SoC03 Mabadiliko haya katika elimu yatachochea uwajibikaji

SoC03 Mabadiliko haya katika elimu yatachochea uwajibikaji

Stories of Change - 2023 Competition

Mhagachi2023

New Member
Joined
Jun 25, 2023
Posts
2
Reaction score
2
Moja, kuanzisha somo mahsusi la katiba na sheria kuanzia shule ya msingi na ngazi ya sekondari. Mabadiliko haya katika mtaala wa elimu yatachochea watu kujua sheria na umuhimu wa kuzitii na kufuata sheria katika maisha ya kila siku. Maudhui ya somo hilo ni katiba ya nchi na sheria zake. Ni vigumu watu wasiojua sheria zinasema nini juu ya jambo fulani wakaweza kupambana na uvunjwaji wake, wakashiriki kuzitekeleza, na wakazisimamia kikamilifu. Hii njia itapelekea watu wengi katika jamii kuzijua sheria mbalimbali.

Moja ya nguzo muhimu katika utawala bora ni utawala wa sheria. Watu wakiwa na ufahamu wa katiba yao na sheria zake, usimamizi, utekelezaji, na ulinzi dhidi ya uvunjwaji wake ni mambo yanayowezekana. Kwa lugha nyingine, sheria zinakuwa hai. Kubwa zaidi, watawala wanakuwa wanajua kuwa watu wana ufahamu wa sheria, hivyo hawatafanya mambo kiholelaholela. Hata sheria zikivunjwa, watu wanajua kwamba sheria fulani imevunjwa na pia wanajua nguvu yao kisheria kupambana na uvunjwaji huo. Uvunjwaji wa sheria umefanyika mara nyingi na maeneo muhimu sana. Tukio kubwa kuwahi kufanyika ni pamoja na lile la kumtoa ofisini mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, mtu muhimu kabisa katika utawala bora anaweza kuchezewa hivyo na umma uko kimya. Jibu ni moja tu, hawana ufahamu juu ya mambo hayo ya kikatiba. Watu kujua katiba na sheria zinasema nini katika mambo mbalimbali itawaondoa watu katika giza nene.

Mbili, kupanua na kuidhatiti elimu ya ufundi na kilimo katika ngazi ya msingi na sekondari. Haya maeneo mawili (kilimo na ufundi) yanabeba shughuli nyingi katika jamii, ukizingatia sehemu kubwa ya jamii inaishi vijijini. Ajira ya moja kwa moja ni kilimo, pia ni shughuli ambayo watoto kwa watu wazima wanajishughulisha nayo kama watoto (Taifa la kesho) mashuleni watapewa elimu ya kilimo, kilimo kitaboreka na kuleta tija katika jamii. Maarifa yatakayotolewa ngazi ya msingi yatakuwa ya jumla na kumpa mwangaza mtoto kuhusu kilimo na ufundi, na katika ngazi ya sekondari maarifa yatatakiwa kumpa uwezo mwanafunzi kufanya kilimo au ufundi katika namna iliyobora. Hii itatakiwa kuambatana na kuandaa walimu wazuri na vitendea kazi vyote ili kufanikisha ufundishaji. Soko la bidhaa za kilimo ni kubwa na la uhakika, kuna nchi nyingi zina mazingira magumu ya kufanya kilimo. Hapa faida kubwa itapatikana katika jamii. Ufundi ni maarifa muhimu katika jamii yoyote inayoendelea. Inaweza kuwa ufundi umeme, umakenika, useremala, uashi, kupaua nyumba, kupakarangi, ususi, usonara, ushonaji mbalimbali, n.k. Kwa kiasi kikubwa, aina zote za ufundi zinahitajika hata vijijini. Badala kutegemea VETA, shule zetu za msingi (ambapo yatatolewa mafunzo ya awali) na sekondari za kata (ambapo yatatolewa mafunzo ya muendelezo kama yale yanayotolewa VETA), hadi kufikia hapo kila mtu atakuwa amepata mafunzo ya kitu cha kufanya katika maisha tofauti na ilivyo sasa.

Kwa hiyo, kuelimisha watoto mashuleni (kilimo na ufundi) ni uwekezaji muhimu. Utapunguza tatizo la ajira na wataweza kujiajiri. Ukiangalia ufaulu wa wanafunzi katika ngazi ya sekondari ya chini (hasa sekondari za kata), utagundua kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hawamudu masomo ya sekondari. Hapo ndipo hitaji hili la kuwapa elimu ya kilimo na ufundi linapokuwa na uzito, na masomo ya sekondari kuwa sio lazima (watasoma wanaoweza).

Pia, mnyororo wa shughuli zinazotokana na kilimo ni mrefu. Kuna watu wataingia shambani na kufanya uzalishaji, kuna watu wataongeza thamani kilichozalishwa, kuna watu watafanya biashara ya mazao ya kilimo yaliongezewa thamani hata yale ghafi pia, kuna watu watafanya biashara ya chakula (migahawa) n.k. Wote hao kwa ujumla wao watatoa ajira kwa watu wengine na hivyo kufanya jamii yao kuendelea.

Tatu, walimu wanaofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya ualimu watambuliwe na wapewe motisha kuongeza ufanisi wa kazi. Wanaweza kupewa nyongeza maalumu ya mshahara, na kwa mwalimu anayeonekana kufanya vizuri kwa muda mrefu anaweza kupandishwa daraja. Hii itachochea ufanisi na uwajibikaji miongoni mwa walimu, tofauti na hali ya sasa ambapo wanaofanya vizuri, wazembe, wavivu, na wategeaji katika kazi wote wanawekwa kapu moja. Hii si sawa.

Tumesikia mara kadhaa mwalimu akijishughulisha na kazi binafsi muda wa masomo. Halafu unakuta mwalimu mwingine anatumia muda wake shuleni, kisha mshahara na upandaji wa madaraja ni sawa kwa walimu wote. Hii inashusha morali ya kazi, hii inapunguza uwajibikaji na kupelekea kushuka kwa ufanisi wa kazi.

Nne, kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, somo la TEHAMA linatakiwa kuwekewa mkazo zaidi. Tumesikia hivi karibuni kuwa moja ya sababu ya kubinafsisha bandari zetu ni kukosa ufanisi ikiwemo mifumo ya TEHAMA. Ni vigumu kwa mfumo wa sasa kupata wataalamu wa TEHAMA wabobezi hata kama mhusika amepata elimu ya chuo kikuu. Mazingira ya elimu yanamnyima mtu uwezo wa juu wa TEHAMA. Fikiria mtu anakuja kujua matumizi ya kawaida ya kompyuta akiwa chuo kikuu, ni kwa muujiza tu mtu huyo kuwa mbobezi wa TEHAMA. Watu wenye uwezo mkubwa wa akili tunao, tunachohitaji ni maboresho ya mfumo wetu wa elimu. Napendekeza kutenga kila mkoa shule ya sekondari na kuipa vifaa vyote vya kujifunzia TEHAMA. Hizi shule zitachukua wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya sayansi ngazi ya shule ya msingi. Hizi shule zitawaandaa wanafunzi kwa masomo ya juu ya TEHAMA kidato cha tano na sita. Uchumi kama unaruhusu shule hizi maalumu ziwepo hadi ngazi ya wilaya, tutakuwa tumeongeza wigo wa kupata wanafuzni wengi zaidi. Hapo mwanafunzi akifika chuo kikuu anakuwa ameshaandaliwa kuwa mbobezi katika TEHAMA. Hatuwezi kuajiri watu kutoka nje kwa ajili ya kuleta na kuendesha mifumo ya TEHAMA iliyobora. Fikiria mtaalamu wetu wa TEHAMA anajifunza kwa mara ya kwanza kutengeneza program za kompyuta akiwa chuo kikuu. Angeweza kupata msingi wa hayo masomo mapema, mfano mtu anasikia kuwa kuna lugha za kutengenezea program za kikompyuta akiwa chuo kikuu. Angeweza kuyajua hayo mapema ngazi ya sekondari na kufanya mazoezi akiwa kidato cha tano na sita. Akifika chuo kikuu, ni muendelezo.

Tano, katika mafunzo ya udaktari, wataalamu wetu wapewe mafunzo kwa vifaa vya kisasa. Hii itatuhakikishia kuwa wanapomaliza masomo, wanakuwa na ubora wa juu wa masomo yao. Yale mazoea ya kupeleka watu nje ya nchi yanaonesha upungufu katika mafunzo ya wataalamu wetu. Na sababu inayosemwa ni kukosa vifaa vya kisasa. Sasa suluhisho ni kuleta hivyo vifaa ili madaktari wajifunzie katika mazingira ya kisasa. Wakati fulani, Hayati John Pombe Magufuli alifanya ziara Hospitali ya Taifa Muhimbili na kukuta mashine za CT scan na MRI ni chache na hazifanyi kazi. Hii inaonesha mazingira ya kujifunzia ya madaktari wetu ni duni. Pia, pawepo na program maalumu ya kupeleka wataalam nje ya nchi kwenda kuchota maarifa. Nimesikia kiongozi mkubwa akiomba kusaidiwa kusomesha madaktari bingwa. Alisema hata wawili. Hii inaonesha hali ilivyo katika sekta ya Afya.

Mwisho, naamini maeneo niliyoyagusa katika mada hii yakifanyiwa kazi, yatapelekea kuongezeka uwajibikaji na huduma kuwa bora, hivyo utawala bora.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom