SoC02 Maandalizi yako, mafanikio yako

SoC02 Maandalizi yako, mafanikio yako

Stories of Change - 2022 Competition

DnS8elpmis

New Member
Joined
Jul 26, 2022
Posts
3
Reaction score
1
MAANDALIZI YAKO; MAFANIKIO YAKO

Maisha ni mnyororo wa matukio. La leo litazaa la kesho, na la kesho litazaa kesho kutwa yake, hadi mwisho. Japokua sisi tunapita tu, maandalizi yanaweza tupatia mafanikio na maisha ya milele katika kumbukumbu za vizazi na vizazi. Maandalizi ni mchakato wa kujiandaa na swala linalo tegemewa kutokea. Kwa mantiki hii maandalizi ni kama tahadhari pia; kufunga mlango usiku ni maandalizi ya kulala salama ama tahadhari dhidi ya hatari.

Mara nyingi zaidi maandalizi lazima yachukue muda mrefu kuliko tukio lenyewe. Yaani mapishi ya masaa kwa mlo wa dakika kadhaa, au masomo ya miezi kwa mitihani ya masaa. Kila mtu atakutana na changamoto za kuendana na uhalisia wake; yuko wapi? Anafanya nini, akiwa na nani? Na pia malengo yake na hali yake. Kilicho dhahiri hapa ni kwamba uhakika wa changamoto kujitokeza upo, na mbaya zaidi kuna uwezekano yakatokea matatizo ambayo awali yalijificha. Ila hata kwa kutambua zipo shida za namna hii na kutumia uangalifu, tayari umejiandaa zaidi kushinda. Adui mkuu wa maandalizi na tahadhari ni upuuzi.

Upuuzi ni ugonjwa nyemelezi, na ni chanzo kikuu cha kuanguka watu wengi. Wengi tunapenda kusubirisha mambo, makubwa na madogo, hadi dakika ya mwisho kabisa. Halafu bila sababu zenye mashiko. Haya bila shaka ni maandalizi ya kushindwa na tahadhari dhidi ya mafanikio. Haba na haba, hujaza kibaba. Anza na mambo madogo, rekebisha mazingira yako, weka vitu katika mpangilio. Jipe muda kutafakari kama maandalizi, yaani mwenendo wako, ni ya ushindi au la.

AINA ZA MAANDALIZI

Maandalizi binafsi

Maandalizi binafsi yanakuhusu wewe mwenyewe.

1)Maandalizi ya kisaikolojia. Hapa inahusu kuweka nia thabiti ya kufanikisha lengo lako. Kuamua kwamba changamoto unazozitegemea, na zitakazo jitokeza hazitakua kikwazo. Kujiandaa kupokea mafanikio pia ni muhimu. Yawezekana shughuli unayofanya ikafanikiwa pakubwa, kiasi kwamba mafanikio yakawa chanzo cha matatizo. Usipate ukabweteka, usitajirike ukalimbuka; yaani ukashindwa kujimudu na kujikuta unakurupuka.

2)Maandalizi ya nadharia na vitendo. Kutegemeana na lengo yawezekana ukahitaji ujuzi au utaalamu kulitimiza. Kwa mfano kuwa daktari au mhandisi yahitaji masomo maalumu, kama vile wana michezo pia wanahitaji mafunzo maalum kufikia ubora. Kwa sababu muamko mkubwa wa utafiti duniani, tasnia zote zinasogea mbele kwa kasi kubwa. Hali hii inalazimu mtaalamu anae endelea kukuza ujuzi wake ili kiwango chake kisishuke.

3)Maandalizi ya muda. Katika kila kitu unacho miliki, muda wako ndio kitu chenye thamani zaidi. Muda ukipotea huwezi kuurejesha. Unapoandaa mambo mbali mbali katika mipango yako kuwa makini ni wapi unachagua kuwekeza muda wako. Maana pale unapowekeza muda mwingi ndio utegemee mavuno mengi. Kuna umuhimu mkubwa wa kulibeba hili kuwa swala nyeti kwa sababu tu ni kitu chepesi kupuuzia. Mazoea hujenga tabia, na muda ndio msingi wa ujenzi huo. Ukiwa makini na muda wako tangu mwanzo, utaikwepa kazi ngumu ya kujivua tabia zinazokurudisha nyuma.

b) Maandalizi ya mazingira

Mazingira yanaweza gawanyika mara tatu

Mazingira kwanza kabisa ni eneo husika la shughuli. Ili kuongeza uwezekano wa kufanikiwa katika lengo ni muhimu kuhakikisha mazingira ni rafiki kadri iwezekanavyo kwa shughuli za kutimiza lengo. Kiujumla mazingira yaliyo katika mpangilio hurahisisha kazi. Hata anayetaka kufanya vurugu hujipanga kuhakikisha anatimiza malengo yake vilivyo.

Watu waliokuzunguka wana nafasi kubwa sana katika kiwango cha mafanikio yako. Tambua kabisa utekelezaji wa jambo katika kiwango cha juu cha ubora sio jambo rahisi. Ndio maana kiwango cha juu zaidi daima kinakuwa na thamani zaidi.

Jitahidi kuwatambua waliokuzunguka, na uhalisia wao katika mafanikio yako. Kwa mfano ni kweli rafiki zako kumi wote wana tija? Ama ni kweli inafaa kujitenga na jamii usisumbuane na watu? Kama mtu ni chanzo cha vurugu, au hisia asi ni muhimu kutathmini usahii wake katika maisha yako.

Muda mwingine kuna mambo unayafanya kwa msukumo wa watu fulani; kama ni mambo yanaendana na maelngo yako, ambatana nao. Kama yako kinyume na malengo yako, achana nao.

Hakuna jambo jipya chini ya jua. Katika maandalizi yako kuna uwezekano wapo waliowahi kupita njia unayoitafuta. Walioanzia ulipo wewe, nyuma yako au mbele yako na kufikia kile ambacho kwako ni ndoto ya maisha. Kujua kuhusu maisha yao yaweza saidia kukupa nguvu, na mwangaza katika safari ya maisha yako.

Binadamu ni viumbe wa mazoea, na sio kwa ubaya. Zama za kale tulijifunza kuzoea misimu, tukawa wakulima. Katika zama hizo tukajifunza kuzoea wanyama, na tukajikuta wafugaji. Tukajifunza kuzoea usalama na binadamu wenzetu tukajenga miji na majiji na kuvumbua mambo mengi ya kustaajabisha.

La muhimu kutambua ni kwamba mara nyingi mabadiliko yanaletwa na wale ambao wanathubutu kujivua mazoea. Wanao diriki kuwaza kwamba kuna namna tofauti ya kufanya au kuwaza jambo ambalo limekwisha zoeleka.

HITIMISHO
Maisha ni mapana, na kila mtu ana changamoto na pia fursa za kwake kwa namna ya kipekee. Na ndio maana hakuna jibu moja linaloweza kumfaa kila mtu. Sio lazima uwe uliyejipanga au kujiandaa sana ili ufanikiwe, na vile vile si kwamba ukiwa na ratiba kuanzia kuamka hadi kulala basi lazima ufanikiwe, hapana.

Maandalizi ni kifaa cha kukusaidia kuongeza uwezekano wa kufanikiwa katika maisha. Umakini wako kimaandalizi binafsi, nadharia na vitendo pamoja na maandalizi ya muda ni vitu vitakusaidia kuhimili mikiki ya maisha. Maandalizi ya kimazingira yanakupa wepesi wa kuweza kuifanyia kazi na kunufaika na fursa zinazoweza tokea.

N.B

Maandalizi yanawezekana tu pale unapokua umejitambua na unajua unapotaka kwenda. Soma andiko hili ili kuzifahamu mbinu za kujitambua.

- SoC 2022 - Uchumi: Siri ya mafanikio ya kudumu
 
Upvote 0
Back
Top Bottom