WanaJF,
Kwa wale mliofuatilia mijadala mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ambayo yamezaa kitu kiitwacho "Nchi ya Zanzibar," ningependa kupitia vipengele kadhaa vya Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar 1984, Na. 9/2010 ili kujua mambo kadhaa yaliyobadilika, ikiwa ni pamoja na status ya Zanzibar kuwa "nchi kati ya nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," vilevile nitagusia mambo mengine yanayogusa Muungano wa Tanzania!
Kifungu cha 3: Kinazungumzia kuwa Zanzibar ni Nchi ambayo mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogovidogo vilivyoizunguka bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Kifungu cha 4: Kinadai kwamba: Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vifungu cha 9, 10 Vinagusa Muhimili wa Mahakama: Kifungu hiki kimerekebisha Ibara ya 24 (3) na ya 25A ya Katiba ya Zanzibar, 1984 na kinadai kwamba kama haki ya mtu yeyote inavunjwa au inaelekea kuvunjwa anatakiwa afungue shauri katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na kilichoongezeka katika mabadiliko haya ni kwamba shauri hilo halitafikishwa katika mahakama ya Rufani ya Tanzania. Haijulikani ni kwa nini hakuna Rufaa tena kama ilivyokuwa awali!
Kifungu cha 11 kinamtaja Rais wa Zanzibar kama "Mkuu wa Nchi ya Zanzibar," Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Kifungu cha 14 kimerekebisha Ibara ya 29 ambayo ilikuwa inalitaka BLW kuongeza muda wa uhai wake endapo Tanzania ipo kwenye vita "ikiwa Zanzibar inahusika na vita hiyo" sasa hivi maneno "ikiwa Zanzibar inahusika" yameondolewa. Hapa ilikuwa inaonesha wazi kwamba endapo ingetokea vita dhidi ya Tanzania kama ilivyokuwa vita ya Uganda, Zanzibar ingejiweka pembeni kama eti haikuhusika na vita hiyo!
Kifungu cha 19 kimefuta allegiance ya Rais wa Zanzibar kwa Muungano kwa kurekebisha Ibara ya 37 (2) ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Kabla ya Mabadiliko Ibara hiyo ilikuwa inasema kwamba Rais wa Zanzibar anaweza kushtakiwa na BLW kwa kuwa "na mwenendo unaodhalilisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar," katika hali ya kushangaza maneno hayo yameondolewa na badala yake yamewekwa maneno "au amekuwa na mwenendo unaokidhalilisha kiti cha Rais."
Kifungu cha 37 kimeondoa ulazima wa Rais wa Zanzibar kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kugawa mikoa ya Zanzibar!
Kifungu cha 48 kinaelezea kuhusu mabadiliko ya Katiba yanayohitaji kwanza kura za maoni ambayo ni kama ifuatavyo:
- Vifungu vyote vya Sura ya Kwanza ya Katiba ambavyo vinazungumzia Zanzibar na Watu,
- Kifungu cha 9 ambacho kinazungumzia Serikali na Watu.
- Vifungu vyote vya Sura ya Tatu ambavyo vinazungumzia "Kinga ya Haki za Lazima na Uhuru wa Mtu Binafsi."
- Kifungu cha 26 ambacho kinazungumzia Ofisi ya Rais,
- Kifungu cha 28 ambacho kinazungumzia muda wa kuendelea urais,
- Vifungu vyote vya Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu ya Sura ya Nne isipokuwa kifungu cha 49 na 50,
- Kifungu cha 80A na 123 vya Sura ya Kumi.
Hata hivyo BLW linaweza kuweka Azimio la Kurekebisha vifungu husika bila kupitia kura za maoni.
Kifungu cha 64 kimerekebisha Ibara ya 124 (2) ya Katiba ya Zanzibar, 1984 kwa kuongeza idadi ya vyombo vya Muungano ambavyo vinapaswa kuwa na Mamlaka Zanzibar. Kabla ya marekebisho vyombo hivyo vilikuwa hivi vifuatavyo:
- Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
- Tume ya Kudumu ya Uchunguzi,
- Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano.
Chombo kilichoongezeka kwa sasa ni "Tume ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano."
Hayo ndiyo baadhi ya Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, 1984 na ambayo yanagusa Muungano kwa namna moja au nyingine! Mabadiliko hayo tumeambiwa kwamba yanalenga "kuimarisha Muungano!" Sijui kama kuna ukweli kiasi gani kuhusu hili!
Tujadili!