni kuwa ikiwa tunataka maendeleo ya kweli, wakati ni huu wa kukikuza Kiswahili chetu kiwe cha kufundishia viwango vyote. Tukumbuke kuwa hakuna nchi yoyote ulimwenguni inayoweza kuendelea ikiwa itadharau lugha yake kama inavyofanywa hapa kwetu. Mtoto hufikiri na kuwa mbunifu kwa kutumia lugha yake na sio kufikiria katika lugha yake na kujieleza katika lugha nyengine. Pia tusizionee haya lugha zetu nyengine. Ingelifikiriwa pia kuangalia uwezekano wa kufundisha lugha zetu za makabila, (angalau kwa matumizi ya ndani, kwani hizi ni lugha kamili) na lugha nyengine za kigeni ili kuwapa fursa na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa vijana wetu. INAWEZEKANA.