Maji ya nazi (Madafu) ni kinywaji maarufu sana mtaani. Ni maji hanayopatikana kwenye nazi changa (Cocos nucifera) ambayo hubadilika kuwa tui baada ya kukomaa kwa nazi.
Kumekuwepo na madai kuwa maji haya sio salama kwa watu wenye Ugonjwa wa figo. Kwa kuongezea, mdau wa JamiiForums amesema kuwa madafu yanaweza hata kusababisha kifo kwa mhusika.
Ukweli wa taarifa hizi upoje?
Ukweli wa taarifa hizi upoje?
- Tunachokijua
- Maji ya nazi (Madafu) ni kinywaji chenye faida nyingi kwa afya. Kwa mujibu wa Taasisi ya USDA, Maji haya ni chanzo kizuri cha Nishati, protini, wanga, nyuzi lishe, madini chuma, calcium, zinc, sodium, copper, folate pamoja na aina mbalimbali za vitamini muhimu kwa afya.
Pia, madafu huwa na kiasi kikubwa cha madini ya Potassium ambayo pamoja na kazi zingine, huhusika katika kutunza kiasi cha maji kinachofaa kwa afya bora ya seli za mwili, kuongoza mfumo wa kati wa fahamu pamoja na kulinda misuli ya mwili hasa ile ya moyo na mishipa ya damu.
Kutokana na uwepo wa chumvi chumvi muhimu zinazofaa, maji haya yanaweza kutumika kwa watu wanaofanya mazoezi magumu, wenye shinikizo kubwa la damu pamoja na wale wenye changamoto ya kuhara.
Wagonjwa wa Figo
JamiiForums imezungumza na wataalam wa afya ambao wamebainisha kuwa utolewaji wa takamwili zenye Madini ya Potassium hufanyika kupitia mkojo.
Watu wenye ugonjwa wa figo wanaweza kupatwa na changamoto ya kubakiza mwilini kiasi kikubwa cha madini ya potassium kuliko kile kinachotakiwa ikiwa watakunywa kiasi kikubwa cha madafu. Hali hii ni hatari kwa afya, kitaalam huitwa Hyperkalemia.
Husababisha kutapika, kuharisha, maumivu makali ya kichwa, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, maumivu ya kuchomachoma kwenye vidole vya miguu na mikono, maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo pamoja na kuathiri mfumo wa fahamu za mwili. Isipotibiwa haraka inaweza kusababisha kupoteza maisha.
Watu wasio na changamoto za figo wanaweza kutumia maji haya pasipo shida yoyote kwa kuwa miili yao huwa na uwezo wa kutosha wa kuondoa mwilini kiasi cha ziada cha madini ya Potassium kupitia Mkojo.
Madafu na Mabusha, soma: KWELI - Maji ya madafu hayasababishi ugonjwa wa Mabusha