SoC02 Mafunzo ya Mama

SoC02 Mafunzo ya Mama

Stories of Change - 2022 Competition

YasinthaPru

New Member
Joined
Aug 19, 2022
Posts
1
Reaction score
5
Sikuwahi kufikiria nitawahi kupata upenyo wa kuongea yaliyositirika kwa muda sana ila hatimae nimefikiwa. Nakumbuka mama aliwahi kuniambia "Mwanangu, siku zote tembea duniani ukivaa viatu vya watu." Kauli ile ilinichanganya ila kadri siku zilivyosonga nilielewa kuwa si kila kiatu ninaweza kuvaa, vingine vinabana na vingine vinapwaya.

Aliniambia mwanangu "Jembe halimtupi mkulima." Nilijua ni kweli ila likimtupa basi hajapata mbinu mbadala za kuweza kujipatia mavuno. Tanzania imebarikiwa wenyeji wenye kujikita na shughuli za kilimo zenye kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo kahawa, chai, tumbaku, korosho, mahindi, pamba na mboga mboga. shughuli hizi zimekuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusiana na kilimo bali kuna uwepo wa elimu ya uzoefu ambayo haiwanufaishi wakulima kwa asilimia kubwa na uvamiaji wa wadudu kwenye mashamba.

Kuna upatikanaji wa nyenzo nzuri za kilimo kama vile trekta za kisasa, mashine aina ya palleting zilizotengenezwa kwaajili ya kuwakomboa wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na kilimo zinazotumia muda mfupi kukoboa mpunga. kuna kilimo cha matunda, uzalishaji wa mbolea na usambazaji, kilimo cha uyoga na maua ambazo ni chache kati ya nyingi zinazoweza kuleta faida nchini endapo zitapewa kipaumbele.
View attachment 2358194
Food and agricultural org.

Wito: Kilimo kipewe kipaumbele kwa watu wote hasa hasa vijana wenye kuonesha nia ya kujifunza na kufanyia kazi, uwekezaji ufanywe kwenye sekta ya elimu inayohusiana na kilimo kusudi kuwepo na mavuno mengi yenye kuweka kilimo nchini katika hali nzuri ya kimataifa. Pamoja na hilo, kampuni mbalimbali zinazo pambana kukuza kilimo cha ndani zipewe motisha na nafasi kubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii

Alipoteza fikra hizo na kuniambia mwanangu "Elimu ni bahari, haiishi kwa kuchotwa." Ni kweli elimu haina mwisho ila baadhi ya walimu hutumia vibaya viapo. Waliapa watatumikia vyema kazi zao, vipi kuhusu wanafunzi wanaolazimishwa kuchota maji na kuchanja kuni wakati wa masomo? Watafika kweli au bora elimu? Vipi kuhusu mwalimu aliemchapa mtoto hadi kifo, je hakuweza kusoma alama za nyakati? Vipi kuhusu binti alieibiwa uschana wake bila kosa lolote? Atakuwa sawa kweli, au bora msongamano na mawazo ya kuondoka duniani? Vipi kuhusu binti aliekosa taulo la kujistiri na kufukuzwa bila sikio kutegwa kwa kushindwa kuhudhuria masomo? Atawahi kuwa na kuona thamani yake kweli au mabadiliko ya mwili yataenda sambamba na chuki binafsi?

Tanzania imepambana kindaki ndaki kukwamua elimu kwa asilimia kubwa sana. Kumekuwa na ujenzi wa madarasa kwa maeneo mbalimbali nchini, ambayo yamejengwa kisasa kwaajili ya kuwatengenezea wnafunzi mazingira bora ya kujisomea. Kuna taasisi mbalimbali zilizojitolea kuwasaidia wanafunzi na mahitaji ikiwemo madaftari, madawati, vyakula, taulo za kike pamoja na mavazi. Hatua hizi zimepelekea kuwepo na ongezeko la ufaulu nchini na kuongeza hamasa kwa wanafunzi kutaka kujifunza kwa kasi na kwa malengo. Walimu nao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanafunzi kujifunza, huku wengine wakiwa wanapambana na hali zao za nyumbani, serikali imehakikisha wanafunzi hasa hasa waliokatisha masomo kutokana na kupata mimba wanarudi shuleni ili kujikomboa kielimu. Sekta kubwa ambayo imepewa kipaumbele ni ya elimu ambayo imepelekea wananchi kushirikiana katika kupiga marufuku maudhui mabaya yanayofanyika na walimu wasio na uchungu wala utu na kazi yao kwakuwa ‘adhama ya mtu hutoka kwake mwenyewe.’

Changamoto kubwa zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara ni pamoja na, walimu kutumia vibaya madaraka yao, wanafunzi kushindwa kuendelea na masomo kutokana na hali zao nyumbani, ikiwemo uchumi na mila zinazokandamiza watoto hasa mabinti kwenda shule.

Wito: Sheria iwashughulikie vikali walimu wenye kwenda kinyume na taaluma zao bila kuangalia cheo wala nafasi katika jamii, elimu izidi kutolewa kwa makabila yenye mila zinazofanya watoto kushindwa kwenda shule na wale wenye kukaidi maagizo ya serikali wachukuliwe hatua stahiki. Elimu ya ujasiriamali iendelee kutolewa kwa wahitimu kusudi waweze kutumia elimu hiyo katika kuwapatia kipato kwa njia halali. Elimu iweze kutolewa kwa wajasiriamali wadogo kuhusinana na njia nzuri za kutumia kujipatia kipato zaidi ili kuongeza uchumi binafsi na wa nchi kwa ujumla.
Screenshot_20220915-213235.png

Tanzania Education Authority

Nilimsikiliza mama kwa umakini nikataka niseme neno,akaninyamazisha na kuniambia "Huchelewi kujisahihisha." Niliingia ndani ya ubongo wangu na kutafuta maana kwa muda wa takribani dakika tatu nijue ni wapi nilikosa ili nijirudi ila wapi, ndipo mama akafunguka na kusema "Mwanangu, siku zote kumbuka ya kuwa haujachelewa kubadilika wala kupokea mabadiliko." Ndipo nilipogundua mama alikuwa haniongelei mimi bali anaongelea mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini. Mnamo miaka ya hivi majuzi, teknolojia imekuwa ikikuwa kwa kasi, hii imepelekea nyanja nyingi zikiwemo za viwanda, kilimo, mawasiliano na ufundi kunufaika kutokana na hilo.

Teknolojia imerahisisha maisha kwa viwango vya juu kabisa kwakuwa shughuli nyingi zinafanyika kwa haraka na urahisi wa hali ya juu. Kumekuwa na ukuaji wa soko la biashara nchini kwa kasi sana. Teknolojia hizo ni pamoja na vikokotozi kwaajili ya kufundishia, vitambazi kwaajili ya kuangalia ubora na uhakiki wa bidhaa, simu za mkononi kwaajili ya mawasiliano, mashine za kukoboa zinazowarahisishia kazi wakulima na nyinginezo nyingi zenye kurahisisha maisha.

Changamoto zilizojitokeza kutokana na teknolojia kwakuwa 'akuna masika yasiyokuwa na mbuu' ni pamoja na kupotea kwa fasihi simulizi kutokana na watu wengi kupendelea sinema na muziki, hivyo kupelekea mila nazo kupotea na mababu zetu bila kurithisha hekima na maarifa kwa kizazi hiki kwa kupitia fasihi simulizi. Shughuli nyingi za viwandani kufanyika na mashine maalumu na hivyo kupelekea ukosefu wa ajira katika sekta hiyo. Kilimo bado kuwa na changamoto zake kutokana na wakulima wengi kukosa elimu ya kutosha juu ya uendeshaji wa teknolojia mbalimbali hivyo kupelekea mazao ya biashara kuwa na uchache kuliko mazao ya kula.


Screenshot_20220915-214215.png

Awali Mwaisanila

Wito: Elimu itolewe kwa upana zaidi juu ya suala zima la sayansi na teknolojia hasa masomo ya sayansi yapewe kipaumbele kwa wanafunzi wenye kuonesha kuvutiwa na sekta hiyo. Fasihi simulizi ihamasishwe kwa kiwango fulani kuhusu kutopoteza kabisa mila na desturi za nchi. Wakulima wenye kujikita na mazao sana sana ya biashara wapewe elimu ya kutosha juu ya mbinu za kisasa zenye kuleta matokeo mazuri na kwa urahisi zaidi.

Mama alisema nami hayo yote na maneno yake yalikuwa ni yenye hekima, busara na uchungu ndani yake. Macho yake yalijawa kiu ya kutaka nifikishe ujumbe huu kwa jamii kwakuwa huenda yanaweza yakaleta mabadiliko kwa kiasi fulani. Basi baada ya hapo alimalizia kwa kusema "Mwanangu, chawa si nzito lakini husumbua, usidharau haya nayokuambia, ni heri kudhibiti tatizo mapema kuliko kusubiri likuelemee."
 
Upvote 6
Back
Top Bottom