Maendeleo yanayoonekana na simulizi za kisiasa: Kwanini wapo wasiotaka kuamini?

Maendeleo yanayoonekana na simulizi za kisiasa: Kwanini wapo wasiotaka kuamini?

MTANZANIA620

Senior Member
Joined
Jun 20, 2023
Posts
105
Reaction score
116
Na GULATONE MASIGA

Katika siasa, mara nyingi ushindani hauhusu tu nani anajenga zaidi, bali pia nani anafanikiwa kujenga simulizi linaloaminika zaidi na wananchi. Ndiyo maana wakati mwingine hata pale miradi mikubwa ya maendeleo inapotekelezwa, bado kunakuwa na sehemu ya jamii inayobaki na mashaka au kutokuamini ukubwa wa mafanikio hayo.

Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeendelea kutekeleza miradi mingi ya kimkakati katika sekta za nishati, usafiri, afya, elimu, maji, mawasiliano na viwanda. Miradi hiyo imekuwa sehemu ya mjadala mkubwa wa kisiasa, ambapo wapo wanaoiona kama ushahidi wa maendeleo ya nchi, na wapo wanaodai kasi hiyo haijafika kwa kiwango kinachotarajiwa au manufaa yake hayajasambaa sawasawa.

Katika sekta ya nishati, kukamilika kwa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha hadi megawati 2,115 ni moja ya miradi mikubwa zaidi katika historia ya Tanzania. Sambamba na hilo, uwekezaji katika vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme pamoja na kuendelea kusambaza umeme vijijini na vitongojini unaonyesha jitihada za kupanua upatikanaji wa nishati kwa wananchi na shughuli za uzalishaji.

Sekta ya uchukuzi nayo imeendelea kushuhudia uwekezaji mkubwa kupitia reli ya kisasa ya SGR, ambapo ujenzi unaendelea katika vipande mbalimbali vinavyolenga kuunganisha maeneo muhimu ya kiuchumi ndani ya nchi na nchi jirani. Vivyo hivyo, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege pamoja na madaraja makubwa unalenga kuongeza ufanisi wa usafiri na kuchochea biashara, utalii na uwekezaji.

Katika sekta ya viwanda, sera za kuvutia uwekezaji zimechangia kuanzishwa au kupanuliwa kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, zikiwemo vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, nguo, bidhaa za elektroniki na bidhaa nyingine za viwandani. Hali hii imeongeza fursa za ajira na kuchangia mapato ya serikali kupitia kodi na shughuli za kiuchumi.

Sekta za afya na elimu pia zimeendelea kupata uwekezaji mkubwa kupitia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, madarasa, maabara, mabweni na nyumba za walimu. Ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa umeongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma ambazo hapo awali zilihitaji wagonjwa kusafiri umbali mrefu au hata kwenda nje ya nchi.

Miradi ya maji safi na salama imeendelea kutekelezwa katika maeneo mengi, huku upanuzi wa minara ya mawasiliano na mkongo wa taifa ukiimarisha huduma za simu na intaneti kwa wananchi na wafanyabiashara.

Aidha, serikali imeendelea kusisitiza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuimarisha sekta ya madini, kukuza kilimo na kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mbalimbali. Haya ni maeneo ambayo kwa pamoja yanaathiri uwezo wa uchumi kukua na serikali kutoa huduma za umma.

Hata hivyo, Swali kubwa ni kwa nini bado kuna wananchi wasiokubaliana na simulizi ya mafanikio hayo? Sababu zinaweza kuwa nyingi. Baadhi hupima maendeleo kwa gharama ya maisha, kiwango cha ajira, kipato chao binafsi au ubora wa huduma wanazopata kila siku. Wengine huangalia zaidi kasi ya utekelezaji wa ahadi na wakitilia mkazo changamoto zilizobaki kuliko mafanikio yaliyopatikana.

Mwisho wa yote, tathmini ya uongozi wowote wa kisiasa haiwezi kujengwa kwa hisia pekee wala kwa propaganda pekee. Inapaswa kujengwa kwa kuangalia ushahidi wa miradi iliyotekelezwa, matokeo yake kwa wananchi, changamoto zilizobaki na uwezo wa kuzitatua. Hapo ndipo mjadala wa kisiasa unakuwa wa kujenga taifa badala ya kuwa mashindano ya kauli.
 
Back
Top Bottom