Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Taarifa zilizopatikana kutoka wizarani zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 150 na 200 husafirishwa na Serikali kwenda nchini India, ambako kuna uhakika wa matibabu, kila mwaka. Idadi hii haijumushi wale wanaolipiwa na ofisi zisizo za serikali au wanaojilipia wenyewe.
Msemaji wa wizara ya afya, Nsachris Mwamaja anaeleza kuwa serikali huwapeleka nje wagonjwa wote wenye mahitaji japokuwa haweki wazi kiasi kinachotengwa kwa ajili hiyo.
Mtu yeyote ambaye atathibitishwa kutoka hospitali za serikali kama Muhimbili na Bugando hugharamiwa matibabu yake yeye pamoja na wanaomsindikiza. Wote hupokelewa na mwambata wa afya aliye katika ubalozi wetu katika nchi husika ambako amependekezewa akapate matibabu hayo, alisema na kuongeza kuwa:
Kiasi cha fedha kinachotengwa hubadilika kila mwaka na huweza kuongezwa kama itaonekana kuna haja katika mwaka husika.
Kwa taarifa zilizopatikana kutoka ubalozi wa India ni kwamba kila mgonjwa anapewa nafasi ya wasaidizi wawili wanaoruhusiwa kuambatana naye na kila mmoja ni lazima awe na taarifa ya fedha ya benki (bank statement) isiyopungua dola za Marekani 1,500.
Hii ni lazima kwa wale wote wanaojilipia au wanaolipiwa na makampuni binafsi, anasema Karki.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la maradhi ya moyo ulimwenguni. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa takribani watu milioni 12 wanakufa kwa maradhi haya duniani kila mwaka huku kukiwa na ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka hapa nchini.
Pamoja na ongezeko hilo, matibabu ya maradhi hayo bado hayakidhi mahitaji kutokana na idadi ya wagonjwa kulemea uwezo wa vituo na hata wataalamu wa kitengo hicho waliopo. Mpaka wakati huu ni hospitali chache zinafanya upasuaji wa moyo na kutibu magonjwa yake nyemelezi.
Hospitali ya Aga Khan
Mkurugenzi wa tiba wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee anathibitisha uwepo wa tatizo hilo na kusema kuwa hospitali yake inajipanga kutoa huduma za uhakika za matibabu hayo hapa nchini; kwa wananchi na hata wageni.
Tumeanza ujenzi wa jengo litakalokuwa maalumu kwa ajili ya maradhi ya moyo ambalo litakamilika Julai mwaka huu. Litakapo kamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 24 kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza idadi ya wanaoenda nje. Tayari tunao madaktari bingwa watatu watakaotoa huduma hiyo, anasema mkurugenzi huyo. Hospitali hiyo hupokea wagonjwa wa moyo wapatao 4,320 kwa mwaka ambao hulazimika kuwasafirisha nje ya nchi kutokana na yenyewe kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.
Kituo cha Moyo-Muhimbili
Mwishoni mwa mwezi Aprili Rais Kikwete alizindua kituo cha upasuaji, tiba na mafunzo ya moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kituo kilichogharimu kiasi cha Sh26.6 bilioni kimejengwa na serikali kwa ufadhiri wa Serikali ya Watu wa China iliyotoa Sh16.6 bilioni huku kilichobaki kikitolewa na Tanzania.
Kituo hicho chenye vitanda 98 na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 400 kwa siku kina changamoto ya wataalamu wa kutoa huduma hiyo kiasi cha kumshawishi Naibu Spika wa Bunge la China, Chen Changzhi, kutoa ahadi ya kuleta wataalamu hao kutoka nchini kwake wakati serikali ikiendela kuwaandaa wa kwake.
Kituo tunachokizindua leo ni chenye vifaa vya hali ya juu vinavyotumia teknolojia ya kisasa katika uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo. Kupatikana kwa kituo hiki, Tanzania inapiga hatua nyingine muhimu katika kuendeleza huduma ya afya nchini, alisema Rais na kuongeza:
Maradhi haya yameanza kuwa tatizo kubwa hapa kwetu, hivyo hatuna budi kuchukua hatua thabiti kukabiliana nayo.
Kwa upande wake Changzhi, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa katika kuendeleza mahusiano mazuri yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili, serikali yake italeta madaktari wa moyo 48 ili wasaidie utoaji wa huduma hiyo hapa nchini.
Fursa
Kwa kujijengea uwezo wa ndani wa kutoa huduma za upasuaji wa moyo siyo tu Tanzania itaokoa fedha zinazotumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi, lakini itajipatia fedha za kigeni kutoka nchi jirani ambazo hazijaanza kutoa huduma hii.
Dk Dharsee anaeleza kuwa kwa sasa wanalazimika kupeleka mgonjwa mmoja kila baada ya wiki tatu nchini Kenya, ambako wana hospitali kubwa, kwa ajili ya huduma zaidi lakini anasisitiza kuwa kukamilika kwa kituo cha hapa nchini kitakuwa msaada kwa watu wengi.
Tunatarajia kuwa kituo kitatoa huduma hii kwa wagonjwa kutoka nchi nyingine tano tunazopakana nazo kama Kongo, Rwanda, Malawi, Msumbiji na Uganda. Tunatarajia kukiimarisha zaidi pindi kitakapoanza kufanya kazi, anasema Dk Dharsee. Naye mkuu wa kituo cha tiba na mafunzo ya moyo, kilichozinduliwa Muhimbili, Dk Robert Mvungi anasema kuwa wamejipanga kutoa huduma hiyo kama inavyotarajiwa na kwamba hakutakuwa na ubaguzi wowote.
Jukumu langu ni kutoa tiba bila kujali kama mgonjwa ni kiongozi wa serikali au raia wa kawaida. Wote watahudumiwa kwa usawa kama inavyotakiwa, anasema Dk Mvungi.
Taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya wagonjwa 363 wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo hapa nchini. Wagonjwa 330 wamefanyiwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na 33 katika kituo hicho kinachotarajiwa kufanya upasuaji mkubwa siku za mbeleni.
Wadau wa afya wanasema kuwa endapo serikali itashirikiana na sekta binafsi kuidhatiti sekta ya afya kuna dalili zote kuwa itajiingizia fedha nyingi za kigeni na kuondokana na madeni kama hili la Sh21 bilioni tunazodaiwa na nchi mbili; Afrika Kusini na India ambazo zimewekeza kiasi cha kutosha.
Pamoja na wizara ya afya kupitisha bajeti ya takribani Sh623 bilioni kwa mwaka huu wa fedha kamati ya bunge ya huduma za jamii iliinyooshea kidole serikali kwa kushindwa kutenga fungu la kutosha ikiwa ni pamoja na kutotekeleza mkataba wa Abuja, uliosainiwa mwaka 2001, unaozitaka serikali za nchi kutenga asilimia 15 ya pato la taifa (GDP) kwa ajili ya wizara ya afya. chanzo.Mabilioni yapelekwa nchini India - Makala - mwananchi.co.tz
YAANI SERIKALI INAPOTEZA MABILIONO YA MAPESA KUWAPELEKA WATU WAKATIBIWE NCHINI INDIA WAKATI HAPOO NCHINI TUNAO MADAKTARI? AU NDIO VIFAA HAKUNA VYA KUTIBIA? KAZI KWELI IPO.