Maendeleo na usalama wa mtandao wa Internet vinatakiwa kwenda sambamba

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121


Katika miaka ya hivi karibuni mtandao wa Internet umekuwa ni moja ya maeneo yenye maendeleo ya kasi duniani. Kuanzia ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano kwa njia ya internet, vifaa vya mawasiliano kwa njia ya internet kama simu na kompyuta, na hata matumizi ya internet, serikali mtandao (e-gov), na hata biashara kwenye mtandao wa internet, mambo hayo yote yameonesha kuwa matumizi ya mtandao wa Internet ndio mwelekeo.



Kwenye mkutano wa kimataifa wa Internet uliofanyika hivi karibuni mjini Wuzhen, Zhejiang China, wenye kauli mbiu ya "Kuelekea kwenye zama mpya ya ustaarabu wa kidigitali - kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja kwenye mtandao wa Internet", maswala muhimu na yanayofuatiliwa kwenye eneo la Internet yalijadiliwa.



Kwenye barua ya pongezi kuhusu kufunguliwa kwa mkutano huo, Rais Xi Jinping wa China alitoa mwito wa kuhimiza uhai wa uchumi wa kidigitali, kuhimiza utoaji wenye ufanisi wa huduma za kiserikali kwa njia za kidigitali, kupanga vizuri mazingira ya kijamii ya kidigitali, pamoja na ushirikiano kwenye mambo ya kidigitali. Bila shaka mambo aliyosema Rais Xi kwenye barua yake yanasisitiza usimamizi bora wa mtandao wa internet, kwani matumizi ya internet kwa sasa yamekuwa ni jambo la kawaida na muhimu ambalo linaleta fursa nyingi, lakini pia lina changamoto zake.



Umuhimu wa Internet si suala la mjadala tena, kwani kuna ushahidi mwingi ulioonekana katika kipindi cha maambukizi ya COVID-19, ambapo internet iliwezesha kufanyika kwa mambo mengi ambayo yalikumbwa na changamoto kutokana na hatua za zuio. Tumeona kwenye sekta ya elimu ambapo shule ziliendelea kutoa elimu kwa njia ya internet (e-learning), tuliona kwenye sekta ya biashara kuwa uagizaji na uuzaji wa bidhaa kwa njia ya Internet (e-commerce) uliendelea, na hata baadhi ya shughuli za kiserikali ziliendelea kwa njia internet (e-gov).



Kwenye nchi za Afrika ambako licha ya kuwepo kwa maendeleo makubwa ya usambazaji wa huduma ya Internet, matumizi sahihi yenye manufaa ya huduma hiyo bado yako kwenye kiwango cha chini. Lakini katika kipindi cha COVID-19 kulikuwa na maendeleo yaliyoonekana kwenye biashara kwa njia ya mtandao wa internet. Na mfano mzuri ni biashara ya mazao ya kilimo kati ya China na Afrika, ambapo baadhi ya bidhaa zilinunuliwa zote ndani ya muda mfupi baada ya kuonekana kwa wateja wa China.



Hata hivyo ni wazi kuwa internet ni uwanja mpana sana ambao mbali na fursa zake, pia una changamoto zake nyingi. Na moja ya changamoto zilizojadiliwa kwenye mkutano wa Wuzhen, ni usalama wa Internet. Kwenye ufunguzi wa mkutano huo naibu waziri mkuu wa China Bw. Liu He, alisema usalama na kuaminika wa miundo mbinu ya internet, vinatakiwa kulindwa na dunia nzima, na serikali katika dunia nzima zinatakiwa kufanya juhudi kulinda usalama wa internet.



Serikali ya China imekuwa inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha usalama wa mtandao wa internet, na kupitisha sheria na kanuni mbalimbali kuhusu usalama wa Internet. Pia imesema itaendelea kuchukua hatua kutekeleza usimamizi wa sheria ya ulinzi wa habari binafsi.



Changamoto nyingine kubwa ambayo mpaka sasa inaonekana kutatiza maendeleo ya internet ni uhasama wa kisiasa na ushindani wa kibiashara. Hivi karibuni kumekuwa na vitendo vya wazi vya kukwamisha ushirikiano kati ya China na nchi nyingine duniani kuhusu maendeleo ya teknolojia ya 5G. Baadhi ya nchi za magharibi zimekuwa zinatumia kisingizio cha “usalama” kama moja ya nyenzo za kuizuia China kwenye ushindani wa kimataifa katika mambo ya internet.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…