PostGE2025 Mahakama Kuu Kigoma yakataa kusimamisha Kesi ya Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini

PostGE2025 Mahakama Kuu Kigoma yakataa kusimamisha Kesi ya Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

Makumbele

JF-Expert Member
Joined
May 9, 2009
Posts
312
Reaction score
1,433
Tarehe 9, Januari 2026

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, imetupilia mbali ombi la Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali la kutaka kusimamisha usikilizwaji wa kesi ya kupinga matokeo ya ubunge katika jimbo hilo.

Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji V.M. Nongwa katika Shauri la Uchaguzi Namba 28949 la mwaka 2025, lililofunguliwa na Johary K. Kabourou na wenzake watatu dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi, Clayton Revocatus Chipando (Mbunge aliyetangazwa), na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kiini cha Mvutano

Mvutano wa kisheria uliibuka baada ya Mawakili wa Serikali, wakiongozwa na Mark Mulwambo, kuiarifu Mahakama kuwa wamewasilisha taarifa ya kukata rufaa (Notice of Appeal) Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi mdogo uliotolewa awali na Mahakama hiyo wa kutupilia mbali pingamizi lao la awali.

Wakili Mulwambo alidai kuwa kwa mujibu wa sheria, kuwepo kwa taarifa hiyo ya rufaa kunatosha kusimamisha shughuli zote za shauri hilo katika Mahakama Kuu hadi hapo Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi. Alirejea kesi mbalimbali kusisitiza kuwa Mahakama Kuu inakosa mamlaka ya kuendelea pindi rufaa inapofunguliwa.

Hata hivyo, Wakili wa Walalamikaji, Bwana John Seka, alipinga vikali hoja hiyo. Alisema sheria ya Mamlaka ya Rufani inakataza kukata rufaa dhidi ya maamuzi ambayo hayamalizi shauri la msingi.

Wakili Seka alionya kuwa kuahirisha shauri hilo kwa muda usiojulikana kungesababisha kesi hiyo kufa kisheria (by operation of law), kwani sheria inataka mashauri ya uchaguzi kumalizika ndani ya miezi sita.

"Wahenga wanasema usitukane wakunga na uzazi ungalipo," alisema Wakili Seka, akisisitiza kuwa haki ya kukata rufaa ipo baada ya hukumu ya mwisho na kwamba hatua ya sasa ni kupoteza muda.

Uamuzi wa Jaji

Akisoma uamuzi wake, Jaji Nongwa amekubaliana na hoja za Walalamikaji kwamba si kila uamuzi katika kesi za uchaguzi unaweza kukatiwa rufaa.

Jaji alirejea Ibara ya 83(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kesi ya Freeman Aikael Mbowe dhidi ya Alex O. Lema, akifafanua kuwa haki ya kukata rufaa katika mashauri ya uchaguzi ipo tu pale ambapo Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa mwisho unaohusu uhalali wa mtu kuchaguliwa au kukoma kwa ubunge.

"Uamuzi ambao haumalizi shauri huwezi kukatiwa rufaa," alisema Jaji Nongwa.

Jaji alisisitiza kuwa mashauri ya uchaguzi yana muda maalumu wa kisheria (miezi sita) na yanagusa maslahi ya umma, hivyo hayapaswi kucheleweshwa kwa rufaa za maamuzi madogo (interlocutory orders).

"Kwa uamuzi huu, maombi ya kusimamisha usikilizaji wa shauri hili kwa muda usio na kikomo, nayakataa na shauri litaendelea kwa hatua ya usikilizaji wa awali kama ilivyokuwa imepangwa," alihitimisha Jaji Nongwa.

Kinachoendelea

Kufuatia uamuzi huu, kesi hiyo itaendelea katika hatua ya usikilizwaji wa awali (Preliminary Hearing) ili kuweka sawa masuala yanayobishaniwa kabla ya ushahidi kuanza kutolewa.

Walalamikaji katika kesi hiyo wanapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025, wakidai kuwepo kwa kasoro katika kampeni na taratibu za siku ya uchaguzi, na wanaiomba Mahakama kubatilisha matokeo hayo na kuamuru uchaguzi mdogo ufanyike.
 

Attachments

ni kweli jaji hajakosea huwezi kukatia rufaa uamuzi mdogo ambao haumalizi kesi, hii inajumuisha vitu hata temporary injunctions.
 
Back
Top Bottom