Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, imesitisha usikilizwaji wa shauri la kinidhamu lililofunguliwa dhidi ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, katika Kamati ya Maadili ya Mawakili. Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji linaloongozwa na Jaji Amir Mruma, likielekeza kuwa hatua za shauri hilo zisubiri uamuzi wa shauri la msingi la kikatiba linalohusiana na mamlaka na mfumo wa kisheria unaosimamia kamati hiyo.
Hatua hiyo inafuatia shauri la kikatiba lililofunguliwa na Mwabukusi kupinga uhalali wa baadhi ya vipengele vya sheria vinavyosimamia Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, mahakama imeamua suala hilo la kikatiba lishughulikiwe kwanza kabla ya kuendelea na mchakato wa kinidhamu dhidi yake.