*TANGU RAIS MAGUFULI AINGIE IKULU ... ~ Prt 3*
Tuendelee kuchambua mambo 10 mengine yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Dk. John Pombe Joseph Magufuli* tangu alipoingia Ikulu mnamo Novemba 5, 2015. Leo tutamulika kuanzia nafasi ya 20 mpaka ya 30.
Tangu Rais Dk. Magufuli aingie madarakani tumeyaona haya yakitokea na kufanyika:-
21. Tumeshuhudia Rais Magufuli akifanya maamuzi magumu, ya haraka, sahihi na kwa wakati pindi Wananchi inapolalamika juu ya kukabiliwa na tatizo la kijamii. Ilishatokea kwenye hospitali ya Muhimbili pindi Mwanamama alipopaza sauti juu ya akina Mama wanaojifungua kulala chini, hapo hapo Rais Magufuli akaamuru zilizokuwa ofisi zibadilishwe na kuwa wodi, ikafanyika hivyo. Pia tusisahau Rais Dkt John Pombe Magufuli alivyowapa wakazi wa Bagamoyo, eneo la Magereza lenye ukubwa wa heka 65. Huyo ndio Dk. John Pombe Magufuli, mwenye maamuzi magumu, sahihi na kwa wakati.
22. Serikali ya Rais Magufuli imekuwa na desturi njema ya kulipa madeni ya ndani na ya nje. Mathalani tumesikia Serikali ikilipa madeni ya ndani ya Wakandarasi, watoa huduma, Waalimu n.k. Pia hivi karibuni Serikali kupitia kwa Msemaji Mkuu wa Serikali imesema imetenga Tsh. Trilioni 1 kulipa deni la Taifa.
23. Serikali ikiacha umangi meza na kwenda palipo na Wananchi, palipo na shida za jamii. Si Wakurugenzi, Wakuu wa wilaya, wa Mkoa, Mawaziri ama Makatibu wakuu wote wapo field kuhakikisha wanaenda kuzitambua na kuzitatua shida za Wananchi. Mtindo wa viongozi kubaki baki ofisini zaidi kuliko kuwa site ulishakufa tangu Rais Dk. Magufuli alipoingia Ikulu.
24. Urasimu kuwaona Viongozi umepungua; Miaka ya nyuma kumuona Kiongozi wa Serikali ilikuwa kazi ngumu kuliko hata kuisaka sarafu baharini, huo ndio ukweli. Viongozi walio wengi walijiwekea ukuta kiasi Mwananchi wa kawaida kumvikia ilihitaji uvumilivu wa hali ya juu. Tangu Rais Magufuli aingie viongozi wenyewe wa Serikali wameweka mfumo mpya wa kiutendaji kwa kutenga siku maalum (siku 2 ama 3 kwa wiki) ambazo Mwananchi anaenda kumuona kiongozi moja kwa moja pasipo kupita kwa Katibu Muhtasari (Sekretari). Pia wapo baadhi ya Viongozi wakubwa wa Serikali wanatoa mpaka namba zao za simu za mikononi ama za wasaidizi wao ili Wananchi waweze kuwasilisha kero na matatizo yao moja kwa moja. Utaratibu huo umerahisisha matatizo ya Wananchi kuweza kufika kwenye mamlaka kwa wakati na kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
25. Viongozi wamepewa meno zaidi; Tangu Rais Magufuli aingie madarakani tumeshuhudia Viongozi, mamlaka za kitaasisi zikipata meno zaidi ya kiutendaji tofauti na hapo awali kila kitu kuachiwa mamlaka ya Urais iamue, ulikuwa ni utegeaji wa hali ya juu. Mathalani leo hii tunashuhudia TAKUKURU ikipata meno zaidi ya kupambana na rushwa nchini hali iliyopelekea kesi za rushwa kuongezeka Mahakamani.
26. Kiwango cha nidhamu, uwajibikaji na uadilifu kwa Viongozi wa Serikali kimezidi kuongezeka. Tangu Rais Magufuli aingie madarakani yale mazoea yasiyo na tija ya viongozi kuzoea kazi hayapo, ule mtindo kiongozi akiharibu hapa anahamishiwa kule haupo, suala la kiongozi anafanya madudu na bado anabaki kwenye ofisi ya umma haupo tena. Kila Kiongozi ama kila Mtumishi wa umma yupo makini akichapa kazi vilivyo kwa nidhamu na uadilifu wa hali ya juu.
27. Ufuatiliaji wa utendaji, ufuatiliaji wa maagizo umekuwa wa hali ya juu. Tangu Rais Magufuli aingie Ikulu ameiambukiza sifa zake za uadilifu, uchapakazi, uzalendo na ufuatiliaji. Naam ufuatiliaji wa majukumu, maagizo, ripoti na tafiti zinazotolewa umekuwa wa hali ya juu. Pindi inapobainika madudu kufanyika ama jambo kutokufanyika kwa wakati Rais Magufuli hasiti kabisa kufukuza Mtu na baadhi yao kuishia mikononi mwa vyombo vya kisheria.
28. Utawala wa Sheria umezidi kuimarika. Rais Magufuli aliapa kuilinda na kuitetea katiba ya nchi iliyo na sheria, taratibu na kanuni, amefanikiwa katika hilo. Leo hii tunazidi kuona mihimili ya dola inapofanya kazi kiukamilifu pasipo mwingiliano, kila mhimili upo huru; Leo hii tunaona Viongozi, Wanasiasa, Watumishi wa umma wakipandishwa kizimbani na wengine wanahukumiwa kifungo jela pindi wanapokutwa na makosa ya kisheria. Hakika, utawala wa kisheria unaoonyeshwa na Serikali ya awamu ya 5 yake Rais Magufuli ni nguzo ya utawala bora.
29. Heshima ya Tanzania kimataifa imezidi kukua zaidi; Hali ya Tanzania kusikika zaidi ilikuwa juu sana kipindi cha awamu ya kwanza kutokana na uwepo wa Mwalimu Nyerere ambapo hii leo Tanzania imezidi kupata sifa zaidi kutokana na uchapakazi wa Rais Magufuli. Nchi mbalimbali Duniania zimekuwa zikivutiwa na Rais Magufuli kutokana na namna anavyopambana na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya pesa za umma, namna Serikali inavyobana matumizi na namna Rais Magufuli anavyoonyesha uzalendo wa kulinda rasilimali za Taifa zimnufaishe Mtanzania. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoifanya leo hii jina, hadhi na heshima ya Tanzania kuweza kupaa juu zaidi tangu Rais Magufuli aingie Ikulu.
30. Heshima ya Mwanamke imezidi kuimarika Serikalini na kwenye jamii. Dalili njema za Rais Magufuli kuweza kuheshimu nafasi ya Mwanamke ilianza kujitokeza pindi alipomteua Mama Samia Suluhu kuwa Mgombea mwenza wa Urais ambaye leo hii ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mama Samia ni Mwanamke pekee aliyeshika nafasi ya juu kabisa kiungozi katika nchi za Afrika Mashariki. Hata mara baada ya kuingia Ikulu Rais Magufuli ameongeza imani kwa kuwateua Wanawake kwenye nafasi mbalimbali za kiuongozi Serikalini. Pia amewateua na kuwapandisha vyeo kwenye nafasi za vyombo vya dola na hata wengineo kuwateua kuwa Majaji. Imani aliyoonyesha Rais Magufuli kwa Wanawake ni ishara tosha ya heshima kubwa aliyowapa Wanawake nchini.
*Na Emmanuel J. Shilatu*