“Kutoka mtwana kuwa bwana, na kuondokana na umaskini na kuwa na maisha bora, ni mambo mazuri zaidi niliyopata maishani mwangu!” Bibi Shiangchiu Ram mwenye umri wa miaka 77 ni makzi wa kijiji cha Anmaixi, Mji wa Chamdo, kusini-mashariki mwa Tibet. Ana nyumba nzuri kubwa ya orofa tatu iliyo karibu na bustani ya maua, na anafurahia sana maisha yake ya anasa. Kwake, anaishi maisha katika dunia nyingine kama ikilinganishwa na zaidi ya miaka 60 iliyopita. Wakati huo, watu wote wa familia yake walikuwa watwana, walikuwa wanaishi katika kibanda kibovu hata wakati wa siku za baridi, walikodisha mashamba ya kabaila, na kumpa zaidi ya asilimia 90 ya mavuno yao, na ilikuwa vigumu sana kwao kupata chakula cha kutosha ingawa walifanya kazi kwa bidii.
Mfumo wa watwana wa kilimo mkoani Tibet ulianza katika karne ya 10, na kuendelea hadi katikati ya karne ya 20. Wakati huo, mfumo wa utumwa ulikuwa umeachwa kabisa duniani, lakini huko Tibet, bado kulikuwa na mamilioni ya watwana. Kutokana na mfumo wa watwana wa kilimo, makundi matatu ya mabwana, wakiwemo maofisa, makabaila, na masufii wa tabaka la juu, ambao walichukua chini ya asilimia 5 ya idadi ya watu mkoani Tibet, walimiliki ardhi na karibu mifugo yote.
Watwana hawakuwa na chochote, mabwana ama makabaila waliwanyima haki zao zote, walikuwa na uwezo wa kuanzisha mahakama za kibinafsi, kuwaadhibu na hata kuwaua watwana wao kama wanavyopenda. Mfumo wa watwana wa kilimo ulikuwa kikwazo kwa maendeleo ya Tibet, na ulipingwa sana na watu. Mwezi Machi, mwaka 1959, kikundi cha masufii wa tabaka la juu huko Tibet, kilichoongozwa na Dalai Lama, kilianzisha uasi kwa lengo la kuifarakanisha China ili kudumisha mfumo wa watwana wa kilimo. Tarehe 28 Machi, mwaka 1959, serikali kuu ya China ilitangaza kuvunja serikali ya eneo la Tibet, na kuanzisha Kamati ya Maandalizi ya Mkoa Unaojiendesha wa Tibet, ili kuendesha mamlaka ya Tibet, na kufanya mageuzi ya kidemokrasia huku ikizima uasi, na kutokana na uamuzi huo, karibu watwana milioni moja walikombolewa.
Baada ya mageuzi ya kidemokrasia, mfumo wa watwana wa kilimo wa Tibet ambao ulidumu kwa karibu miaka elfu moja ulipinduliwa, na watwana wakageuka kuwa mabwana wa Tibet, wakapewa ardhi na haki za kisiasa, kiuchumi na kijamii sawa na watu wa kawaida. Kutokana na sababu za kijiografia na kihistoria, kiwango cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii cha Tibet kimekuwa nyuma kwa muda mrefu. Baada ya kuondolewa kwa mfumo wa watwana wa kilimo mkoani Tibet, China imetekeleza miradi mingi mikubwa ya kiuchumi inayohusiana na maendeleo ya muda mrefu ya Tibet na uboreshaji wa maisha ya watu, na kupata mafanikio makubwa.
Mwaka 2021, pato la mkoa wa Tibet lilizidi dola bilioni 31.45 za Kimarekani, na kiwango cha ukuaji wa uchumi kimekuwa mbele ikilinganishwa na mikoa mingine nchini kwa miaka mingi. Wakulima na wafugaji wa Tibet bila shaka ni kundi linalofuatiliwa zaidi. Kuanzia mwaka 2012 hadi 2020, wastani wa kipato cha mtu wa kijijini kwa mwaka mkoani Tibet kiliongezeka kwa mara tatu, wastani wa ukuaji wa kipato hicho kwa mwaka ulikuwa asilimia 12.5. Tangu mwaka 2015, kiwango cha ukuaji wa kipato cha watu wa vijijini mkoani Tibet kimeshika nafasi ya kwanza kati ya mikoa yote nchini China kwa miaka sita mfululizo.
Dini ni suala lingine linalofuatiliwa zaidi mkoani Tibet. Kabla ya kupinduliwa kwa mfumo wa watwana wa kilimo, makabaila walitumia dini kudhibiti mawazo ya watwana, na kuwanyima haki zao zote, hata kuwaua hovyo. Katika majumba ya makumbusho mkoani Tibet, bado kuna vyombo vya kidini vilivyotengenezwa kwa mafuvu, ngozi na mifupa ya watwana waliouawa, jambo ambalo ni la kutisha sana. Baada ya serikali kuu kukomesha mfumo wa watwana wa kilimo, ilitoa katiba na sheria zilizolinda uhuru wa kuabudu, na watu wa Tibet walianza kufurahia imani ya dini kihalisi. Hivi sasa kuna zaidi ya mahekalu 1,700 kwa ajili ya shughuli za kidini mkoani Tibet, pamoja na sufii zaidi ya 46,000. Ili kukuza elimu ya dini, Shirikisho la Dini ya Kibuddha la China pia ilianzisha Chuo cha Buddha cha Tibet huko Lhasa, ambacho kinatoa mafunzo kwa watu wanaoamini dini ya kibuddha.