SoC02 Mada ya aibu

SoC02 Mada ya aibu

Stories of Change - 2022 Competition

hatedthemost

JF-Expert Member
Joined
Oct 20, 2021
Posts
469
Reaction score
324
Unakumbuka ile mada ya shule wote tuliipenda na kuisubiri kwa hamu? Mada ile ambayo hata nyumbani hatukupaswa kuisikia? Ile mada tuliyodhani itajibu maswali tuliyoona haya kuuliza kwa sauti?

Naomba nikupeleke mpaka nilipokua darasa la sita, nimeketi na wenzangu tukisubiri kwa hamu mwalimu wa sayansi aingie darasani. Siku ile mwalimu alipaswa kuingia na kufundisha hiyo 'Mada ya Aibu'.

Mada hii wazazi wangu na wako walikuwa wakiiongelea kwa uoga na mara nyingine tulikuwa tukitolewa walipotaka kuiongelea. Mada hii inaleta mkanganyiko na amri ya sita kwenye dini ninayoiamini.

Pamoja na sisi tulikuwa na mshawasha wa kusikia mada ile ikifundishwa kwetu; ajabu ni kwamba mwalimu yule aliingia darasani na badala yake akatupa msururu wa maandishi nasi tuyaandike na akaishia pale. hakuzungumza kama tulivyotarajia.

Miaka mitatu baadae; Niko kidato cha pili ninasubiri mwalimu wa somo langu pendwa aingie darasani kuongelea mada ile ambayo sikufundishwa nikiwa darasa la sita.Siku ile nilidhani labda kwasababu umri umesogea, mwalimu angeongelea bila kuhofia.

Unataka kujua tulifundishwa nini? Huku ilikuwa mbaya zaidi kwasababu mwalimu aliingia na kuagiza tujisomee mada hiyo.

Kwa mara nyingine nilinyimwa haki yangu ya kujifunza mada ambayo inagusa maisha ya watu wote ulimwenguni. Mada ambayo mimi kama kijana na vijana wengine inatugusa.

Siku moja nilimuuliza mtoa huduma ha afya kuhusu mada hii,mbaya zaidi hata yeye pia alinionea aibu nilipomuuliza juu ya mambo hayo. Aliniona kuwa binti niliyeharibikiwa kimaadili. Ninakosea kuuliza ninavyojiskia. Ninakosea kuuliza juu ya mwili wangu na maswali yanayonitatiza.

'ELIMU YA AFYA YA UZAZI NA NGONO' ndio mada yenyewe! Leo ikiwa ni miaka sita tangu nimalize kidato cha pili, kunayo mambo mengi yaliyotokea, yapo mengi niliyoskia pia lakini kubwa zaidi ni kuwa nimefahamu kwamba kuna mengi mageni kuhusu mwili wangu kama mwanamke na mwili wa mwanaume tunapozungumzia maswala ya uzazi na ngono.

Uzazi wa mpango, haki ya kuomba na kuombwa ridhaa kabla ya kujamiiana, mimba, matamanio na yanayohusiana. Vijana wa kike na wa kiume hawafahamu juu ya miili yao na maswala ya kawaida kama hedhi na mzunguko wa hedhi na magonjwa ya zinaa. Yote hayo niliyafahamu vizuri baada ya kuamua kuondoa aibu na kutazama mada hii kwa uwazi, kusoma vitabu,kuuliza maswali bila kuwaza jinsi watakavyonitazama na kutokuacha kuwa mwanafunzi.

Aibu mpaka lini na kwanini? kwanini aibu ya kuongelea swala linaloleta athari nyingi mpaka mwaka huu 2022? Mimba za utotoni na mimba zisizotarajiwa, athari nyingine ikiwemo wenzi kuogopa kusema wanaposhindwa kuridhishana katika tendo.

Mpaka lini hii aibu? Ni lini tutaacha kuwaona wanaopiga hatua kutumia kondomu na njia zinginezo za uzazi wa mpango ni watu walioshindikana? Mimi sitaona aibu nitasema. Nitasema tena kwamba nilinyimwa haki yangu ya kufahamu mwili wangu vizuri, nilinyimwa haki ya kuelewa kwamba hedhi si jambo la ajabu, nilinyimwa haki ya kuelewa kwamba matamanio ya kimwili ni kawaida kwa mtu yeyote anapofikia umri wa balehe. Nilinyimwa haki ya kufahamu Uzazi wa mpango. Mimi naidai jamii yangu wewe je?

Je, unadhani ukimya kwenye mada hizi zisizongumzika tunasaidia tatizo la mimba za utotoni? Unadhani itawapa wanawake kwa wanaume sauti pale wanapofanyiwa ukatili wa kingono bila kujua ni ukatili? Unadhani itaokoa mahusiano yanayozunjika kutokana na kutokuridhishwa kimwili? Unadhani ukimya huu unazidi kudumisha maadili haya tunayoyatunza kwamba tusipotoa elimu sahihi itazuia vijana kuyafanya hayo tunayoyahofia? Unadhani itapunguza watoto tusiowatarajia?

Aibu hunizunguka mimi kama mwanamke na wanawake wengi ulimwenguni wanapopaza sauti kusema hawasikii raha wakiwepo na wenzi wao. Wakati jamii ikilazimisha wanawake wengi kujifunza jinsi ya kumridhisha mwanaume. Nasikia uchungu kwasababu zipo hadhi nyingi za wanawake wengi wanaopitia changamoto hiyo na inawapasa kukaa kimya kwasababu ni 'wanawake'. Wanaume nao wao huambiana wanajua sana kiasi kwamba hawataki kujua chochote kuhusu miili yao na miili ya wanawake .

Mimi sitaona aibu kuongea popote itakaponibidi! Sitamuonea aibu mdogo wangu kwani natamani ajue ana haki ya kukataa kujamiiana kama hayuko tayari, ana haki ya kupewa elimu ya afya ya uzazi na kuuliza maswali, ana haki ya kuongelea hedhi kama jambo la kawaida na sio uchafu. Natamani tungewekeza nguvu nyingi kwenye kuondoa aibu iliyofunika jamii yetu sisi kama walimu wa vijana wanaokua, wazazi wa vijana na watoa huduma wa afya ya uzazi na ngono kwa vijana.

Hujui ufanye nini? Nakuachia hili kama mzazi au mlezi;uwe mtu wa karibu na mtoto wako kwasababu wewe ni mtu mwenye sehemu kubwa katika maisha ya mtoto ama kijana. Anza kwa kumueleza sehemu asizopaswa kushikwa sehemu za mwili wake na mtu akiwa mtoto mdogo; muoneshe sehemu kama makalio na sehemu zake za siri, anapozidi kukua akielekea balehe mueleze mabadiliko yake ya kimwili hasa swala ya matamanio na ngono, mueleze swala ya mimba,mueleze kuhusu hedhi.

Umri unaposogea anapoelekea ujana mueleze mimba inavyotokea, muelekeze kuhusu mzunguko wa hedhi (kwa vijana wa kiume na wa kike), mueleze kuhusu njia zote za uzazi wa mpango zinazopatikana kwa faida na hasara zake.Inapowezekana mpeleke sehemu inayotoa huduma akaelimishwe.

Unaweza kuanzia hapo kuondoa aibu inayokabili afya ya uzazi na ngono. Ukali na vitisho havijaonesha kuzuia ngono. Naamini katika urafiki na ushirikiano wa familia, shule pamoja na sekta ya afya.

Naleta kwako mada hii ya aibu isiyozungumzwa kwa uwazi. Tupazie sauti 'mada ya aibu' na sote tuwe sehemu ya mabadiliko.

Nakuacha na msemo unaosema, "kamwe hauwezi kuwapakaza aibu watu waliomua kujivua aibu"
Nawasilisha!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom