Zack Abdul
JF-Expert Member
- Mar 9, 2026
- 1,194
- 911
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na usambazaji wa video mbalimbali mitandaoni za kuhadaa vijana ili waingie kwenye vurugu zinazopachikwa jina la maandamano ya Julai 7.
Miongoni mwa Video hizo ni za matukio ya zamani ikiwemo ya maandamano ambayo yaliruhusiwa kisheria na kupewa ulinzi na polisi, video hiyo pamoja na mambo mengine inamuonesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwakumbusha wafuasi wa Chadema wakienda kwenye maandamano wakaandamane kwa amani, video hiyo ni ya zamani, Januari 24, 2024 na haihusiani na hali ya sasa. Ni muhimu kwa vijana kuwa makini na kuchunguza ukweli wa taarifa kabla ya kuziamini au kuzisambaza.
Mitandao ya kijamii imekuwa chombo muhimu cha mawasiliano, lakini pia kuna matapeli na wahalifu wasiopenda amani ya nchi yetu ambao kwa makusudi husambaza taarifa za kupotosha ili kuwaingiza mkenge wananchi hasa vijana.
Video za zamani zinapowasilishwa kana kwamba ni matukio ya sasa lengo la wahalifu hao ni kuwahadaa wanachi ili waamini kinachoitwa maandamano ya Julai 7 yameruhusiwa kisheria kumbe si kweli.
Wananchi hususan Vijana wanashauriwa kuthibitisha tarehe, mahali na chanzo cha video au taarifa yoyote wanayoipokea. Kutegemea vyanzo rasmi na vya kuaminika kutasaidia kupata taarifa sahihi na kuepuka kudanganyika na hatimaye kujiingiza matatizoni.
Kila mmoja ana wajibu wa kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na uwajibikaji. Badala ya kusambaza taarifa zisizothibitishwa, ni vyema kushiriki ujumbe unaojenga amani, umoja na maendeleo ya jamii.